Shetta: Ukiyapatia maisha utazushiwa kila jambo baya

Muktasari:

Ni mwanamuziki maarufu aliyeibuka baada ya kuachia wimbo wenye mashairi tata “Nidanganye” akimshirikisha supastaa, Diamond Platnumz. Baadaye aliachia nyimbo kama Mama Qayla, Kerewa na sasa anatamba na wimbo Namjua.

Starehe limefanya mahojiano na Shetta aliyetambulisha uongozi wake mpya hivi akiwamo meneja na mlinzi mmoja.

Nurdin Bilal ndiyo jina lililopo katika hati ya kusafiria, vyeti vya shule, leseni na vitambulisho vingine lakini la kutafutia ugali ni Shetta.

Ni mwanamuziki maarufu aliyeibuka baada ya kuachia wimbo wenye mashairi tata “Nidanganye” akimshirikisha supastaa, Diamond Platnumz. Baadaye aliachia nyimbo kama Mama Qayla, Kerewa na sasa anatamba na wimbo Namjua.

Starehe limefanya mahojiano na Shetta aliyetambulisha uongozi wake mpya hivi akiwamo meneja na mlinzi mmoja.

Ulitumia kiasi gani cha fedha kutambulisha uongozi wako mpya?

Unajua ile shughuli ilisimamiwa na Heinessy kwa hiyo kuna vitu walikuwa wanafanya wao na kuna vitu tulivifanya sisi, kwa hiyo inakuwa vigumu kidogo kutaja kiasi cha fedha ambacho kilitumika. Bado kuifikiria, lakini haiwezi kupungua chini ya Sh27 milioni.

Video ya Namjua ulitumia kiasi gani cha fedha kuikamilisha?

Mara nyingi huwa sipendi kutaja gharama za video au audio ninazozitumia, awali niliwahi kutaja lakini ikawa inasababisha mambo mengi sana, huwa napenda kwa mfano mtu akitaka kujua gharama inatakiwa kuacha tu sababu inajenga maneno mengi, mtu unaweza kutaja kwa nia nzuri tu, lakini ikawa vinginevyo.

Video ya wimbo Namjua inafanana na “My Number One” ya Harmonize “Bado” kwanini imetokea hivyo?

Hazifanani. Nafikiri kutumia boti na ndege ambazo kwenye Number One na huko kwa Harmonize vimetumika, lakini inategemea inatumikaje kwa sababu katika video nyingi imetumika na inategemea inatumikaje, kwangu nimetumia kivingine na Diamond pia kivingine hakuna ufanano kabisa.

Mpaka sasa una nyimbo ngapi ambazo umerekodi?

Nyimbo nilizowahi kurekodi ni nyingi, kwa mfano nikiachia wimbo mmoja. Mpaka sasa nimeachia nyimbo 11 na nyingine tatu zilizovuja kwa hiyo jumla yake ni nyimbo 14 zipo mtaani. Mimi huwa sipendi kuachia nyimbo kila wakati, nimerekodi nyimbo nyingi sana sina idadi kamili.

Nini kinakuboa kwenye kolabo? Umeshawahi kukataa kolabo?

Huwa sikatai kolabo kwanza kwa sababu hata mimi nimetoka huko hasa kwa wasanii wachanga lazima niwasikilize na nifanye nao kazi vizuri. Ila kinachoniboa ni sipendagi kukutana na mtu ambaye nampa nafasi halafu kipaji hana huwa naenjoy sana ninapokutana na mtu ambaye ninampa nafasi na yeye ananipa nafasi nzuri pia nafurahi kwa kuwa ninampenda mtu mwenye kipaji.

Muziki umekufanyia nini?

Vitu vingi sana, mabadiliko ya kimaisha unajua ukiwa maarufu unapata utajiri mwingi ukiachilia mbali fedha, biashara, kuanzia mwaka 2009 kurudi nyuma Shetta ni mtu mwingine kabisa mafanikio yapo ya kimaisha pia.

Vipi kuhusu shoo zinapatikana? Ndani na nje ya nchi?

Za kutosha kwa mfano nimetoa wimbo “Namjua”, nimefanikiwa kupata shoo mbili na baada ya Ramadhani naamini kwamba tutakuwa bize sana na shoo kwa sasa tumepumzika kidogo.

Vipi kuhusu masuala ya mirabaha, umewahi kuitwa na kupewa kitita chako?

Bado naona kama hazijaanza kufanyika kwa sababu sidhani kama kuna mtu ameitwa kwa ajili ya hiyo ni kitu kizuri, lakini sijaona kama kimeanza kufanya kazi yoyote.

Shughuli gani nyingine unafanya mbali ya muziki?

Mimi ni mfanyabiashara ndogondogo, maisha yanaenda kwa hiyo vitu vingi na ndivyo vinavyosababisha Quaylah aende shule na maisha yanakwenda.

Kwanini umeamua kuwa na baunsa?

Ulinzi ni muhimu sana, sehemu yoyote kwenye mazingira ya watu wengi mara nyingi sijui nani anakuja, nani mzuri au mbaya, sehemu yoyote ambayo ninahisi kwamba usalama wangu utakuwa mdogo nahitaji kujilinda.

Unaweza kuoa mke mwingine?

Hapana siwezi kabisa na wala sifikirii kabisa na si kuoa tu hata kuzaa na mwanamke tofauti.

Una ugomvi wowote na Diamond? Kuhusu ishu ya kukuchukulia mkeo Mama Quaylah ni kweli?

Kama unanifuata Instagram au Diamond utagundua kwamba si kweli. Wakati mwingine kila mtu anaongea kitu ambacho anajisikia kuongea na hayawezi kutusababisha tuwe tofauti. Ukiwa staa vitu kama hivyo ni kawaida na ukishaanza kuvisikia na kuendelea kuvisikia haviumi wala nini.

Mara nyingi umekuwa ukihusishwa na biashara ya dawa za kulevya, ukweli wake ukoje?

Sipendi kulizungumzia hilo kwa sababu halina maana kwangu. Unajua tena ukishaanza kupata riziki kila baya utazushiwa.