UCHAMBUZI: Tuunge mkono bila kulitia Taifa hasara

Rais John Magufuli

Taifa linapitia katika aina mpya ya siasa ambayo hatukuizoea tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992.

Kwa muda mrefu, tumekuwa tukishuhudia wanasiasa wakihama kutoka chama kimoja cha siasa kwenda kingine, lakini wimbi la sasa la viongozi wa kuchaguliwa, hasa wa upinzani kujivua uanachama na kuhamia chama tawala, CCM, karibu wote wakieleza kumuunga mkono Rais John Magufuli ni aina mpya ya siasa.

Hivi sasa kampeni zinaendelea kwa ajili ya kujaza majimbo ambayo wabunge wawili wa upinzani, Maulid Mtulia wa Kinondoni (CUF), na mwenzake Dk Godwin Mollel (Chadema), wa Siha wamejivua uanachama na kuhamia CCM kumuunga mkono Rais Magufuli.

Hadi kufikia Januari 10, madiwani 21 walioshinda viti vyao kupitia upinzani, hasa Chadema walikuwa wamejivua uanachama na kuhamia CCM.

Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Iringa na Mara ambako upinzani ulipata viti vingi ndiyo yanayolengwa na wimbi la hilo.

Ni haki ya kikatiba na kisheria kwa mtu kujiunga na chama chochote cha siasa na wakati wowote, lakini vitendo vya viongozi hawa waliochaguliwa kuhamia vyama vingine kabla ya kumaliza kipindi chao vinalitia hasara Taifa.

Hii ni kwa sababu uchaguzi mdogo unalazimika kufanyika kujaza nafasi zao kumalizia kipindi kilichosalia.

Licha ya kuwapo taarifa tofauti za gharama za uchaguzi katika jimbo moja, ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikisema ni takriban Sh3 bilioni na Tume ya Uchaguzi ikiseka ni Sh1 bilioni, fedha hizo ni nyingi.

Kwa hesabu za kawaidi, Serikali italazimika kutumia mabilioni ya shilingi kugharamia chaguzi ndogo katika majimbo na kata ambazo wabunge na madiwani wamejivua uanachama na kuhamia vyama vingine.

Ni kweli demokrasia ni gharama. Lakini hizi za kujitakia za viongozi wa kuchaguliwa kuhamia vyama vingine katikati ya muda wao unaturejesha nyuma kiuchumi kwa Taifa kutumia fedha ambazo zingegharamia miradi ya maendeleo kuliko kugharamia uchaguzi mdogo katika maeneo yao.

Sh14 bilioni si haba katika Taifa ambalo bado tunashuhudia upungufu wa madawati, majengo ya vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo, ofisi na nyumba za walimu katika shule zetu za umma.

Gharama ya kujenga jengo la darasa moja ni kati ya Sh7 milioni hadi Sh9 milioni wakati bweni moja linakadiriwa kugharimu hadi Sh15 milioni.

Fedha hizi zingeweza kununulia dawa na vifaa tiba katika hospitali za umma.

Gari moja la kubeba wagonjwa linakadiriwa kugharimu kati ya Sh250 milioni hadi Sh300 milioni.

Fedha za kufanya uchaguzi ndogo kwenye kata 21 zingenunua magari 21 ya wagonjwa kwa ajili ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu na hivyo kupunguza vifo vya wajawazito na watoto vinavyotokana na kukosa huduma za dharura kutokana na tatizo la usafiri wa kufika maeneo ya huduma.

Mashine moja ya kipimo cha CT-Scan inauzwa kwa wastani wa Sh1.8 bilioni. Sh14 bilioni za kughramia chaguzi ndogo katika majimbo na kata ambazo wabunge na madiwani wake wamehamia vyama vingine zingenunua karibu mashine kumi.

Nadhani muda wa kufanyia marekebisho sheria zetu umefika ili kuongeza vifungu vinavyowaruhusu viongozi wa kuchaguliwa kuendelea na nyadhifa zao hata baada ya kuhamia vyama vingine.

Tumuunge mkono Rais lakini siyo kwa kuitia Taifa hasara.

Ngollo John ni mwandishi wa gazeti hili Mwanza; [email protected] au 0757708277.