Ukiishi Mbeya umasikini ni wa kujitakia

Wakulima wa mpunga wakisafirisha magunia kwa kutumia pawertiller. Hili ni zao mojawapo linaloweza kuwatoa wakazi wa Mbeya kutoka kwenye umskini. Picha na Geodfrey Kahango

Muktasari:

Kwa hali ilivyo, ni miongoni mwa mikoa michache inayoweza kukumbwa na baa la njaa, kwani una mazao ya aina nyingi yanayolimwa na kuvunwa kwa nyakati tofauti na kutoa fursa za kuwapo kwa kipato wakati wote.

Mkoa wa Mbeya unatajwa kwa jina la utani la ‘The Green City’ yaani mji wa kijani, kutokana na kubarikiwa mvua nyingi inayoifanya mimea mingi kubakia katika hali ya kijani kibichi karibu kipindi chote cha mwaka.

Kwa hali ilivyo, ni miongoni mwa mikoa michache inayoweza kukumbwa na baa la njaa, kwani una mazao ya aina nyingi yanayolimwa na kuvunwa kwa nyakati tofauti na kutoa fursa za kuwapo kwa kipato wakati wote.

Mkoa una eneo la kilometa za mraba 35,960 zilizogawanywa katika wilaya tano na halmashauri saba ukiwa na tarafa 15, kata 178 na vijiji 533 pamoja na mitaa 216.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla anasema watu wanaoamini walizaliwa wakiwa masikini na wanaoendelea kushikilia mawazo hayo, ndiyo watakaobaki na umasikini mkoani mwake.

Kwa nini? Anasema mkoa wake umezungukwa na fursa nyingi za kiuchumi ambazo mpaka sasa hazitumiki na zingine hazijaibuliwa. Mojawapo ya fursa hizi ni zile zinazopatikana kwenye sekta za kilimo na ufugaji.

Fursa za kiuchumi

Wengi wanaamini kwamba ukitaka kuwa mmoja wa matajiri Mbeya, unaweza kufanikiwa kama utaamua kwa akili, nguvu na moyo wote kufanya kile kilichopangwa mbele yako.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye viwanda na Kilimo (TCCIA) Dk Lwitiko Mwakalukwa anasema fursa kubwa za uchumi zinapatikana kupitia kilimo, ufugaji,

Kwa mujibu wa takwimu za pato la mkoa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hivi sasa pato la mkoa limepanda kutoka Sh2.352 trilioni mwaka 2008, hadi Sh6.761 trilioni kwa mwaka 2015.

Wastani wa pato la mtu binafsi limeongezeka kutoka Sh940,310 mwaka 2008 hadi Sh2.3 milioni mwaka 2015.

Dk Mwakalukwa ambaye ni ofisa mifugo mstaafu, anasema Mbeya ni maarufu kwa kilimo cha mazao ya chakula ambayo yanahitaji fursa za kujengwa viwanda vya kuyasindika.

Miongoni mwa mazao hayo ni mpunga, mahindi ndizi, maharage, njugu, ngano, kunde, njegere, machungwa, matikiti maji, na mazao ya viungo vya aina mbalimbali hususan nyanya, vitunguu, pilipili, tangawizi, bizari, iriki na hata bamia.

Aidha, anaeleza kuwa mkoa una fursa kubwa ya kilimo cha umwagiliaji katika mabonde ya Usangu na Kyela.

Anataja fursa kwa mazao ya biashara kuwa ni pamoja na chai, kahawa, cocoa, chikichi, tumbaku na upandaji wa miti ya mbao, huku fursa za viwanda vya kusindika mazao hayo zikihitajika zaidi.

Kwa hali hiyo ipo fursa kubwa ya kuanzishwa kwa viwanda vya pembejeo, mbolea, na dawa za mimea kwa mifugo.

Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia kilimo, Nyasebwa Chimagu anasema mkoa una eneo kubwa linalofaa kwa kilimo, lakini mwaka 2015/16 eneo lililolimwa lilifikia hekta 549,801

ambazo zilitoa mavuno ya karibu tani 3.79 milioni wakati mahitaji ya chakula ni tani 512,564 kwa mwaka.

Anasema mazao ya biashara mwaka 2015/16 yalilimwa katika eneo la hekta 101,760 na mazao yaliyovunwa hadi Juni yalikuwa tani 109,267 sawa na asilimia 89 ya malengo.

Mkoa una miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali na pia unatekeleza mradi wa kujenga na kukarabati maghala ya mahindi na mpunga katika halmashauri za Mbeya, Mbarali na Kyela.

Fursa za ufugaji

Mkoa hauko nyuma katika masuala ya ufugaji kwani una jumla ya mifugo 3,095,116 wakiwamo ng’ombe 653,304, mbuzi 195,569 na pia una mabwawa 1,179 ya kufuga samaki.

Hata hivyo licha ya kuwapo mito mingi inayoingia kwenye Ziwa Nyasa na mabwawa ya asili yakiwa na samaki mpaka sasa mkoa hauna kiwanda cha nyama wala samaki.

Masoko ya ndani

Pamoja na Mkoa wa Mbeya kuwa na mazao ya aina nyingi, lakini mpaka sasa una masoko 49 na magulio 35 ambayo nayo yanatumiwa na wachache . Ipo fursa kubwa ya kuongeza masoko yanayoweza kutumika kama fursa za kuuza na kununua bidhaa mbalimbali.

Usafirishaji

Katibu Tawala, Mariam Mtunguja anasema Mkoa wa Mbeya umejaliwa kwa barabara nyingi za lami zinazounganisha karibu wilaya zake zote.

Ubora wa barabara hata za wilayani unasababisha kuwapo usafiri wa kutosha wa mabasi kuelekea wilaya mbalimbali ya mkoa kama wilaya za Kyela, Rungwe na Mbarali.

Mkoa pia umepitiwa na reli ya Tazara ambayo inatoa fursa ya kusafirisha mizigo kutoka na kwenda mikoa ya Pwani na nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Zambia.

Hali kadhalika mkoa unacho Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Songwe (Sia) kilichopo kilometa 20 kutoka katikati ya Jiji la Mbeya.

Kiwanja hicho kina uwezo wa kupokea ndege kubwa, jambo ambalo sasa linatoa fursa kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji kufika hapa bila wasiwasi.

Changamoto

Pamoja na mazingira bora ya kiasili yanayoweza kuwavutia Watanzania kuingia kwenye sekta ya kilimo na ufugaji, baadhi ya wadau wanaojihusisha na kilimo kwa sasa wanasema kilimo bado kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa soko.

Mkulima wa mpunga wilayani Mbarali Uswege Kyaniki anasema wakulima wengi wanabaki na mazao majumbani kwa kipindi kirefu kutokana na kukosa soko la uhakika,.

“Kwa bahati nzuri wengine wanapata masoko nchi za Malawi au Zambia, lakini Serikali inazuia kuuzwa mazao hayo jambo ambalo ni kero’’ anaeleza.

Kero inayotajwa na Kyaniki haina budi kufanyiwa kazi na kina Makalla na hata viongozi wa Taifa.

Haitoshi kutoa sifa kedekede za mkoa, ikiwa wanaojitokeza kuzifanyia kazi fursa za kiuchumi wanalia kukwazwa ikiwamo kuzuiwa kuuza mazao yao maeneo yenye soko.

Tuwahimize Watanzania wajikite kwenye kilimo, lakini tufungue milango ya mazao yao kuuzwa kwenye masoko ya ushindani. Kinyume na hapo Mbeya utabaki mji wa kijani, lakini usio na manufaa kwa wakazi wake na nchi kwa jumla.