Bunge lishughulike na wajibu wake kwa CAG

Muktasari:

  • Katika masuala ya kifedha pia, Serikali inajiendesha kwa bajeti maalum. Bajeti hiyo kabla haijaanza kazi lazima Bunge liijadili, liipunguze, liiongeze, liibadilishe na hata kuikataa. Kwa hiyo ili Serikali iwepo na ifanye kazi, haiwezi kukwepa mamlaka na wajibu wa Bunge.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge ndicho chombo chenye mamlaka ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Kwa lugha nyingine Bunge ndicho chombo cha pekee ambacho kimepewa mamlaka ya wananchi ya kuiwajibisha Serikali. Bunge linaweza kumwondoa Rais madarakani na kwa hiyo linao uwezo wa kumtia adabu mtu yeyote katika nchi.

Katika masuala ya kifedha pia, Serikali inajiendesha kwa bajeti maalum. Bajeti hiyo kabla haijaanza kazi lazima Bunge liijadili, liipunguze, liiongeze, liibadilishe na hata kuikataa. Kwa hiyo ili Serikali iwepo na ifanye kazi, haiwezi kukwepa mamlaka na wajibu wa Bunge.

Ripoti ya CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hivi karibuni ameweka hadharani ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali za mwaka wa fedha 2016/17 kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Katika ripoti hiyo pamoja na mambo mengine mengi, CAG ameonyesha amekagua fedha za Makusanyo yaliyokusanywa (yaliyo mikononi mwa serikali/yaliyopatikana).

CAG ameonyesha kuwa kwa mwaka 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya Sh29.5 trilioni kutoka kwenye vyanzo vya mapato yote; yaani mapato yatokanayo na kodi, mapato yasiyo ya kodi, mapato yatokanayo na mikopo ya ndani, pamoja na mapato yatokanayo na mikopo ya nje na misaada ya wahisani. Ufafanuzi huu wa CAG umo kwenye ukurasa na 29 katika Jedwali Na. 12 la Mchanganuo wa Bajeti ya Makusanyo.

Ripoti hiyo ya CAG imeendelea kuonyesha kuwa Serikali ilifanikiwa kukusanya Sh25.3 trilioni, na kushindwa kukusanya Sh4.2 trilioni. Fedha ambazo Serikali ilishindwa kukusanya ni sawa na asilimia 14.3 ya Bajeti yote ya mwaka wa fedha 2016/17. Haya yamo kwenye Ukurasa wa 30 na wa 31 wa Muhtasari wa Ukusanyaji wa Mapato ya Fedha Zilizotolewa.

CAG alizihakikisha, akaziona na kuzikagua fedha hizi zilizokusanywa (yaani Sh25.3 trilioni) kwa sababu ziliingia au kuingizwa kwenye Hesabu Jumuifu za Taifa (Consolidated Accounts) jambo ambalo ndiyo utaratibu sahihi wa makusanyo na matumizi ya fedha za taifa letu.

Ripoti ya CAG inaonesha Serikali iliweza kukusanya Sh25.3 trilioni kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kwa mchanganuo maalum ambapo; vyanzo vya kodi (Sh14.27 trilioni), vyanzo visivyo vya kodi (Sh2.072 trilioni), mikopo ya ndani (Sh5.916 trilioni) na mikopo nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo (Sh3.047 trilioni). Mchanganuo huu wa vyanzo ambavyo viliipa fedha Serikali umeoneshwa kwenye ukurasa wa 32 wa Kielelezo namba 6 cha Mwenendo wa Mapato ya Serikali kwa miaka minne.

Maelezo hayo ya CAG yana maana ya kwamba yeye kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliweza kukagua fedha ambazo zimekusanywa na Serikali na kutumika na kama hiyo haitoshi, Serikali ilimpa CAG nyaraka zote muhimu za uwepo wa fedha hizo na ndiyo maana akazikagua.

Utata wa Sh1.5 trilioni

Katika ukaguzi CAG ameonesha kuwa, kati ya Bajeti ya Sh29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya Sh25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote na ilishindwa kukusanya kiasi cha Sh4.2 trilioni, sawa na asilimia 15 kama nilivyoeleza hapo juu.

Ripoti hiyo ya CAG inaonesha kuwa, katika fedha zote zilizokusanywa (Sh25.3 trilioni) ni Sh23.8 trilioni tu ndio zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali na riba (zilitumika). Sh1.5 trilioni zilizobaki hazijulikani ziko wapi. Fedha hizi ambazo ni asilimia 6 ya fedha zilizokusanywa zimeleta utata wa wazi na mjadala mkubwa.

Nimemuona CAG mwenyewe akihojiwa na kituo cha Televisheni cha Azam na akisisitiza ya kwamba “tofauti ya fedha alizokagua na zile ambazo hazionekani inapaswa kushughulikiwa na Bunge” (maneno yangu). Wito wa CAG ni katika jukumu lilelile la kuhakikisha kwamba mihimili ya dola inafanya kazi yake na majibu ya masuala ambayo yeye hakujulishwa yaweze kuwasilishwa kwenye vyombo vinavyohusika na kumaliziwa huko.

Majibu ya Serikali

Serikali na chama kinachoongoza dola vimejitokeza hadharani kujibu ukaguzi wa CAG hasa katika kipengele cha wapi ziliko Sh1.5 trilioni? Ufafanuzi wa Serikali ni kwamba, fedha zote ziko salama na hakuna upotevu wa Sh1.5 trilioni.

Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi, kama ilivyo kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha wameweka bayana kuwa, hicho kinachoitwa kuwa ni pesa zilizopotea ni uongo na uzushi.

