Saturday, November 18, 2017

Utajiri wa rasilimali za uvuvi nchini unavyosaidia kukuza uchumi na sekta ya viwanda

 

By John Mapepele

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili.

Raslimali hizo zinajumuisha madini ya aina tofauti, gesi, misitu ya asili, mbuga na hifadhi za wanyama pamoja na eneo kubwa la maji ya mito, maziwa na bahari.

Katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza kila mara kuwa kama Tanzania itatumia vizuri rasilimali zake, itafika wakati nchi itakuwa na uwezo kutoa misaada kwa nchi nyingine badala ya kutegemea misaada kutoka mataifa mengine kama ilivyo sasa.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchi yetu imejaliwa maeneo mengi ya maji ambayo ni muhimu katika shughuli za uvuvi ambazo huwapatia wananchi lishe, kipato na ajira.

Maeneo hayo hujumuisha eneo la maji baridi na maji bahari. Eneo la maji baridi hujumuisha maziwa makuu matatu ambayo ni Ziwa Victoria (35,088km2), Ziwa Tanganyika (13,489 km2) na Ziwa Nyasa (5,700 km2)

Aidha, kuna maziwa ya kati na madogo 45, mito 29, mabwawa ya asili na ya kuchimbwa pamoja na maeneo oevu.

Kwa upande wa maji ya bahari, Tanzania ina ukanda wa pwani wa Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilometa 1,424 ambao umegawanyika katika eneo la Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) lenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,000 na eneo la Ukanda wa Uchumi wa Bahari lenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000. Katika maeneo haya kuna rasilimali nyingi za uvuvi ambamo shughuli za uvuvi hufanyika.

Taarifa za utafiti zilizofanyika kwa vipindi tofauti zinaonyesha kwamba, kiasi cha samaki kilichopo katika maziwa makubwa ni takriban tani 2,914,296 (Ziwa Victoria tani 2,451,296, Ziwa Tanganyika tani 295,000 na Ziwa Nyasa tani 168,000).

Umuhimu wa sekta ya uvuvi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dk Yohana Budeba anasema umuhimu wa sekta ya uvuvi unajidhihirisha katika kuchangia uchumi wa Taifa, lishe bora na ajira kuanzia katika ngazi ya familia.

Anasema zaidi ya watu milioni nne wameendelea kunufaika na sekta ya uvuvi ikiwamo uchakataji wa samaki, utengenezaji wa zana na vyombo vya uvuvi, biashara ndogondogo na mama lishe.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega anasema changamoto zinazowakabili wawekezaji katika sekta ya uvuvi ni pamoja na upungufu wa maofisa ugani wa uvuvi ukilinganisha na mahitaji, upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki, upatikanaji wa vyakula bora vya samaki, upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya wavuvi, mabadiliko ya tabia nchi na uhifadhi wa mazao ya uvuvi

Anasema Serikali itaendelea kupambana na changamoto ya uvuvi haramu ili kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinaboreka na hivyo kuchangia katika uchumi wa nchi.

Mchango katika viwanda

Pamoja na changamoto za kwenye sekta hii, ni ukweli usiopingika kwamba unapozungumzia Tanzania ya viwanda, huwezi kuacha kuitaja sekta ya uvuvi kama moja ya mzalishaji mkubwa wa malighafi za viwanda hususan vile vya nyama na usindikaji kwa ujumla.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina anasema katika kipindi cha miaka miwili cha Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwapo mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi.

‘Katika mwaka 2016/2017, jumla ya tani 362,595 za samaki wenye thamani ya Sh 1.49 trilioni zilivunwa na wavuvi 203,529 ikilinganishwa na tani 362,645.3 za samaki wenye thamani ya Sh 1.48 trilioni waliovunwa mwaka 2015/2016,’’ anasema na kuongeza:

Pia, katika mwaka 2016/2017, jumla ya tani 39,691.5 za samaki na mazao ya uvuvi yenye thamani ya Sh526.99 bilioni yaliuzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa jumla ya Sh 14.30 bilioni kama ushuru.

Dk Budeba anasema Wizara imeendelea kuimarisha na kuongeza miundombinu ya uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki kwa kujenga mabwawa na kuweka matanki katika vituo vya Serikali vilivyopo Bagamoyo (Pwani), Kingolwira (Morogoro), Machui (Tanga), Mwamapuli (Tabora), Nyamirembe (Geita), Nyengedi (Lindi) na Ruhila (Ruvuma).

