Alianzia African Lyon sasa aitaka Zanaco

Muktasari:

  • Hilal ambaye anacheza kwa mkopo, Chemelil Sugar akitokea Tusker ni miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania ambao Spoti Mikiki, imewavumbua na wakapata nafasi ya kuitwa, Taifa Stars.

Winga wa zamani wa African Lyon, Abdul Hilal amekuwa kwenye mipango ya muda mrefu ya kuondoka Kenya na kwenda, Zambia kwenye klabu ya Zanaco ambayo tayari ameingia nayo mkataba wa awali.

Hilal ambaye anacheza kwa mkopo, Chemelil Sugar akitokea Tusker ni miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania ambao Spoti Mikiki, imewavumbua na wakapata nafasi ya kuitwa, Taifa Stars.

Nyota huyo ameichezea, Chemelil Sugar ya Ligi Kuu Kenya michezo nane na katika michezo hiyo amefunga mabao manne na kutengeneza mengine mawili tangu ajiunge nao mwanzoni mwa mwaka huu.

Spoti Mikiki imeongea na Hilal ambaye ameweka wazi sababu zilizomfanya kuandika barua kwenye klabu yake ya Tusker ya kuomba kutolewa kwa mkopo pia ilikuwaje akapata dili la Zambia na maisha ya Kenya kiujumla anavyoishi.

“Msimu uliopita sikuwa napata nafasi ya kucheza mara kwa mara na sikuwa nafurahia hali ile binafsi, nilianzisha ratiba za kufanya sana mazoezi ili nitakapo kuwa napata hizo nafasi chache nizitumie kwa kujihakikishia namba.

“Muda ulisogea na mwisho msimu ukamalizika bila ya kufikia malengo ya nilichojiwekea, bahati nzuri Zanaco walinitumia barua ya kuomba nikafanya majaribio kwenye timu yao.

“Sikuona kama ni tatizo kwangu na kwakuwa msimu ulikuwa umemalizika nilienda kimyakimya na kufanya kisha kurejea huku lakini wakati huo tukiwa tumeshamalizana kabisa,” anasema.

Hilal anadai kumalizana kwenye ni kwa kuingia makubaliano ya awali mara baada ya kuvutiwa na uwezo wake ili mkataba wake utakapomalizika atue kwenye klabu hiyo kwa kusaini mkataba rasmi.

Wakati amerejea kutoka Zambia hakuna aliyetambua kutoka Tusker kuwa amesaini mkataba wa awali na kikanuni aliruhusiwa kutokana na mkataba wake na Tusker kusaliwa na miezi sita kabla ya kumalizika.

“Kuliko kuendelea kusugua benchi na kupata nafasi mara chache niliona ni uamuzi wa busara kwangu kuandika barua kwa uongozi kuomba wanitoea kwa mkopo.

“Hapakuwa na ugumu wa aina yoyote, kabla ya msimu kuanza walinipa ruhusa ya kujiunga na Chemelil,” anasema winga huyo.

Akiongelea maisha anayoishi Kenya, Hilal amesema yanautofauti mkubwa na yela ambayo alikuwa anaishi nyumbani kuanzia malazi, vyakula na anavyochukuliwa na jamii iliyomzunguka.

“Wakenya ni watu safi sana, sio watu wa chuki labla ukiwakwaza, nilipokewa vizuri sana Chemelil na kufurahiwa na kila mchezaji. Kila nachotaka kula kwa huku nakipata kwa wepesi na kula, napendelea sana kula wali na kuku.

“Vyakula Kenya sio gharama sana.Huku nimekuwa mwenyeji tayari kuna nyumba ambayo naishi na marafiki zangu, ujue japo sio kwa kiwango kikubwa sana ila Watanzania tuna mioyo ya kusaidia na niwatafutaji sana.

“Mtanzania anayekuja huku kutafuta maisha ya mpira sio rahisi kukosa sehemu ya kufikia, tumejijengea utaratibu wa kusaidiana, ilikuwa hivyo kipindi ambacho nilikuja Kenya moja kwa moja nikitokea Tanzania,” anasema Hilal.

Kuhusu kuwa na mke, Hilal anasema bado muda wa kuanzisha familia yake haujafika na ukifika itapendeza akiwa kwenye hatua kubwa ya kucheza soka la kimataifa nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

“Nina mpango wa kuoa lakini sio kwa miaka ya hivi karibuni, nawaza kupambana na kufikia ndoto zangu za kucheza mpira kwenye ligi kubwa, nilianza Tanzania, nikaja hapa Kenya kwa sasa nawaza kwenda Zambia mwisho wa msimu.

“Mchumba ninaye japo siwezi kumweka wazi ila huwa namweleza nini nawaza kwa sasa, najua kama nikizembea soka langu litaishia, Afrika Mashariki na kati, Mungu akipenda baada ya Zambia nitakuwa natazama zaidi Afrika Kusini,” anasema.

Hilal anasema mbali na maisha yake ya uwanjani amekuwa mtu wa kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kijamii na majirani zake nchini Kenya na ndiyo maana amekuwa akiishi nao vizuri.

“Kuishi kwa kujitenga na kutoshiriki mambo ya kijamii ni ushamba kwa kujikuta eti ni staa, nilifundishwa nyumbani kuwa ukiishi vizuri na watu na wao wataishi vizuri na wewe,” anasema winga huyo wa Tusker.

Kama Hilal atafanikisha dili lake ya kujiunga na Zanaco, atakuwa amefuata nyayo za David Naftar ambaye naye ni Mtanzania aliyemtimka Kenya na kutua, Kabwe Warriors ya Zambia.