Uvuvi haramu na hatari ya kutoweka kwa Sangara Ziwa Victoria

Muktasari:

Katika utafiti huo wa ACCORD, unaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2048 kutakuwapo na upungufu mkubwa wa samaki katika ziwa hilo kwa kuwa uzalishaji wa samaki nchini umeshuka kwa asilimia 50, kutoka tani 400,000 hadi tani 200,000, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Mazingira katika Ziwa Victoria yameharibiwa na kusababisha aina nyingi za samaki kutoweka. Wavuvi haramu wameharibu mazingira kwa kutumia njia zisizokuwa salama wakati wa kuvua samaki.

Wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi, hawaogopi vyombo vya dola wala kujali usalama wa samaki katika ziwa hilo.

Vitendo vya uvuvi haramu vimechangia kupungua kwa samaki katika ziwa hilo kutokana na mazalia ya samaki kuharibiwa na sumu ama vifaa ambavyo havitakiwi katika uvuvi.

Kutokana na hali hiyo serikali na wadau wengine wanatafakari njia mbadala za kulinda mazingira katika ziwa hilo ili kunusuru maisha ya watu kuribu milioni 120 wanaotumia Ziwa Victoria kutoka Tanzania, Uganda, na Kenya.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Utafiti wa Mazingira la ACCORD –Tanzania, kuna hatari ya kutoweka kwa aina zote za samaki katika Ziwa Victoria zaidi ya miaka 30 ijayo, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na uvuvi haramu.

Samaki kutoweka Ziwa Victoria
Katika utafiti huo wa ACCORD, unaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2048 kutakuwapo na upungufu mkubwa wa samaki katika ziwa hilo kwa kuwa uzalishaji wa samaki nchini umeshuka kwa asilimia 50, kutoka tani 400,000 hadi tani 200,000, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Utafiti huo hauna tofauti na ule wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria ( LVFO), uliofanyika mwaka 2005, ukionyesha kwamba katika miaka 40 iliyopita, mpaka sasa, aina 200 za samaki wametoweka katika ziwa hilo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, miaka ya 1920, Ziwa Victoria lilikuwa na takribani aina 400 za samaki, lakini sasa kuna aina tatu pekee za samaki wanaovuliwa kwa ajili ya shughuli za  kibiashara ambao ni sangara, sato, na dagaa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe anasema samaki wanapungua katika Ziwa Victoria kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvuvi haramu.

Kanali Massawe anasema awali viwanda vya samaki mkoani Kagera ambavyo ni Vicfish na Kagera Fish vilichakata tani 45 za samaki kwa siku, lakini sasa vinachakata tani kumi tu, kiwango ambacho ni kidogo na kutishia viwanda hivyo kufungwa.

Ofisa Mfawidhi Kitengo cha Kukuza Viumbe Hai Majini, mkoani Kagera, Erick Kiiza anasema mkoa una mabwawa 241 ya kufugia samaki na kati ya hayo yanayomilikiwa na serikali ni matatu na mengine ni ya watu binafsi.

Hata hivyo ofisa huyo alishindwa kupata takwimu za samaki wanaozalishwa katika  mabwawa ya serikali na kiasi cha fedha kinachopatikana.

Wavuvi haramu 400 wakamatwa
Mkuu wa zamani wa kikosi cha doria katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera, Lodrick Mahimbali anasema doria zilizofanyika  mwaka 2009/2010 na mwaka 2010/2011, wavuvi haramu 476 walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mahimbali anasema kilo 23,047 za samaki aina ya sangara nasato kilo 8,716, na zana haramu zenye thamani ya Sh1.5 bilioni zilikamatwa na kuteketezwa kwa moto.

Zana haramu zilizokamatwa ni makokoro 503, timba 785, makila 12,965, nyavu za dagaa 293, mitumbwi ya kuvulia kokoro 495, kamba za kuvutia makokoro zenye urefu wa mita 192,274, na katuli nane.