Wawakilishi wa chama na serikali wameeleza kuwa kati ya fedha zinazotajwa kupotea au kutoonekana au kutokaguliwa, hizo ni fedha ambazo zilikuwa zinatarajiwa kukusanywa (receivables) pamoja na fedha zilizokusanywa na TRA kwa ajili ya kuzikabidhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali imesisitiza kuwa CAG hajaituhumu kuwa imepoteza fedha na kuwa wanaosema hivyo wapuuzwe.

Maswali muhimu

Kwanza, CAG alipofanya ukaguzi na kuukamilisha na akaibua hoja hizo za ukosekanaji wa fedha hizo (Sh1.5 trilioni), kwa nini Serikali ilishindwa kumpa ufafanuzi huu inaoutoa leo baada ya tuhuma hizi kuwa hadharani?

Pili, Kwa kawaida CAG humpa mkaguliwa yeyote muda wa wiki tatu ili mhusika alete nyaraka na ushahidi juu ya kutoonekana kwa fedha fulani au jambo lililompa CAG wasiwasi. Kama fedha hizi zilikuwa na maelezo kuwa ni makusanyo tarajiwa na Fedha za Zanzibar na tena Serikali ikitumia kurasa tatu tu kulifahamisha Bunge, kwa nini Serikali isingelitumia kurasa tatu hizohizo kumpa CAG maelezo na nyaraka ya fedha hizo?

Tatu, CAG hufanya Exit Meetings (Vikao vya Kuhitimisha Ukaguzi na kuagana na mkaguliwa). Serikali ilifanya vikao hivi na CAG mwezi Januari 2018. Kwa kawaida (uzoefu wangu na kukaguliwa nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF), mkaguliwa huweza kutumia fursa hii (Vikao Hitimishi) kufafanua masuala ambayo hakuyafafanua kwenye zile wiki tatu za muda wa ziada na muda huu wa vikao vya kufungia bado mkaguliwa hakatazwi kumpa CAG nyaraka ili CAG arekebishe wasiwasi wake juu ya mkaguliwa. Kwa nini bado Serikali ilishindwa kutoa ufafanuzi kuwa fedha hizo ambazo hazionekani ni makusanyo tarajiwa (receivables) na zingine ni fedha zilizokusanywa kwa ajili ya Zanzibar?

Nne, Ufafanuzi huu wa Wizara ya Fedha, sawasawa na ule wa msemaji wa CCM, kwa nini usiwe ushahidi tosha kuwa serikali ilifanya makusudi kutompa CAG wakati wa ukaguzi, kipindi cha wiki tatu za nyongeza na hata kwenye vikao vya kuagana? Serikali iliogopa nini kutoa ufafanuzi huo ili kama CAG angeliona inafaa aweze kukagua nyaraka na ajiridhishe na maelezo ya Serikali? Kwa nini Serikali haikumpa Mkaguzi nafasi yake na sasa inalipatia Bunge taarifa ya juujuu kuwa fedha ziko salama na hazijapotea?

Bunge likate mzizi wa fitina

Narejea tena mwanzoni mwa makala hii. Jukumu la Bunge letu kwa mujibu wa Katiba yetu ni kuisimamia Serikali. Sote tunao uzoefu wa huko nyuma. Yapo masuala makubwa yalitokea katika nchi, Serikali ikang’ang’ana kutoa ufafanuzi na kutaka watu wauamini ufafanuzi huo. Bunge (huko nyuma) lilipounda kamati maalum za uchunguzi mara zote lilikuta ya kwamba Serikali ilificha mambo mengi sana.

Mfano mzuri ni Oparesheni Tokomeza ambayo maelezo ya awali ya Serikali yalikuwa kwamba Oparesheni imeendeshwa vizuri na kwa mafanikio. Bunge lilipounda Kamati Maalum likakuta Oparesheni ile ilifanywa kinyama, kwa uonevu mkubwa na iliacha vidonda visivyoponyeka. Baada ya Kamati ya Bunge kumaliza kazi yake mawaziri wanne walijiuzulu mara moja. Iko mifano mingine mingi sana.

Katika hili la tuhuma hizi nzito kwa Serikali, kwa sababu CAG alishamaliza kazi yake na hakupewa ushirikiano wowote na Serikali (Serikali ikimficha kila kitu kuhusu matumizi ya fedha hizi), ni lazima Bunge liunde Kamati Maalum ili ichunguze fedha hizo zilikwenda wapi?

Spika wa Bunge atimize wajibu wa Bunge kikatiba, aunde Kamati Maalum au aruhusu Kamati mama ya Bunge kwenye masuala haya yaani PAC, ikabidhiwe jukumu la kufanya uchunguzi maalum wa fedha hizi na ama Bunge linaweza pia kutumia wataalamu maalum huru na hata taasisi za kimataifa za ndani na nje ya nchi kuweza kufanya ukaguzi maalum.

Kwa hali ilipofika na kwa asili ya uzito wa tuhuma hizi, itakuwa ni aibu sana na itakuwa ni kosa kubwa sana ikiwa Bunge litakwepa kwa namna yoyote ili kufuatilia jambo hili kwa weledi na mamlaka yake. Taarifa ya leo ya Serikali (sawa na ile ya msemaji wa CCM) zinamaanisha kuwa Serikali imetumia pesa, Serikali imemkwepa CAG asikague pesa hizo, na sasa Serikali inautangazia umma matumizi ya fedha hizo (Serikali imetumia, imejikagua na inatangaza ukaguzi wake).

Uchunguzi maalum kwenye fedha hizi ndiyo utatupa mwanga, Serikali itapata haki yake na taifa litapata haki yake, na kama serikali inasingiziwa kinachoweza kutuhitimishia kuwa inasingiziwa ni Kamati Maalum ya Bunge. Bunge litimize wajibu wake.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])