Friday, March 17, 2017

Ukali wa wazazi husababisha hofu iliyopitiliza kwa watoto ukubwani

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi makala@mwananchi.co.tz

Mwili wa mwanadamu ni mfano wa mashine ngumu kuielewa inavyofanya kazi, kwani mwanadamu ameumbwa na hofu au wasiwasi ikiwa ni sehemu muhimu ya kujihami na matukio ya kila siku.

Hofu hii ina kiwango chake ambacho ikipitiliza inakuwa tatizo la kiafya hasa ya akili linalohitaji matibabu na ushauri.

Wataalamu wa afya ya akili wanaiita hofu au wasiwasi uliokithiri kama Generalised Anxiety Disorder (GAD), tatizo linalowakosesha ajira baadhi ya watu kutokana na kutojiamini katika usaili.

Hofu iliyopitiliza huambatana na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku bila mhusika kuwa na sababu ya kuwa nayo. Watu wenye hofu kubwa bila sababu ya msingi mara nyingi huwa wanahisi kutokewa na janga kwenye familia zao, fedha, afya, ajira, masomo au biashara zao.

Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi na huzuni kiasi kwamba hutawala mawazo ya mhusika na kuingilia utendaji wake wa kila siku ikiwemo kazi, masomo, shughuli zake za kijamii au uhusiano na mwenza wenza wao.

Inakadiriwa, kati ya watu milioni nne mpaka tano nchini Marekani hukumbwa na tatizo hili kila mwaka. Ingawa hakuna takwimu zinazoonyesha ukubwa wa tatizo hili nchini, wapo waathirika wake.

Kwa kawaida, wanawake huathiriwa zaidi kuliko wanaume. Aidha, hofu hii mara nyingi huanza kipindi cha utoto au kabla ya ujana ingawa pia inaweza kutokea wakati wa utu uzima.

Dalili

Viashiria au dalili za hofu iliyopitiliza huathiri uwezo wa mtu kufikiri ingawa baadaye unaweza kumletea mushkeli wa afya mwilini. Hali hii inaweza kuambatana na dalili mbalimbali, zikiwamo zinazohusu utendaji wa mwili.

Baadhi ya dalili hizo ni kuwa na hisia ya kuwapo kwa janga kwamba kitu kibaya kitatokea muda wowote na hatari kubwa inamnyemelea mhusika au chochote kinachomhusu.

Baadhi ya waathirika huhisi kutaka kukimbia, kujitenga na jamii kwa kutaka kwenda mbali, kubadilika kwa rangi ya ngozi na kuwa nyeupe kama mtu aliyeishiwa damu. Wengine huhisi ngozi kuwaka moto, koo kubana au limefunga ama wamekabwa.

Wapo wanaochanganyikiwa, wanaohisi kutengwa na ulimwengu, wanaopoteza hisia, kutojitambua mwenyewe, kupata kizunguzungu, kichwa kuwa chepesi, kupepesuka na mvurugano wa hisia.

Nyingine ni hofu ya kurukwa akili, kupoteza uwezo wa kujidhibiti wenyewe

au kuhisi kama vile kuna kitu kinachobana kichwani na kuhisi baridi au joto kali ingawa hali ya hewa yaweza kuwa kinyume chake.

Kushindwa kujituliza, kubanwa tumbo, kichefuchefu, ganzi au hali ya kuchomachoma sehemu fulani fulani za mwili na kuhisi kuziba masikio. Moyo kudunda au kwenda kasi isivyo kawaida, maumivu makali kifuani, shingoni, kwenye mabega, kichwani au usoni.

Mgonjwa anaweza kuhisi kukosa hewa au kupumua kwa shida, kutokwa jasho, kubanwa na kifua, kutetemeka kunakoonekana wazi au kwa ndani bila mtu mwingine kutambua, kuchafukwa tumbo, kuhisi haja mara kwa mara, uchovu wa mara kwa mara na shida ya kupata usingizi au kuupata wa mang’amung’amu.

Sababu

Chanzo halisi cha matatizo ya kuwa na hofu kupita kiasi hakifahamiki. Hata hivyo kuna baadhi ya vitu ambavyo vimegundulika kuchangia kuwapo kwa tatizo hili ambavyo ni pamoja na nasaba au genetics.

Baadhi ya watafiti wanasema nasaba ina nafasi kubwa ya kumfanya mtu wa familia yenye watu wenye hofu iliyopitiliza naye kuwa na uwezekano wa kuipata. Hii inamaanisha, hofu iliyopitiliza inaweza kurithiwa miongoni mwa wanafamilia.

Sababu nyingine ni mfumo wa kemikali za ubongo. Hofu iliyopitiliza inahusishwa na kiwango kisicho sahihi cha baadhi ya kemikali zinazosaidia kusafirisha taarifa kwenda ubongoni yaani neurotransmitters.

Iwapo kemikali hizi zitakuwa kwenye kiwango kisicho sahihi; kupungua au kuongezeka taarifa hazitaweza kusafirishwa na kuufikia ubongo kama inavyotakiwa. Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko katika utendaji kazi wa mwili na mgonjwa kupatwa na hofu iliyopitiliza.

Sababu za kimazingira nazo zinaelezwa kuchangia tatizo hili. Matukio kama vile ajali, kuumia au kunyanyaswa, kufiwa na mtu wa karibu, talaka, kuachishwa au kufukuzwa kazi au shule ni chanzo cha hofu iliyopitiliza

Aidha, ulevi, uvutaji wa sigara au unywaji wa kahawa uliopitiliza ni sababu nyingine. Inaelezwa, watu waliokuwa watumiaji wa vitu hivyo wakiacha ghafla, hukumbwa na tatizo hili.

Iwapo mgonjwa ana dalili za hofu, kwanza daktari atataka kufahamu historia yake kwa kumuuliza maswali juu ya maisha yake na dalili zinazomsumbua kabla ya kumfanyia uchunguzi wa mwili mzima kufahamu kama hana tatizo jingine.

Kutambua, daktari atafuatilia tatizo; kufahamu dalili zilipoanza kujitokeza na iwapo tatizo hili linamfanya mgonjwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Iwapo daktari atabaini mgonjwa amekuwa akisumbuliwa na dalili hizi kila siku au kwa muda mwingi kinachozidi miezi sita, atajiridhisha, bila shaka kuwa mgonjwa ana GAD. Dalili hizi pia lazima zionekane kuathiri maisha ya kila siku.

Ingawa hakuna kipimo cha kugundua ugonjwa huu, daktari anaweza kufanya vipimo vingine kuchunguza iwapo mgonjwa ana tatizo jingine lolote la kiafya.

Matibabu

Iwapo uchunguzi utaonesha mgonjwa hana tatizo jingine, huduma za wataalamu wa afya ya akili watakuwa na msaada zaidi.

Hofu iliyopitiliza haina kinga ya moja kwa moja, hata hivyo yapo baadhi ya mambo yanayosaidia kupunguza ukubwa wake ambayo ni pamoja na kuacha au kupunguza matumizi ya vyakula au vinywaji kama vile kahawa, chai, cola au chokoleti. Kuepuka dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Kufanya mazoezi mepesi na kupata ushauri nasaha ni namna nyingine za kukabiliana nao.

Muhimu kujifunza mbinu za kudhibiti msongo wa mawazo kwa kufanya mazoezi mbalimbali kama vile kucheza muziki unaohusisha maungo mengi ya mwili na kufanya massage.

-->