Ndoto zake zazimika baada ya kuvunjwa mgongo, shingo

Muktasari:

Ilikuwa ni siku moja tu baada ya sikukuu ya Krismas ya mwaka 2011. Mishaly, alikuwa akitoka kazini kwake yeye wakati huo akiwa muuguzi katika Hospitali ya Dk Joseph Bakes iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Ni miaka mitano sasa tangu Mishaly Sumary (29), muuguzi wa zamani katika Hospitali ya Dk Bakes iliyopo Kibaha, alipopata tatizo la mfadhaiko wa viungo na kumsababishia kuishi kwa tabu huku ndoto zake zikitoweka.

Ilikuwa ni siku moja tu baada ya sikukuu ya Krismas ya mwaka 2011. Mishaly, alikuwa akitoka kazini kwake yeye wakati huo akiwa muuguzi katika Hospitali ya Dk Joseph Bakes iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Saa moja na nusu jioni, alipigiwa simu na dada wa rafiki yake ambaye alikuwa akihitaji ushauri. Walikubaliana wakutane katika eneo la lango kuu Kibaha. Mazungumzo yao yalipomalizika, Mishaly alitaka kuchukua usafiri wa bodaboda ili umuwahishe nyumbani kwake. Lakini rafiki yake alimshauri atembee kwa miguu kwa kuwa usiku haukuwa mwingi.

Mishaly, aliukubali ushauri ule na akaanza kuchepuka akielekea nyumbani kwake.

Dakika takriban 10 baada ya kuagana na rafiki yake, Mishaly alisikia kishindo cha watu nyuma yake. Ghafla aliwaona wanaume wawili wakimwendea kwa kasi. Walimkaba, mmoja akimshika miguu na mwingine akiikamata shingo yake.

“Nilijaribu kupiga kelele, lakini mmoja wao alinikaba shingoni, nilijitahidi kupigana nao lakini haikuwa kazi rahisi,” anasema Mishaly.

Wanaume wale walimwambia: “Sali sala yako ya mwisho,” lakini Mishaly aliendelea kujitetea kwa kurusha miguu.

Walitaka kumrushia katika kisima cha Dawasco kilichopo karibu na eneo hilo, lakini wakaghairi. Walipoona anajitetea kwa nguvu, mmoja akaikunja mikono yake kwa nyuma …akaweka goti katikati ya mgongo na kumvunja kama mtu avunjavyo kuni.

“Nilipiga kelele kwa maumivu makali niliyoyapata, nikasikia watu wanakimbilia katika lile eneo, nikawasikia wale wanaume wakisema, maliza kazi tusiuze gazeti,” anasimulia Mishaly.

“Mwishoni, mmoja wa wanaume wale alichukua chuma bapa chenye urefu wa sentimita kama 50 na kunipiga

nacho mdomoni ambacho kilivunja meno mawili na kunipasua mdomo sehemu ya chini,” anasimulia Mishely.

Wakati huo huo, mwanamme mwingine aliishika shingo na kuizungusha kama mtu anayekamua nguo. “Watu walianza kujaa katika lile eneo, aliyenivunja shingo akakimbia, lakini nikamshika shati yule wa mbele aliyenipiga na chuma,” anasema.

Katika kujaribu kukimbia, kijana aliyeshikwa shati alimng’ata Mishaly mdomoni. Alimng’ata kwa nguvu kiasi kwamba meno yalipenyeza ndani ya mdomo. Baada ya kumng’ata alivua shati lake na kukimbilia katika vichaka.

Je, ni kisasi?

Hadi hii leo Mishaly hafahamu nini lilikuwa kusudio la wavamizi wale waliomvunjia ndoto zake.

“Sikuwa na ugomvi na mtu, sifahamu kwanini walinivamia na kuniumiza karibu waniue, inaonyesha nia yao ilikuwa wanimalize kabisa. Hadi sasa watu wale hawajakamatwa na hakuna kesi yoyote iliyofunguliwa,” anasema Mishaly.

Apelekwa hospitali

Akiwa na maumivu makali Mishaly alipelekwa polisi na wasamaria wema ili kupata PF3 kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

“Nilikimbizwa katika hospitali ya Tumbi nikalazwa. Kwa kuwa hali ilikuwa mbaya nikapewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ila sikupatiwa huduma kwa kuwa nilikutana na mgomo wa madaktari,” anasema.

Baada ya kukaa muda mrefu Muhimbili bila kupata huduma stahiki sehemu ya mwili wake iliingia ganzi kikabaki kichwa tu kinaweza kufanya kazi.

“Sikuwa na hisia zozote kuanzia mikononi hadi miguuni…, sikuweza kufanya chochote, kichwa changu tu ndicho kilikuwa na ufahamu,” anasema.

Baada ya vipimo, picha ya X-ray ilionyesha kuwa pingili tatu za uti wa mgongo wa Mishaly zimekatika, nyonga imeharibiwa vibaya lakini na shingo kuvunjika.

Maisha yake kwa sasa

Mishaly anaishi kwenye nyumba ya kupanga ndani ya mji mdogo wa Kibaha. Anasema hawezi kwenda kujisaidia au kuoga mwenyewe, hivyo ni lazima awe na mtu wa kumsaidia na katika hali hiyo anajikuta anasaidiwa na mtu yeyote katika vitendo hivyo vya faragha bila kujali hata jinsia.

