Wasomi wanavyouchambua utafiti wa Twaweza kuhusu kiu ya kumkosoa Rais

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza, Dar es Salaam jana wakati wa uwasilishaji wa tafiti iliyofanywa na Taasisi ta Twaweza kuhusu mtazamo wa wazazi kuhusu lugha gani itumike kufundishia Shuleni. Katikati ni Mkurugenzi wa Udhibiti na ubora wa Elimu nchini, Marystella Wassena na Profesa Kitila Mkumbo kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanyika mwaka 2017, asilimia 81 ya Watanzania wanaamini kwamba kupitia ukosoaji huo wanaweza kuisaidia Serikali kutofanya makosa.

Hivi karibuni taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti wake kuhusu uhuru wa maoni ikibainisha kuwa watu nane kati ya 10 (asilimia 80) wanataka kuikosoa Serikali na Rais kwa kufanya uamuzi mbaya na kutosikiliza ushauri.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanyika mwaka 2017, asilimia 81 ya Watanzania wanaamini kwamba kupitia ukosoaji huo wanaweza kuisaidia Serikali kutofanya makosa.

Utafiti huo umebaini kwamba idadi kubwa ya wananchi hawajisikii huru kumkosoa Rais (asilimia 60), Makamu wa Rais (asilimia 54) na Waziri Mkuu (asilimia 51). Hata hivyo, idadi kubwa ya wananchi wanasema wanapaswa kuwa huru kuikosoa Serikali na Rais kwa kufanya maamuzi mabaya na kutosikiliza ushauri (asilimia 80),” anasema Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze.

Hata hivyo, mara baada ya utafiti huo kuwekwa bayana, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Dk Hassan Abass akasema Rais ni mtu mkubwa kiasi ambacho kumshauri kunahitaji utafiti.

Dk Abass anasema kuna mtu anadhani kukosoa ni kufanya chochote ikiwamo kutukana na kumdhalilisha mtu mwingine.

Dk Abass alienda mbali zaidi na kutoa mfano wa nadharia ya Ubuntu kutoka Kusini mwa Afrika, Dk Abass akisema kuna ngazi za kumshauri Rais zinazofanana na heshima katika familia.

“Sisi kwenye mambo ya media tunatumia theory inaitwa Ubuntu, inaeleza levels (ngazi) jinsi ya kumkosoa mtu hata katika familia, baba au kaka wakikosea, kaka unaweza kumwambia lile neno letu kwamba ‘umebugi’ lakini baba kuna namna ya kumwambia,” anasisitiza.

Dk Abass anaongeza, “Mimi kama mshauri mmoja wapo wa Rais, namshauri kila siku na anasikiliza. Wewe umemshauri wapi? Rais ana power (nguvu), anaweza kuwa na taarifa nyingi

Wakati Dk Abass akisema hayo, wachambuzi wa masuala ya siasa wanaungana na ripoti ya utafiti huo wakisema upo umuhimu wa wananchi kupata uhuru wa kuzungumza ili kutoa mawazo yao.

Hata hivyo, wasomi na wachambuzi wa siasa wanasema ripoti hiyo imekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inahitaji mabadiliko makubwa katika mfumo wa siasa.

Wakati waziri wa zamani, Njelu Kasaka anasema suluhu ya mambo hayo ni Serikali kusikiliza wananchi, Msomi wa siasa, Profesa Mwesiga Baregu anamtaka Rais John Magufuli kupokea utafiti huo kwa moyo mkunjufu na mtazamo chanya.

Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anayaelezea matokeo ya utafiti huo kuwa yanaakisi hali halisi, ingawa anasema kitendo cha Twaweza kuingia mkataba na wahojiwa kina walakini.

“Kama methodolojia uliyotumia ni ileile, ni dhahiri kwamba kuna walakini. Ukiachilia mbali kwamba mmepata sampuli lakini mmeingia nao (wahojiwa) mikataba na mmewawezesha simu. Kwa hiyo, kama wahojiwa wanajua taarifa zao mnazo, inaweza kuathiri wanachokiamini,” anasema Dk Mbunda wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Wakati mhadhiri huyo akisema hayo kwa upande wake mwanaharakati na wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia anasema Watanzania wengi wana hofu ya kutoa maoni, “Sijajua ubora wa respondents (wahojiwa) wetu. Kwa sababu kama wametawaliwa na hofu, wana shaka, basi hakuna linalofanyika.”

Anaongeza “Utafiti ni mzuri lakini aina ya watu tuliowauliza hatujui wakoje, kwamba ni aina ya watu waliofundishwa kukaa kimya. Tangu shule za msingi tulifundishwa kukaa kimya.”

Akifafanua, Sungusia alisema jamii za Kiafrika, Tanzania ikiwamo zina utamaduni wa kifalme ambao hauruhusu kuwahoji viongozi.

“Utamaduni wetu unazungumzia mfalme, huwa hahojiwi, haulizwi swali. Sisi kama nchi za Afrika tumekuja kurithi demokrasia bila kuwa na misingi yake ya mwanzo.”

Aliitaja misingi hiyo kuwa ni demokrasia ya kimiundombinu, demokrasia ya kiufundi na demokrasia ya kisasa akisema Waafrika tuliruka hatua hizo na kuingia kwenye ile ya kisasa.

