Balozi husaidia kukuza, kujenga heshima ya biashara

Muktasari:

Miongoni mwa mikakati ya kufanikisha hilo ni kuwa na balozi wa biashara ambaye ni mtu anayenunua bidhaa kwa bei nafuu ili aitangaze kwa wengine kwa hadhi au umaarufu wake analipwa na kampuni ili aitangaze kampuni ama bidhaa zake kwa muda maalum watakaokubaliana.

        Mfanyabiashara anahitaji kujitahidi kusoma na kupata ushauri kama anadhamira ya kuendelea kupata faida na kufanya vizuri sokoni.

Miongoni mwa mikakati ya kufanikisha hilo ni kuwa na balozi wa biashara ambaye ni mtu anayenunua bidhaa kwa bei nafuu ili aitangaze kwa wengine kwa hadhi au umaarufu wake analipwa na kampuni ili aitangaze kampuni ama bidhaa zake kwa muda maalum watakaokubaliana.

Balozi anaweza kuwa wa bidhaa maalum ama wa kampuni bila kujali ndani ya kampuni kuna aina ngapi za bidhaa. Mabalozi wanaweza kuwa wengi kwa bidhaa au kampuni fulani kutegemea malengo ya kampuni husika.

Kuna aina nyingi ya mabalozi wa biashara lakini kwa mazingira yetu tutazungumzia aina tatu. Aina ya kwanza ni anayepata punguzo la bei. Balozi huyu sifa yake ni kuwa mtumiaji wa mara kwa mara wa bidhaa hizo ambao ndio msingi wa kupata punguzo la bei.

Anapewa punguzo la bei kwa lengo la kuwa balozi wa bidhaa ama kampuni kwa kufanya kazi ya kushawishi wenzake kununua bidhaa hizo. Punguzo hilo ni malipo ya kushawishi watu kununua bidhaa ili kampuni iuze kwa wingi.

Kuna mabalozi wanaotokana na umaarufu au hadhi zao katika jamii. Balozi huyu hulipwa na kampuni kwa kukubali kwake na kuna makubaliano maalumu yanaingiwa ili balozi atekeleze baadhi ya majukumu ambayo yatachangia kampuni kuongeza mauzo na kuwa na sifa nzuri kwa jamii.

Miongoni mwa kazi ambazo balozi huyu hutakiwa kufanya hujumuisha kuvaa fulana au kofia za kampuni, kuizungumzia vyema kampuni na bidhaa zake popote atakapokuwepo pamoja na kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Aina ya mwisho ni balozi anayelipwa na kushiriki matukio muhimu ya kampuni. Balozi huyu haitaji kuwa maarufu au hadhi katika jamii. Huyu hutengenezwa kwa kuchaguliwa kutokana na vigezo vitakavyowekwa na kampuni. Atafanya kazi zote baada ya kupewa mafunzo maalum. Hushiriki kwenye maonesho ya biashara, promosheni na matukio ya kibiashara ya kampuni husika.

Biashara za aina zote na ukubwa tofauti zinahitaji mabalozi kama njia ya kuongeza wateja na mauzo ili kupata faida na kukua. Kila biashara itatengeneza mabalozi wake kwa kulingana na uwezo wake.

Kuna faida nyingi za kuwa na balozi wa biashara. Miongoni mwa faida hizo ni kuongeza mauzo, faida, kukuza jina na kupanuka kibiashara na kuwa na uhakika wa soko la bidhaa kila siku.

Tumeshuhudia bodaboda na madereva wa daladala wanavyochukua nafasi kubwa ya kupata mlo kwa akina mama na baba nitilie. Ni elimu ndogo tu inahitajika kumtambua dereva mwenye ushawishi kwa wenzake. Ukishampata, unaongea naye kwa kumpa punguzo la bei ya chakula kila siku akija na wenzake watano na zaidi. Hali hii itamuhakikishia mama nitilie mauzo ya uhakika.

Elimu ya biashara katika kona hii ya mabalozi wa biashara ni ya kawaida endapo utapata ushauri kutoka kwa wataalam wa biashara, utahudhuria semina, utaangalia vipindi vya biashara katika runinga, kusikiliza redio, kusoma vijitabu, magazeti na majalida ya biashara.

Ni muhimu kutambua kwamba mafanikio ya biashara hutegemea mambo mengi likiwamo jina zuri ambalo wateja watalitambua. Kufanikiwa kujenga jina mbele ya jamii kunahitaji mikakati imara itakayotekelezwa kwa umakini mkubwa.

Kila mjasiriamali anapaswa kulifahamu hili na kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha anaendelea kudumu sokoni tena kwa mafanikio makubwa. Mabalozi wa biashara, ni nyenzo muhimu ya kutimiza kusudi hili.

Baada ya kuifahamu siri hii, ni uamuzi wa mfanyabiashara husika kuangalia kama inamfaa kwa biashara yake na kuanza kuitumia mara moja bila kusubiri kwani wakati ni sasa. Fursa huwa hazimsubiri mtu, zikitokea unatakiwa kuchangamka.