CUF waenda kortini kumkataa Jaji

Muktasari:

Chama hicho kiliwasilisha maombi kikimtaka Jaji Kihiyo na kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo Desemba 6 mwaka jana, pamoja na mambo mengine kikidai hakina imani naye kuwa atatenda haki.

Dar es Salaam. Licha ya Jaji Sekieti Kihiyo kugoma kujitoa katika kesi ya CUF, chama hicho kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kimeshikilia msimamo wa kumkataa baada ya kuamua kwenda Mahakama ya Rufaa kumpinga.

Chama hicho kiliwasilisha maombi kikimtaka Jaji Kihiyo na kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo Desemba 6 mwaka jana, pamoja na mambo mengine kikidai hakina imani naye kuwa atatenda haki.

Walidai wameona mwenendo wake unaashiria kuubeba upande wa pili (wadaiwa).

Katika uamuzi wa Desemba 14 mwaka jana, Jaji Kihiyo aligoma kujitoa katika kesi hiyo akidai kuwa sababu zao hazina msingi na wadai wanachokifanya ni kumtafuta jaji wanayemtaka wao. Aliamua kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo na alipanga kuisikiliza jana.

Hata hivyo, jana kesi hiyo haikuendelea na Jaji Kihiyo aliiahirisha hadi Machi 22 baada ya wadai kusisitiza kutomkubali.

Wakili wa wadai hao, Juma Nassoro aliieleza mahakama kuwa wameamua kwenda mahakamani kukata rufaa kupinga uamuzi wake.

Kesi hiyo imefunguliwa na sehemu ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa CUF, wanaoungwa mkono na Maalim Seif dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wadaiwa wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara, Magdalena Sakaya na wanachama tisa waliosimamishwa. Mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.