“Sasa sisi tumeruka hizo hatua tunakuja kuzungumzia uhuru wa maoni. Kwa jamii nyingine hiyo ni hatua ya mbele mno kwa tamaduni zetu.

Kuhusu utafiti

Kwa mujibu wa utafiti huo, licha ya wananchi wengi kuunga mkono kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa, asilimia 95 hawajawahi kuomba taarifa katika ofisi za Serikali; asilimia 93 hawajaomba taarifa kwenye mamlaka za maji; na asilimia 93 hawajawahi kuomba taarifa kwenye vituo vya afya.

Badala yake, utafiti huo ulibaini kuwa wananchi wameendelea kutegemea vyanzo vilevile vya taarifa hususan televisheni ambayo alisema utegemezi wake umepanda kutoka asilimia saba mwaka 2013 hadi asilimia 23 mwaka 2017.

Inasema imani kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka, redio imeshuka kutoka asilimia 80 mwaka 2016 hadi asilimia 64 mwaka 2017; runinga kutoka asilimia 73 mwaka 2016 hadi asilimia 69 mwaka 2017.

Pia, imani kwa maneno ya kuambiwa nayo inaelewa kushuka kutoka asilimia 27 mwaka 2016 hadi asilimia 13 mwaka 2017.

Utafiti huo pia unasema licha ya imani kushuka, alisema bado wananchi wanaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari na asilimia 62 wanapendekeza gazeti lililochapisha habari za uongo liombe radhi na kuchapisha marekebisho; huku asilimia 54 ya wananchi wakitaka Serikali ipate ridhaa ya mahakama kufanya uamuzi wa kuliadhibu gazeti.

Pia, unataja changamoto ya wananchi kutozijua sheria zinazohusu masuala ya habari na kuwa ni asilimia 10 tu wanaoijua Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015; huku asilimia nne tu ya wananchi wakiifahamu Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Wachambuzi wazungumza

Akizungumza nini kifanyike, Kasaka anasema Serikali haipaswi kuweka mazingira ya wananchi kushindwa kutoa maoni yao na kuikosoa.

Anasema badala yake inapaswa kusikiliza kila hoja inayotolewa iwe ya kupongezwa au kukosolewa kisha kutoa majibu yanayohusiana na maswali hayo.

Anaongeza kwa jambo la msingi ni baada ya kusikiliza na kujitathimini na kuona kwamba kuna ugumu wa utekelezaji huo wanapaswa kutoa ufafanuzi.

“Wanachosema wananchi si ugomvi wala dhambi na wakumbuke kwamba bila wao hakuna Serikali, hivyo watoe nafasi ilimradi hakuna anayevunja sheria maana hata katika haki kuna wajibu pia,” anaongeza Kasaka.

Kuhusu hoja kwamba huwezi kumkosoa Rais bila kufanya utafiti, waziri huyo wa zamani ambaye alikuwa katika kundi la G55 anasema hoja hiyo haina mashiko.

“Hivi mwananchi anahitaji utafiti wa nini ili toe mtazamo wake wa masuala yanayomhusu ambayo yamemzunguka katika maisha yake. uwaache watoe mawazo, viongozi kazi yetu kutoa mrejesho wa hoja hizo,” anasisitiza Kasaka.

Kwa upande wake Profesa Baregu, utafiti huo ni muhimu sana kwa kipindi hiki ambacho Watanzania wanakipitia.

Baregu anasema kama labda kulikuwa na hisia kwamba Watanzania wanapenda kazi za Rais John Magufuli pekee kama kutumbua wabadhirifu na kubana matumizi sasa wamempa mrejesho kwamba pamoja na mazuri yote, lakini Serikali isipowasikiliza wananchi wake hakutakuwa na amani.

“Naamini ataipokea ripoti hiyo kwa moyo mkunjufu lakini pia kwa mtazamo chanya kwamba pamoja na yote anayofanya anachotakiwa sasa ni kuwasikiliza wananchi.

“Mimi naona anayesemwa ni yeye mwenyewe, hivyo ni vyema akaitafakari ripoti; mfano sasa wananchi wanaona vyuma vimekaza lakini yeye anasema vimelegea na wanapaswa kuweka grisi, Rais lazima uwaelewe wananchi wako,” anasisitiza Profesa Baregu ambaye pia ni mwanasiasa.

Anasema huu ni mrejesho mzuri, utafiti huo umetoa taswira ya hoja zilizokuwa zimebebwa na vyama vya upinzani wakilalamikia mambo kadhaa ikiwamo usawa katika kufanya siasa zao kulinganisha na chama tawala, lakini muda wote wamekosa fursa ya kusikilizwa, ni juu ya Rais kuchukua hatua katika kunusuru hali hiyo.

“Sasa wananchi wameamua kuwasaidia wapinzani kubeba ajenda yao ni muda muafaka sasa kwa Serikali kuona umuhimu wa kukutana nao na kuweka mambo sana, hatuwezi kwenda wakati wengine wanalalamika.”

Baregu anasema kiongozi hapaswi kubomoa madaraja kati ya watu anaowaongoza na badala yake anapaswa anayajenga yote na kuhakikisha yanapitika katika vipindi vyote vya msimu.

Anasema wananchi wana haki ya kuzungumza kwani hata Katiba imeruhusu uhuru wa maoni, hivyo kuwazuia kunaongeza chuki dhidi ya viongozi wao.