UCHAMBUZI: Sekta binafsi ishirikishwe kutatua uhaba wa dawa vituoni

Rashid Kejo 

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hadi kufikia Machi, 2017, asilimia 81 ya dawa muhimu zaidi (essential medicine) zinapatikana katika Bohari ya Dawa Tanzania (MSD). Alisema ongezeko hilo la upatikanaji wa dawa kutoka asilimia 36 kipindi cha Juni 2016 na kufikia asilimia 81 hadi Machi mwaka huu, limetokana na uamuzi wa Serikali wa kuongeza bajeti ya dawa na kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya dawa, vifaa, vifaa vya tiba, na vitendanishi. “Aidha, wizara kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo ya ununuzi wa dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama za dawa na kuongeza uwezo wa MSD kununua nyingi zaidi. Lengo la wizara ni kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inafikia asilimia 90 ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha 2016/17.”

Taarifa hizo zinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na taasisi zinazojishughulisha na masuala ya afya nchini likiwamo Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika ambalo linaeleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeimarika kutoka asilimia 51 kwa mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 81 mwaka huu.

Sababu zilizobainishwa na Sikika zinashabihiana na matumizi sahihi ya fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya dawa, MSD kuanza kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji viwandani na kuondoa gharama ambazo ilikuwa inamlipa mtu wa kati.

Jingine ni lile ambalo wadau wengi walikuwa wakilipigia kelele la ukiritimba uliokuwapo wa MSD kuwa sehemu pekee ya vituo vya kununulia dawa.

Hii ilimaanisha kwamba, kama Bohari hiyo haikuwa na dawa zilizokuwa zikihitajika, hapakuwa na njia nyingine ya kuzipata hata kama wahitaji walikuwa na uwezo wa kifedha wa kuzinunua kwingineko.

Hali hiyo ilikuwa na mchango katika uhaba wa dawa na baada ya Serikali kuvifungulia milango vituo hivyo ya kununua kutoka kwa watu binafsi dawa ambazo MSD haina, tumeanza kuona matunda yake.

Naamini kwamba hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kufikia asilimia hizo 81 za upatikanaji wa dawa muhimu.

Ndiyo maana nasema kitendo cha MSD kuendelea kuwa mnunuzi na msambazaji pekee wa dawa nchini ni changamoto hasa kwa kuzingatia uwezo wa taasisi hiyo kulinganisha na ukubwa wa nchi ambayo ina vituo vingi vya afya.

Kwa mujibu wa Shirika la Viwango la Taifa (NBS), idadi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

Mathalan, NBS inaonyesha kwamba, 2010 kulikuwa na hospitali 240, vituo vya afya 687 na zahanati 5,394 ambavyo kwa pamoja vilifikia 6,321, idadi ambayo iliongezeka mwaka hadi mwaka na ilipotimu 2015, kulikuwa na hospitali 252, vituo vya afya 718 na zahanati 6,549 (zikiwamo kliniki 89) na kufanya jumla kuwa 7,519.

Sehemu kubwa ya vituo hivyo vya tiba vinamilikiwa na Serikali na ndivyo vinavyoitegemea MSD kuvipatia dawa. Kwa maana hiyo, mzigo huo ni mkubwa mno kwa Bohari.

Pamoja na Serikali kufanya mapitio ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika mfumo wa ugavi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa vya tiba, vitendanishi na chanjo kwa lengo la kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji ili kuwa na mfumo madhubuti wenye kukidhi mahitaji ya nchi, naamini kwamba ushiriki wa sekta binafsi katika kufanikisha hili ni jambo muhimu.

Naamini kwamba sekta binafsi ikishirikishwa kikamilifu, kisha Serikali ikawekeza zaidi katika mashine za vipimo katika ngazi za chini, mrundikano wa wagonjwa katika hospitali zake za rufaa utapungua, wananchi watapata tiba bora na za uhakika kwa wakati hivyo kutumia muda wao mwingi kwenye uzalishaji na kulijenga Taifa.

0784 322193