Bunge linavyoshughulikia bajeti ya Serikali

Owen Mwandumbya

Muktasari:

Mwaka wa Fedha wa Serikali huanza Julai Mosi ya kila mwaka wa kalenda. Ndiyo sababu mikutano yote ya Bunge ya bajeti siku zote hufanyika kuanzia katikati ya Aprili na kumalizika kabla ya Julai Mosi.

Katika uchambuzi wa leo, nitaeleza jinsi Bunge linavyoshughulikia bajeti ya Serikali katika vikao vyake. Kwanza ni vyema ikafahamika kuwa Bunge lina kazi kuu kubwa mbili; ya kwanza kutunga sheria za nchi na ya pili ni kupitisha bajeti ya Serikali ili iweze kupata fedha za kufanyia kazi zake katika mwaka unaohusika.

Mwaka wa Fedha wa Serikali huanza Julai Mosi ya kila mwaka wa kalenda. Ndiyo sababu mikutano yote ya Bunge ya bajeti siku zote hufanyika kuanzia katikati ya Aprili na kumalizika kabla ya Julai Mosi.

Kazi ya Bunge kushughulikia bajeti ya Serikali inaanzia wakati ambapo vitabu vya bajeti hiyo vinapowasilishwa ofisini kwa Spika ili vifanyiwe kazi na Bunge kwenye ngazi ya kamati za Bunge za kisekta kupitia mapendekezo ya bajeti kwa kila wizara.

Baada ya hapo ndipo inafuata hatua ya pili, ambayo ni kuwasilisha makadirio ya kila wizara kwenye Bunge lenyewe.

Kila waziri anawasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake bungeni akifafanua pia shabaha na malengo yanayokusudiwa kutekelezwa na wizara yake katika mwaka wa fedha unaohusika. Wizara zote kwa pamoja zimetengewa jumla ya siku zisizozidi 58 kikanuni za kujadiliwa bungeni.

Waziri mhusika hutoa hotuba ya kuwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka huo na kufuatiwa na maoni ya kamati pamoja na maoni ya msemaji mkuu wa upande wa upinzani anapewa nafasi ya kutoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusu shabaha na malengo hayo yanayokusudiwa kutekelezwa na wizara hiyo.

Baada ya taarifa hizo, mjadala unakuwa wazi kwa mbunge yeyote anayependa kuchangia mawazo yake ama kwa mdomo au kwa maandishi atakayompelekea waziri mhusika na baada ya majadala kufungwa, Bunge linajigeuza kuwa Kamati ya Matumizi kwa ajili ya kupitia kifungu kimoja kimoja cha matumizi yanayopendekezwa.

Ni katika hatua hiyo ndipo baadhi ya wabunge huwa wanatoa hoja ya “kuondoa shilingi”. Maana halisi ya hoja hiyo pamoja na madhumuni yake vimeelezwa katika Kanuni za Bunge kanuni ya 103 (1) hadi (11).

Bunge linapopitisha bajeti ya wizara fulani, maana yake siyo kwamba Bunge limeipatia wizara hiyo fedha taslimu ambazo ziko tayari kutumika. Kinachofanyika na Bunge ni kutoa idhini tu ya kuiwezesha Serikali kukusanya mapato ya kodi na ushuru kwa kiwango hicho kilichoidhinishwa na Bunge. Ni dhahiri kwamba fedha ambayo bado haijakusanywa haiwezi kutolewa.

Kukamilika kwa Bunge kushughulikia makadirio ya wizara ni baada ya Kamati ya matumizi kukamilisha kazi yake na Bunge linarudia, linapokea taarifa kutoka kwenye kamati hiyo ya matumizi, ndipo linapitisha rasmi makadirio ya wizara hiyo.

Baada ya Bunge kumaliza kupitisha makadirio ya bajeti kwa kila wizara, kwa siku zisizopungua sita Kamati ya Bajeti hukutana na Serikali kushauriana kufanya majumuisho kuzingatia hoja zenye masilahi kwa Taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara.

Baada ya zoezi hilo kukamilika, Waziri wa Fedha na Mipango husoma hotuba ya bajeti ya Serikali ikiwa imetanguliwa na taarifa ya hali ya uchumi na mjadala wa hotuba hiyo huwa wa siku saba na huitimishwa kwa Bunge kupiga kura ya wazi.

Ili utekelezaji wa bajeti ya Serikali uanze baada ya kupitishwa na Bunge, mwishoni chombo hicho hupitisha miswada miwili ambayo ni muhimu kwa Serikali ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi (The Appropriation Bill, 2016) na Muswada wa Sheria ya Fedha (The Finance Bill, 2016) ambapo lengo la miswada hii ni kuiwezesha Serikali kukusanya na kutumia fedha kama zilivyopitishwa na Bunge.

Mwandishi ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge. Anapatikana kwa baruapepe:[email protected]