Daktari aliyebobea katika tiba na dawa

Mtaalamu wa Dawa na Tiba, Dk Sajjad Fazel

Muktasari:

  • Pia, baadhi yao wanapomaliza masomo huwaza kupata kazi kubwa na ikiwa haitatokea, basi hubaki kulalamikia ugumu wa maisha.
  • Mtaalamu wa Dawa na Tiba, Dk Sajjad Fazel (25) anasema kilichomuwezesha kutimiza ndoto zake ni bidii katika kuifikia mipango mizuri aliyojiwekeza kwenye maisha yake tangu akiwa mdogo.

Miongoni mwa vitu ambavyo huwafanya vijana wengi kutofikia ndoto zao za kimaisha ni kutokuwa na malengo na hata wakiwa nayo, hawawezi kusimamia utekelezaji wake.

Pia, baadhi yao wanapomaliza masomo huwaza kupata kazi kubwa na ikiwa haitatokea, basi hubaki kulalamikia ugumu wa maisha.

Mtaalamu wa Dawa na Tiba, Dk Sajjad Fazel (25) anasema kilichomuwezesha kutimiza ndoto zake ni bidii katika kuifikia mipango mizuri aliyojiwekeza kwenye maisha yake tangu akiwa mdogo.

“Nilitamani kuwa daktari, nikaweka mkakati katika kusoma masomo ya sayansi na sasa imekuwa. Ndoto hii imetimia kwa sababu nilitembea kwenye mipango yangu,” anasema.

Kilichomsukuma kusomea udaktari ni hali ya afya ya baba yake ambaye kutokana na ugonjwa wa kisukari alihitaji zaidi kuwa karibu na wataalamu wa afya, hivyo aliamini ikiwa atakuwa daktari itakuwa rahisi kumuhudumia.

“Baba yangu kitaaluma ni mhasibu, sikuwahi kupenda kazi ya baba yangu ila nilipenda kusomea kitu kitakachoniwezesha kumsaidia yeye na wengine wenye uhitaji. Kupitia udaktari niliamini nitaendesha maisha yangu anasema.

Dk Sajjad ambaye kwa sasa ni Meneja Msaidizi wa Hospitali ya Sanitas, jijini Dar es Salaam anasema hakuwahi kuchoka kujitolea kufanya kazi wakati alipokuwa hajaajiriwa tofauti na mtizamo wa vijana wengi ambao hupenda kupata mishahara minono mara wanapomaliza masomo yao.

Safari yake ya maisha

Anasema safari ya maisha yake kielimu ilianzisha Shule ya Msingi Agakhan jijini Dar es Salaam, kisha Shule ya Sekondari ya Mzizima kabla ya kujiunga na Heaven Peace Academy alikohitimu kidato cha sita.

Kwa kuwa aliwekeza katika masomo ya sayansi, haikuwa kazi ngumu kwake kuchagua kozi ya udaktari aliyoiota tangu akiwa mdogo.

Anasema alijiunga na Chuo Kikuu cha Manipal, nchini India ambako alianza safari ya miaka sita akibobea katika masomo ya udaktari wa tiba na dawa.

Anasema kozi hiyo imesomwa na watu wachache na kwamba kwa Tanzania mpaka sasa ni madaktari 10 tu waliobobea kwenye masuala ya tiba na dawa.

Anasema alitumia muda wake wa likizo kufanya kazi kwa kujitolea katika maeneo mbalimbali ili aweze kuhudumia wagonjwa kama alivyotamani siku zote.

“Ninaamini kwenye kujitolea, hakuna kitu kizuri unachoweza kupata kama hutakuwa na moyo wa kujitolea. Japo nilikuwa bado mwanafunzi, nilipenda kuona wagonjwa wakihudumiwa kikamilifu kwa kupata tiba kulingana na magonjwa yao,” anasema.

Miongoni mwa maeneo aliyowahi kufanya kazi kwa kujitolea ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Mamlaka ya chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Anasema baada ya miaka sita, alihitimu masomo yake na kwamba haikuwa kazi ngumu kuajiriwa kwa sababu tabia yake ya kujitolea ilifanya taasisi nyingi kumuamini.

“Unajua vijana wengi wanasahau, wanabaki kulalamika ajira hakuna wakati wanaweza kuanza kazi kwa kujitolea. Ukishaonwa kwamba unajituma itakuwa rahisi kwako,” anasema.

Kazi nyingine anazofanya

Mbali na udaktari, Dk Saajad amekuwa akiitumia taaluma yake kuandika makala mbalimbali za kijamii zinazohusu masuala ya afya ili kuisaidia jamii.

“Huwa naandika kupitia gazeti la The Citizen, tunawajibika kuielimisha jamii kuhusu afya zao, sio mpaka waugue na kuja hospitali ndipo tuwatibu,” anasema.

Pia huwa anafundisha kupitia vipindi vya redio, runinga na mitandao ya kijamii ikiwamo, facebook na twitter, ni mkakati wake kuhakikisha anaendelea kuishauri jamii namna ya kuwa na afya bora.

Taaluma ya udaktari

Dk Saajad anasema wataalamu wa afya kama zilivyo taaluma nyingine wanayo miiko na wajibu wao.

Anasema ni jukumu la jamii kuitambua na kuithamini taaluma hiyo kama zilivyo nyingine kwa kuwa inahusika moja kwa moja na maisha yao.

“Tunayo miiko yetu lakini jamii inapaswa kututambua na ituthamini kwa sababu tunapowahudumia, tunahusika moja kwa moja na maisha yao,” anasema.

Familia

“Bado sijaona, naamini Mungu akinijalia mwaka huu au mwakani nitafanya hivyo. Natamani sana kuwa na familia yenye furaha na upendo,”anasema.

Wito wake

Dk Sajjad anasema ili kujenga jamii yenye usawa ni lazima kila mmoja atambue wajibu wake na kufanya kazi kwa bidii.

Anasema bidii inalipa na kwamba hakuna kitu kinachoweza kupatikana kiurahisi ikiwa hakutakuwa na bidii yoyote ya kukitafuta.

“Bidii hii inapaswa kuanzia kwenye ngazi ya kifamilia, kila kitu unachopanga kukifanya lazima ukifanywe kwa bidii uli ufanikiwe. Baba na mama wakitimiza wajibu wao familia yao itakuwa bora na watoto watafikia malengo makubwa waliyojiwekea,”anasema.

Anawashauri vijana hasa wanaohitimu elimu ya juu kuacha kuchagua kazi badala yake wajitume kwa kila wanachoweza kufanya kihalali kiwasaidia kuingia kipato.

“Ukiendelea kulalamika kwa kukosa ajira wakati hutaki hata kuonyesha ujuzi wako haitasaidia, vizuri tuanze kwa kuona ni wajibu wetu kulitumikia taifa. Mwalimu ukijitolea kufundisha wanafunzi zikitokea nafasi utaweza ku”