Camfed lilivyomuokoa msichana Victoria

Victoria Fedelis, mmoja wa wanufaika wa mpango wa asasi ya Camfed inayojihusisha na kusaidia kielimu watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Picha na Sharon Sauwa

Muktasari:

TAKWIMU

30 milioni: Idadi ya watoto wanaoishi mitaani na katika mazingira hatarishi  barani Afrika

199,008: Idadi ya watoto waliosaidiwa na Camfed tangu mwaka 2006. 

Victoria Fedelis mkazi wa kijiji cha Gongwe Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro,  ni miongoni mwa wasichana wanaoishi katika mazingira magumu ambao wamelazimika kuacha kujiendeleza kielimu ili kuwasaidia wadogo zake kutokana na kipato kidogo cha familia.

Kwa mujibu wa Shirika laUmoja wa Mataifa  la Kuhudumia Watoto (Unicef) inakadiriwa kuwa watoto 120 milioni wanaishi  mitaani na katika mazingira magumu duniani, huku bara la Afrika likiwa na watoto 30 milioni.

Tanzania inatajwa kuwa  miongoni mwa nchi zenye changamoto kubwa kwa kuwa na ongezeko la watoto hao kila kukicha.

“Baba yangu alimtelekeza mama yangu tukiwa wadogo, hivyo tulilelewa na mama ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza nyanya. Maisha yalikuwa magumu fedha iliyopatikana ilikuwa ni kwa ajili ya chakula, malazi na afya,”anasema.

Anasema alipofika darasa la saba alifaulu na kuchaguliwa kwenda kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Gondwe Wilaya ya Kilosa lakini kutokana na maisha aliyokuwa akiishi nyumbani, alikata tamaa  ya kuendelea na masomo.

 “Nilikata tamaa kabisa, niliona hakuna uwezekano wa kusoma tena baada ya kuona hali ya maisha tuliyokuwa tukiishi ingawa nilifaulu na kuchaguliwa kwenda sekondari,” anasema.

Anasema alikaa muda mrefu nyumbani akisubiri labda atatokea mtu wa kumfadhili ili aweze kuendelea na masomo yake ya sekondari.

Victoria anasema akiwa nyumbani ulipita usajili wa kuangalia watoto waliokuwa katika mazingira hatarishi na kubahatika kupata ufadhili wa kusomeshwa.

 “Nikiwa mazingira ya nyumbani alikuja mwalimu mkuu wa sekondari, kiongozi wa kijiji na mwalimu wa shule ya msingi, wakatuhoji jinsi gani mama alivyoshindwa kunisomesha mimi elimu ya sekondari. Mimi nilijieleza yote,”anasema.

Anasema baada ya mahojiano hayo,  waliitwa yeye na kaka yake  kusaini mkataba na shirika lilajihusisha na kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi la Camfed linalojihusisha na kusaidia watoto wanaoshi katika mazingira magumu.

“Ndoto yangu ilitimia nikaanza masomo yangu ya sekondari kwa kulipiwa ada ya shule na gharama nyingine za kuniwezesha kusoma na shirika hilo,”anasema.

Victoria anasema ingawa Serikali imeondoa ada kwa wanafunzi wa msingi hadi sekondari lakini suala la ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi ni jambo la msingi,  ili kuwawezesha wanafunzi wa kike kuepuka changamoto wanazokutana nazo njiani na nyumbani.

“Kuna changamoto kwa mfano,  mtoto wa kike akirudi nyumbani ana shughuli za shamba inabidi amsaidie mzazi, kuna kupika na kuwasaidia wadogo zako unajikuta huna muda wa kusoma lakini ukikaa bweni unakuwa na muda mrefu wa kusoma,” anasema.

Anasema yeye alikuwa analazimika kutembea umbali wa kilomita 10 kwenda na kurudi shuleni kila siku na alikuwa anaamka saa 11 asubuhi ili awahi shule.

Anasema aliporudi nyumbani alikutana na shughuli za nyumbani ikiwa ni pamoja na kufanya usafi, kupika na kuwalea wadogo zake, jambo lililomkosesha muda wa kusoma.

“Watoto wa kiume mara nyingi wanapata muda wa kujisomea wakirudi nyumbani kwa sababu hawakutani na kazi, lakini kwa watoto wa kike inakuwa ngumu,”anasema.

Maisha kwa  sasa

Baada ya kumaliza shule, Victoria hakuchaguliwa kujiunga na masomo ya juu ya sekondari na hivyo alibakia nyumbani ingawa alikuwa na kiu ya kwenda chuoni.

Uamuzi wa kutohangaika  kutafuta elimu zaidi, ulitokana na wadogo zake wanaomfuatia kuhitaji msaada wake kimasomo na hivyo aliamua kujikita katika ujasiriamali.

“Nilianza kupika maandazi baada ya kupata mtaji kutoka katika kampuni ya Wachina ambayo nililipwa Sh15,000 kama ujira wa kufanya kazi ya kupanda mahindi katika shamba lao. Nilipopata fedha hizo nilizigawa nusu nikanunua debe la mahindi kwa ajili ya chakula nyumbani na zilizobaki nilianzisha mradi wa kupika maandazi,”anasema.

Anasema pia utaratibu wa Camfed baada ya kumaliza masomo chini ya ufadhili wa shirika hilo, ni mnufaika kuwasaidia wengine ikiwa ni kurudisha fadhila za kusomeshwa.

Harakati za Camfed

Mwenyekiti wa Bodi ya Camfed, Jeanne Ndyetabura anasema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 2006,  miradi   inayotekelezwa kwa kushirikiana  na jamii imeweza kuwasaidia watoto 199,008 wa shule 675 za msingi na sekondari nchini.

Anasema watoto hao wamepata msaada wa ufadhili wa  shule kama vile ada, sare za shule, malazi na vifaa  vya usafiri.

“Ufaulu kwa wanafunzi wanaopata ufadhili umefikia asilimia 55.1 kwa mwaka 2016 kutokea asilimia 50.3 mwaka 2015. Na kwa shule zinazopata ufadhili, ufaulu umefikia asilimia 57.5 kwa mwaka 2016 kutoka asilimia 55.4  mwaka 2015,”anasema.

Jeanne anaomba wasichana wanaoishi katika mazingira magumu kupewa kipaumbele, pindi wanapoomba kujiunga  katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu.

“Kwa mfano tungetamani kuona wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu wanapatiwa asilimia 100 ya mikopo wa elimu ya juu pale wanapomba. Pia tunaomba kuwapo kwa  njia mbadala za kujifunzia hasa kwa wanafunzi  waliokwishatoka katika mfumo rasmi wa elimu,”anaeleza.