Tufanye siasa za maendeleo kwa wote kwenye uchaguzi mdogo

Muktasari:

  • Yawezekana pia tukaweka msingi mpya wa kuwa wanasiasa. Kupenda siasa. Kufanya siasa na kuhakikisha fani hiyo inatoa dira ya Taifa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ratiba ya uchaguzi wa marudio utakaofanyika Januari 22, 2017.

Yawezekana siasa zitapewa sura mpya mwaka huu. Pia, tutaachana na siasa chafu, zenye ‘majitaka’ kama tulivyozoea kuziita.

Yawezekana pia tukaweka msingi mpya wa kuwa wanasiasa. Kupenda siasa. Kufanya siasa na kuhakikisha fani hiyo inatoa dira ya Taifa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

Neno siasa linaashiria mambo yanayohusu jamii. Kwa ufupi hii ndiyo maana ya siasa. Maana hii fupi hata hivyo inabeba taswira nzima ya jamii: Uchumi, elimu, mfumo wa haki na sheria, mgawanyo wa mali wa jamii husika, utamaduni, mazoea, imani ama dini, uhusiano wa ndani na nje ya jamii husika.

Kumbe siasa inahusu maisha ya wanadamu na wanasiasa ni watu wanaojishughulisha na mambo ya jamii. Ni watu wanaokerwa na kasoro katika jamii na wanakuwa na nia ya kutaka kushiriki kutafuta ufumbuzi wake. Ni aina ya watu wenye wito na taaluma ya sayansi ya jamii, sayansi ya siasa zenyewe na matokeo yake kwa jamii.

Aidha, kuna siasa za aina nyingi na wanasiasa inaonekana wapo kila mahali. Ukitembelea taasisi yoyote ama kundi la watu, unakuta watu wanazungumza siasa za eneo lao; yaani wanazungumza mambo ya ustawi wao katika eneo husika.

Siasa huanzia nyumbani

Mume na mke huweka utaratibu wao wa kuishi pamoja, huweka mambo yanayowahusu na utaratibu wa kuyafikia, kama vile kuleta familia na kuilea. Mmoja akivunja masharti husababisha taasisi kupoteza kusudi la awali la kuundwa kwake.

Siasa za nyumbani huhamia kwa jirani na kwa makundi mengine ya jamii kama vile taasisi za wafanyabiashara, wachimbaji, wakusanyaji na wawindaji.

Pia, siasa za wakulima na wafugaji zinaonyesha dhahiri kuvunjika kwa mkataba wa amani kati yao na kusababisha kukosekana kwa uvumilivu wa Kitanzania wa kuzungumza kunapotokea hitilafu za uhusiano katika jamii.

Siasa za wanawake, watoto, wazee, wenye ulemavu na maumbile tofauti zimewaweka hawa katika makundi maalumu dhaifu katika jamii. Yote haya ni kuonyesha athari za dhana ya siasa na jinsi kila mtu na kila kiumbe katika nafasi yake hujihusisha na siasa kwa njia moja ama nyingine.

Tanzania vyama vya upinzani vinapambana na chama tawala kila kimoja kikitaka kushika nafasi ya uongozi kuanzia wa chini wa mitaa na vijiji hadi urais kitaifa. Hizo ndizo siasa zinazozungumwa kama chafu, siasa maji taka zinazotumika wakati wa kampeni.

Kwa kuwa mazingira yote ya maisha yana ladha za kisiasa, tunahitaji kuhakikisha siasa zinatujenga, zinatuunganisha, zinatuelimisha, zinatukosoa na kuturekebisha na kwa hiyo siasa zitaonya, zitaelekeza, zitazuia na kuruhusu jambo jingine.

Siasa ya aina hii haiwezi kuwa siasa chafu, haiwezi kuwa ulaghai ama uganga njaa. Haiwezi kujitafutia mambo yake binafsi na haiwezi kuwa uongo. Kwa sababu hii kampeni za uchaguzi ulioko mbele yetu zitupe sura hii ya vyama vya siasa kuweka wagombea watakaouza sera na siasa za masuala ya jamii.