Aidha, vitotoleshi 15 vya samaki aina ya perege vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga 11,520,000 kwa mwaka katika kituo cha Kingolwira vimewekwa.

Kuhusu uzalishaji na usafirishaji wa mazao ghafi ya mwani nje ya nchi Dk Budeba anasema umeongezeka kutoka tani 1,176.51 zenye thamani ya Sh 350 milioni mwaka 2015/2016 hadi tani 1,197.5 zenye thamani ya Sh 412 milioni mwaka 2016/2017.

Aidha, sekta binafsi imeanzisha vituo vitano vya ukuzaji viumbe kwenye maji na kufikia vituo 13. Vilevile, mabwawa ya samaki yameongezeka na kufikia 22,702 mwaka 2016/2017 ikilinganishwa na mabwawa 22,545 mwaka 2015/2016 ambayo yamewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki kwenye mabwawa kutoka wastani wa tani 3,613.55 mwaka 2015/2016 hadi tani 11,000 mwaka 2016/2017.

Anasema serikali imeimarisha udhibiti ubora na usalama wa mazao ya uvuvi ili kulinda soko la ndani na nje ya nchi kwa kutumia maabara ya taifa ya uvuvi ya Nyegezi mkoani Mwanza ambayo ilipata ithibati ya kimataifa. Pia ukaguzi wa mazao ya uvuvi umeimarishwa kwenye viwanja vya ndege, bandari, mipakani na minadani.

Mkakati dhidi ya uvuvi haramu

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ulega, anasema Serikali imezindua mkakati unaolenga kutokomeza uvuvi haramu, kwa kuanzisha operesheni ya kutumia ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu ili kudhibiti eneo hilo.

Anasema doria hiyo ni ya kikanda ambayo inahusisha nchi nane zikiwamo Tanzania Kenya, Msumbiji, Ushelisheli, Reunion, Comoro, Mauritius na Madagascar.“Tunaruhusu ndege ya doria leo, ili kuongezea nguvu njia za kudhibiti wavuvi haramu. Tulianza kwa njia ya bahari na sasa ni kwa njia ya anga. Changamoto ya uvuvi haramu ni kubwa, mtu anapiga bomu kwenye matumbawe anafanya uharibifu ambao kuyatengeneza tena yanachukua zaidi ya miaka 100, huku yeye akiharibu kwa dakika tano, ” anaeleza.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Hosea Mbilinyi anasema ndege hiyo licha ya kuzunguka angani ikifanya doria, ina uwezo wa kupiga picha na kueleza kinachoendelea.

Anasema kutokana na teknolojia hii ya kisasa ya kutumia ndege katika doria, itasaidia kudhibiti kabisa uvuvi haramu katika ukanda wa nchi za Kusini Magharibi

Agosti mwaka 2016, Rais Magufuli alisisitiza kwamba Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza makokoro katika ziwa Victoria, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji wa minofu ya samaki katika viwanda.

Alibainisha kuwa lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika minofu ya samaki lifanikiwe.

Hata hivyo kumekuwapo na nadharia mbalimbali katika uhifadhi wa rasilimali za uvuvi duniani. Miongoni mwa hizo kubwa ni mbili yaani ile ya kuwashirikisha wananchi(participatory approach) ambayo nchi yetu inatumia na ile ya kijeshi (para miritary) ambayo nchi nyingine kama Kenya inatumika.

Zote zimeonekana kuwa na faida na hasara. Mwaka 1998 jeshi lilitumika kufanya operesheni maalum ya kutokomeza uvuvi haramu katika ukanda wote wa pwani na kukawa na mafaniko makubwa.

Kutokana na nadharia hizo wataalam wa masuala ya uhifadhi wa rasilimali za uvuvi wamegawanyika; wapo wanaodhani wakati umefika mfumo wa kuhifadhi rasilimali za majini uwe wa kijeshi kama unavyofanywa kwenye hifadhi za Taifa ili kusaidia sekta ya uvuvi kuboreka na kuchangia katika uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025. Wengine bado wanaona kuwa mfumo wa sasa bado unafaa. Tusubiri tuone, muda utaamua!

0784 44 11 80

-->