Mahimbali anasema fedha zilizopatikana kutokana na faini katika mwaka 2009/2010 na mwaka 2010/2011, ni zaidi ya Sh37.7 milioni.

Eneo kubwa la ziwa hilo liko Mkoa wa Kagera kiasi cha kilometa za mraba 10,017. Shughuli nyingine za zinafanyika katika ziwa Burigi, Ikimba, Rushwa na Rumanyika na katika mito ya Kagera, Ngono, na Ruvuvu.

Mmoja wa wadau, Bushir Hussein Rashid (41) mkazi wa Kijiji Ruhanga, tarafa Kamachumu wilayani Muleba anasema ameamua kuanzisha shughuli za ufugaji samaki katika mabwawa kwa kushirikiana na mwenzake Julius Onesmo.

Bushir anasema wameamua kufuga samaki ili wawe mfano kwa vijana wengine wanaovua kwa kutumia zana haramu na kuharibu mazalia ya samaki.

Anasema mafunzo ya ufugaji ameyapata Kajanse nchini Uganda na Vietnam huku akidokeza kwamba alianza shughuli za uvuvi  mwaka 1986 baada ya kumaliza darasa la saba.

Bushir anasema baada ya kupata mafunzo hayo mwaka 2007, walianza kufuga samaki katika eneo la Kimwani la heka 60 na baadaye walihamishia shughuli za ufugaji Ruhanga lenye ukubwa wa heka 27 kutokana na Kimwani kuwa na upungufu wa maji .

Anasema kuwa katika eneo la Ruhanga kwa sasa kuna samaki aina ya Sato 20,000 na aina ya Kambale 6,000 na samaki hao ni mbegu zinazosubiri kuzalishwa.

Anabainisha kwamba walitumia mtaji wa kuvua samaki kuanzisha shughuli za kufuga samaki na kupata msaada kutoka serikalini ikiwamo kupimiwa eneo lao la ufugaji.

Wakati Bushir akivua samaki alikuwa akipata ujira Sh50,000 mpaka Sh100,000 kwa mwezi, lakini sasa anapata wastani wa faida ya Sh3.5 milioni baada ya kuondoa matumizi.
 
Jinsi mayai yanavyototolewa
Kuhusu namna ya kuzalisha samaki, anasema kutotoa mayai kunachukua saa 12 na baadaye mayai hayo yanawekwa kwenye tanki maalum na kukaa humo kwa saa 12 pia, na baada ya kutolewa mayai yanakaa siku 15 na kupata samaki wadogo.

Anasema kuna uzalishaji wa aina nne, na njia zote zina faida. Samaki mdogo kabisa aina ya sato anauzwa Sh300 wakati sato wakubwa mwenye kilo moja, anauzwa kati ya Sh2,500 mpaka Sh4,000.

Samaki mdogo aina ya kambale, mmoja anauzwa Sh80 mpaka Sh120 na  kambale mkubwa anauzwa Sh5,000 mpaka Sh10,000 kutegemeana na ukubwa wa samaki.

Kwa kawaida samaki wadogo aina ya kambale wanatumika kama chambo cha kunasia samaki katika ziwani. Pia Kambale wanane wanaweza kuzalisha kambale wadogo 500,000 hadi milioni moja kwa mwezi.

Pamoja na mafanikio hayo wamejipanga kuwa na mabwawa 36 ili wavune samaki aina ya sato 700 kwa siku kwa ajili ya kitoweo kwa wananchi na kusambaza samaki wadogo aina ya sato 10,000 kila mwezi.

Kwa upande wa samaki aina ya kambale, wamelenga kuuza samaki 200 kwa siku na kuuza samaki wadogo milioni moja kwa siku 60.

Wafugaji hao wanataka kutumia mradi huo kutoa mafunzo kwa watu wengine ili wajifunze jinsi ya kufuga samaki na kuinua kipato chao.

“Tunataka kujenga maabara, hosteli kwa ajili ya watakaokuja kujifunza, na soko la samaki kwa ajili ya wananchi,”anasema.