Maisha yamekuwa na changamoto nyingi na wanasiasa wanapaswa kuisaidia jamii kupata mwelekeo kutokana na kazi zao na hasa wakati huu wa kuuza wagombea.

Kwa hiyo, wapigakura tutegemee mijadala mikali juu ya itikadi za vyama na jinsi zinavyotutaka tukipe chama fulani kura na siyo kingine kwa ushawishi kuwa itikadi yetu hii inaweza kulifikisha Taifa hatua moja mbele.

Vyama vya siasa na wagombea wao vituambie vinataka kutufanyia nini kwenye uchumi. Kuwa vitafanya nini kuhakikisha uchumi unakua na unaonekana kukua katika maisha ya kawaida ya Mtanzania.

Kwamba kwa mfano chama kimejipanga vipi kudhibiti rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali na ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi ya dawa za kulevya kama mtandao unaotengeneza fedha haramu kwenye mzunguko wa uchumi na unaohusisha rushwa kubwa.

Vyama vituambie vipaumbele vyao katika uendeshaji wa halmashauri  na changamoto za huduma za jamii. Watatumia mfumo gani kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ubora na unafuu ama bure kabisa kwa wananchi; kwa mfano elimu bure inapatikanaje? Afya na maji ni bidhaa muhimu kwa maisha ya kila raia.

Kufanyia biashara huduma hizi kama ilivyo sasa ni dalili kuwa hakuna uwiano wa makusanyo ya kodi na matumizi yake kwamba kama tunalipa kodi kwa kila bidhaa tunayonunua, kisha tunalipia huduma hizi muhimu, ni nini maana ya kodi halisi na kodi ya ziada kwa kila bidhaa.

Kwa nini mfanyakazi, mfanyabiashara, mkulima na mfugaji analipa kodi kwenye shughuli yake, kisha analipa kodi kwenye kila bidhaa anayonunua?

Vyama vije na hoja hizi na vitusaidie kuchambua unafuu wa chama kimoja na kingine kuwafikia wananchi. Vyama vituambie uhalali na faida ya kuwapa wageni rasilimali za Taifa na hasara zake kama wangepewa wazawa.

Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa hivi karibuni juu ya mikopo ya wanafunzi na suala zima la elimu kwa watoto na watu wazima wanaotaka kujiendeleza.

Vyama vya upinzani vije na njia mbadala juu ya sekta hii muhimu. Elimu ndiyo njia pekee ya kuandaa nguvu kazi ya umma.

Tukiwanyima wanafunzi mikopo maana yake tunajinyima fursa ya kujiandalia nguvu kazi hii. Tuwaambie wananchi tuna mpango gani na utaratibu wa kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya umma haisimami.

Ni lazima tuhakikishe inapatikana wakati wote.

Migogoro kati ya wakulima na wafugaji imezidi hadi kufikia kiwango cha kuua uzalendo na undugu ambao ni nguzo kuu za Taifa letu.

Tufanye nini kuhakikisha migogoro hii inaisha? Kwa nini hatufikii suluhu ya tatizo hili kwa sasa? Wakulima wenyewe na wafugaji wanasema nini juu ya hili? Na juu ya kila changamoto inayoikabili taifa katika kila eneo husika.

Siasa ni tasnia inayojihusisha na maisha ya watu. Kila mwanasiasa na kila chama cha siasa kituonyeshe kiwango kinachoguswa na maisha ya watu katika kila eneo la uchaguzi kama sababu ya msingi ya kuweka mgombea katika eneo husika.

Siasa za aina hii ziwe kichocheo cha maboresho ya mfumo wetu wa uendeshaji siasa nchini. Wanasiasa na raia wapende kujua siasa za utawala, kama tunavyojitahidi kujua siasa za nyumbani na za shughuli zetu mbalimbali.

Niwatakie wote Salaam za amani, umoja, mshikamano unaopatikana kutokana na uendeshaji wa siasa safi kama moja ya nguzo kuu za utawala bora. Kwaheri mwaka 2016 karibu mwaka 2017. Uje na mwamko wa Siasa za masuala ya jamii. Amina.

Anna Mghwira ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT – Wazalendo na aliyekuwa mgombea urais wake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Anapatikana: [email protected]