ANTHONY MTAKA : Mkuu wa Mkoa mwenye vipaji lukuki

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Anthony Mtaka.

Muktasari:

  • Si hayo tu lakini pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli Machi 13 mwaka huu.
  • Awali, kabla ya kupata cheo cha Ukuu wa Mkoa, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Jina la Anthony Mtaka siyo geni masikio mwa Watanzania hasa wapenzi na mashabiki wa mchezo wa riadha, kwani ndiye Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Si hayo tu lakini pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli Machi 13 mwaka huu.

Awali, kabla ya kupata cheo cha Ukuu wa Mkoa, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Baadhi ya wa Watanzania, hasa wakazi wa Hai na Simiyu wanamjua Mtaka kama kiongozi wao wa Chama cha Riadha Tanzania , lakini mkuu wa mkoa huyo ana cheo kingine na vipaji kadhaa ukiachana na kazi hiyo.

Alikuwa askari

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Gazeti hili, hivi karibuni Mtaka alisema kabla ya kupata vyeo hivyo alikuwa askari wa jeshi la polisi aliyepata mafunzo yake kuanzia mwaka 2004 hadi 2005 katika Chuo cha Polisi Moshi, kilichopo mkoani Kilimanjaro.

“Mimi ni askari wa akiba namba yangu ni F 6886 PC Anthony Mtaka. Zikirindima leo nakamata silaha. Kazi yangu niliifanya Mkoa wa Mbeya,” anasema Mtaka.

Mbali na hilo, Mtaka anasema yeye ana kipaji cha kuimba nyimbo za Injili na katika siku za usoni ataanza kurekodi nyimbo zake mpya ambazo hakuwa tayari kuzitaja kwa sasa.

Pia, Mtaka anasema ana uwezo wa kuandika makala na anafanya kazi hiyo katika moja ya gazeti la Kiswahili linalotoka mara moja kwa wiki.

Kitu gani ambacho huwezi kukisahau

Mtaka anasema miongoni mwa mambo ambayo hatayasahau maishani mwake ni siku alipoteuliwa na Kikwete kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

“Nilikuwa nafikiri wanaopata nafasi ya ukuu wa wilaya ni watoto wa vigogo. Lakini nilivyopata nafasi sikuamini,” anasema Mtaka.

Ni Yanga damudamu

Mtaka anasema yeye ni mwanachama na shabiki mkubwa wa klabu ya soka ya Yanga na ikitokea siku timu ikafungwa anajisikia vibaya.

Wasanii anaowapenda

Bila kuwa na kigugumizi Mtaka anasema humwambii kitu kwa msanii wa kike Judith Wambura maarufu Lady Jay Dee anayetamba na kibao cha ‘Ndindindi’.

“Nampenda Jay Dee, kwa sababu ni msanii wake kike aliyethubutu na ameweza kusimama mwenyewe hadi sasa. Pili ni mtu asiyechoka kutafuta mafanikio”.

“Msanii mwingine ni Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ni kijana wa tofauti, ameleta kitu kipya katika muziki wa kizazi kipya,” anasema Mtaka.

Ukiwa nyumbani unapenda kufanya nini

“Nikiwa nyumbani napenda kusoma vitabu vya Lugha ya Kingereza na Kiswahili.Tangu mwaka huu uanze nimesoma vitabu sita,” anasema Mtaka.

Nini mkakati wake

“Nataka kuifanya Simiyu izibe pengo la nchi kuagiza vitu mbalimbali ikiwamo utengezaji wa chaki na pamba za hospitali nikiwa na kaulimbiu ya ‘wilaya moja bidhaa moja au bidhaa moja wilaya moja’,” anafafanua.

Pia, katika kipindi chake cha uongozi anataka kuiona Simiyu inakuwa moja ya mikoa itakayongoza katika elimu na kilimo cha zao la pamba kutoka tani milioni 70 zinazozalishwa sasa hadi milioni 140.

Oktoba mwaka huu, Simiyu itaanza kuzalisha bidhaa za chaki ikishirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido).

“Kwa mantiki hii uagizaji wa chaki kwa Mkoa wa Simiyu utakuwa wa kihistoria. Kuanzia mwezi ujao ni marufuku kuagiza chaki nje ya Mkoa wa Simiyu. Kwa sababu tutakuwa tukizalisha wenyewe,” anasema Mtaka.

Anamzungumziaje Rais Magufuli

Mtaka anasema utendaji kazi wa Rais Magufuli umerahisisha utendaji kazi kati ya viongozi na wananchi, kutokana na mkuu huyo wa nchi kufanya kazi zake kwa vitendo na kuhimiza maendeleo.

“Mfano sasa hivi baadhi ya wafanyabiashara wanatoa stakabadhi kwa wateja.Hata wateja wanaokwenda kununua bidhaa nao wanadai risiti, hii inatokana na msimamo wa Rais Magufuli wa kutaka kila mtu alipe kodi,”anasema Mtaka.