Boresha afya na kipato kwa kuzalisha rosella

Muktasari:

  • Baadhi ya matumizi ya zao la rosella ni pamoja na kutengenezea         juisi,       jamu,    mafuta,                sosi.

Rosella ni mmea wenye virutubisho vingi kama vile vitamini, na madini ya chumvichumvi. Kwa miaka mingi, zao hili lilitumika kwa wingi katika mabara ya  Asia, Amerika Kusini,  Caribbeani na Ulaya.

Rosella ni moja ya mazao ambayo yana matumizi mengi na kwa namna tofauti tofauti.  Baadhi ya matumizi ya zao la rosella ni pamoja na kutengenezea juisi, jamu, mafuta, sosi.Rosella pia hutumika kuukinga mwili na magonjwa mbalimbali kama vile saratani, ini na ukosefu wa lishe. Pia inasaidia kupunguza lehemu  na kutibu shinikizo la damu.

Sifa za mmea wa rosella ni zipi?

Majani yake yanaweza kuliwa kama mboga,  ni zao la biashara na hutumiwa nyumbani. Mmea huu hukua na hufikia urefu     wa mita 3.5 kwa msimu. Shina pamoja na matawi yake vimenyooka

Sifa nyingine majani yamepishana kimpangilio na kugawanyika katika sehemu tatu hadi saba, pembeni yakiwa kama msumeno. Mmea una rangi ya kijani, nyeusi hadi nyekundu. Maua ni makubwa yenye rangi nyekundu hadi njano.

Una mzizi mrefu na hutoa maua                wakati wa kiangazi.  Pia unavumilia ardhi yenye tindikali ya juu na ya chini pamoja na magonjwa.

Aina  za  rosella

 Zao la rosella limepewa majina ya aina mbalimbali kulingana na maeneo na watu wa maeneo hayo walivyo onelea kuwa ni vyema. Kwa mfano, mmea wa rosella wenye maua mekundu hujulikana kama choya huko Dodoma na maeneo mengine, wakati ukanda wa pwani ya Tanzania huitwa mkakaka.

Kimsingi kuna aina mbili za rosella Rosella imegawanyika katika makundi (majina) mawili ambayo yanafahamika kitaalamu na watu maeneo mbalimbali. Kitaalamu inafahamika kama         Hibiscus sabdariffa: Hii ni aina ya rosella ambayo ina vikonyo vya rangi nyekundu na vingine vya njano. Vikonyo hivyo vinaliwa.  Aina nyingine ni Hibiscus altissima Webster.  Aina hii ya rosella hupandwa zaidi kwa ajili ya kamba kamba (fibres) zake lakini vikonyo haviliwi.

Jinsi ya kustawisha zao hili

Zao hili linastawi maeneo ya tropiki yenye mvua                kati ya milimita  1500 – 2000 kwa mwaka. Kuwe na mwinuko wa hadi meta  600 kutoka usawa wa bahari.

Ni zao linalovumilia joto na hali ya unyevunyevu, mafuriko, upepo mkali na maji yaliyotuama.

Rosella hupendelea udongo wa mchanga wenye rutuba ambao maji hupenyeka kwa urahisi. Hata hivyo, inaweza kukua kwenye aina mbalimbali za udongo. Huhitaji palizi ya mara kwa mara ili kuondoa kivuli na majani.

Unapotaka kupanda, unahitaji vikapu, mbolea, udongo, mchanga huku ukifuata hatua hizi; tifua ardhi vizuri kwenda chini kiasi cha sentimeta 20, chimba  mashimo ya ukubwa wa sm15 kwa sm 15 na kina cha sm 5.  Panda mbegu kilo11 – 22 kwa hekta

Ni vyema kupanda mbegu kwa mistari, palizi  katika mwezi wa kwanza ni muhimu sana. 

Mbolea za asili zinafaa kutumika na husaidia

Mtindo wa kubadilisha mazao  hutumika hasa kwa ajili ya mdudu anayeshambulia mmea huu kwenye mizizi. Unaweza kubadilisha na mazao ya kijani kama kunde na mahindi.

Kwa mashamba  madogo nyumbani,  panda mistari halafu ikishaota punguza iwe katika mistari ya mita 1  kwa  1. Kwa sashamba makubwa, mbegu zioteshwe kwenye kitalu halafu zipandwe shambani kwa upana wa mita 1.3 hadi 2.6 na mistari ya upana wa mita 2 hadi 3.

Magonjwa

Ugonjwa mkubwa kwa zao hili ni ukungu (Fangasi): Kuna aina mbalimbali za ukungu ambazo hushambulia rosella kwenye mizizi na majani. Kutibu, nyunyiza dawa za asili zinazotumika kudhibiti na kuondoa ukungu kwenye mazao haraka iwezekanavyo.

Unaweza kutumia dawa za kukinga kabla ya mlipuko wa ukungu. Uangalizi wa shamba ni muhimu hasa palizi, kukata mapukutu, kufyeka, kunyweshea, uwekaji mbolea, udhibiti wa wadudu waharibifu. Hivi vyote ni muhimu katika utunzaji wa shamba la rosella ili kuwa na uhakika wa mavuno bora.

Uvunaji wa matunda na vikonyo hufanyika majuma matatu baada ya maua kuchipua.     Inashauriwa vikonyo viondolewe baada ya kuchemsha matunda.

Kwa hisani ya mkulimambunifu