“Ninapata wakati mgumu lakini Mungu ana maajabu yake, kutokana na matatizo yangu hayo hata mkojo ungejaa vipi hauwezi kutoka mpaka nijiminye.”

Anasema hata madaktari wa India walipotaka kumfanyia operesheni ya tatizo hilo alikataa kwa kuwa japo ni tatizo lakini linamuepusha na adha ya kujichafua.

Awali alikuwa na dada wa kazi akimsaidia kupika na kufanya usafi wa nyumba, lakini imembidi amrudi sha baada ya kukosa pesa za kumlipa.

“Nilikuwa nina msichana wa kazi na nilikuwa namlipa fedha ambazo watu mbali mbali walikuwa wanajitolea kunisaidia lakini sasa naona kama wamechoka, hawanisaidii tena, hivyo nilimwambia arudi tu nyumbani kwao.

“Niliona aibu ya kukaa na mtoto wa mtu kila siku ananibeba, kuniogesha na kunipikia lakini sina pesa ya kumlipa,” anasema Mishaly.

Mishaly anasema maisha yake kwa sasa hayana tofauti na ya ndege, kwani anakula chakula ambacho hajui kinatoka wapi wala kimeandaliwa vipi, wasamaria wema tu wakiniletea nakula na kumshukuru Mungu kwa siku hiyo.

Pia kutokana na kukaa kitandani kwa muda mrefu ananyemelewa na magonjwa mengine ikiwamo homa za mara kwa mara na msongo wa mawazo.

“Huwa napata homa mara nyingi, madaktari wanasema ni kwa kuwa misuli mingine haifanyi kazi hivyo hata uzalishaji wa kinga za mwili siyo nzuri, sasa ninapata msongo wa mawazo kutokana na kukosa faraja,” anasema Mishaly.

Licha ya matatizo aliyonayo, wengine wameyachukulia kama fursa kwao kwa kumdhulumu haki zake kwa kuwa hana uwezo wa kuzipigania.

Mishaly anasema kabla ya kuhamia mahali anapoishi sasa aliwahi kupanga katika nyumba ya mama mmoja ambaye hakumtaja jina na baadaye alimtafutia visa kisha kumfukuza ndani ya mwezi mmoja wakati huo akiwa amemlipa kodi ya miezi sita.

“Kuna mama mmoja hapa Kibaha nyumba yake anaitumia kujitajirisha, akishakupangisha lazima atakutafutia sababu utaondoka na mimi aliweza kunifanyia hivyo kirahisi kutokana na hali niliyokuwa nayo,” anasema.

Ahitaji upasuaji mwingine

Mishaly anatakiwa kufanyiwa upasuaji nchini India ili kurekebisha mgongo na shingo yake. Alishawahi kwenda India kwa matibabu lakini aliishiwa na pesa, kwani alijua atakaa miezi miwili tu lakini daktari wake alimweleza kwa kuwa amechelewa kupatiwa matibabu itamlazimu kukaa miezi sita.

“Daktari aliyekuwa akinihudumia aliniuliza ni kwanini nilikaa muda mrefu bila kupata matibabu. Nilimweleza kuwa pesa ndicho kilikuwa kikwazo kikubwa. Akaniambia kuwa tatizo langu lingeweza kushughulikiwa mapema lisingefika lilipo na lilipofikia linahitaji utaalamu na teknolojia ya hali ya juu ili kuweka mambo sawa.

Mishaly anasema baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali alianza kupata ahueni kwani mikono yake ilianza kufanya kazi na hata baadhi ya sehemu za mwili zilianza kuhisi.

“Nilikuwa nimeshaanza kurejea kuwa katika hali ya uzima na ndiyo kwa bahati mbaya fedha zikawa zimeniishia ikanibidi kurudi nyumbani,” anasema.

Baada ya kurejea nchini alianza kutafuta fedha tena kwa ajili ya kurudi India kuendelea na matibabu lakini hakufanikiwa kwani alipata Sh120,000 tu wakati zinahitajika Sh18 milioni.

Mishaly bado mchango wake unahitajika kwa taifa, hajiwezi kwa lolote, ni wa kubebwa, kufuliwa na kusaidiwa kwa kila hali, muda wake mwingi anautumia kitandani. “Kitanda kinachosha sana, namuomba Mungu aninyanyue hapa kitandani.”

Mishaly anaimini ipo siku atapona na anasema anatamani na yeye siku moja awe na familia yake.

Maoni ya daktari

Daktari kiongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Stanley Binagi anasema sasa kuna mapinduzi makubwa ya teknolojia na operesheni kubwa kama za Mishaly zinaweza kufanyika ila tu inatokana na kiwango cha tatizo lilipofikia.

“Sijaona picha ya X-ray ya huyo mgonjwa lakini sasa mataifa yaliyoendelea yanafanya operesheni kubwa hata za kuzindua misuli iliyosinyaa ila nina wasiwasi kuwa huenda alichelewa kupata matibabu,”anasema Binagi.

Ili kumsaidia Mishaly, piga namba 0718-626642