Dj Sinyorita kutoka XXL mpaka redioni kwako

Akiwajibika jukwaani

Muktasari:

Kutokana na upekee wa kazi anayoifanya, Starehe ilimtafuta na kufanya mahojiano naye ambapo amezungumzia mengi kuhusu kazi na maisha yake.

Madj ni watu muhimu kwenye muziki. Ni mfano wa ngazi zenye uwezo wa kushusha au kuupandisha wimbo wowote pale wanapoamua. Ili kuthibitisha umuhimu wao jua kwamba, u-Dj ni moja ya nguzo za  muziki wa Hip Hop.

Hata hivyo, duniani kuna idadi kubwa ya ma-Dj wa kiume kuzidi wa kike na hii imesababisha kazi hii kuonekana ni ya kuime, ingawa kuna baadhi ya wanawake wamevunja fikra hizo kwa kuamua kujitosa kwenye tasnia na kufanya u-Dj,  miongoni mwao ni Dj Sinyorita.

Jina lake halisi ni Aisha Said. Ni Dj katika kituo cha redio Clouds FM na kazi zake zinasikika mara nyingi kwenye kipindi cha XXL kinachoruka kuanzia saa 7.00  mchana mpaka saa 10.00  alasiri kuanzia Jumatatu hadi  Ijumaa.

Kutokana na upekee wa kazi anayoifanya, Starehe ilimtafuta na kufanya mahojiano naye ambapo amezungumzia mengi kuhusu kazi na maisha yake.

Starehe: Lini uligundua una wito wa kuwa Dj?

Dj Sinyorita: Muda mrefu sana, tangu nikiwa shule. Nilikuwa napenda sana kusikiliza muziki na kwa kipindi kile Dj wa kike Tanzania niliyekuwa namsikia alikuwa ni Dj Fetty tu. Kupitia yeye nikajikuta natamani sana kuwa Dj na nikahisi kwamba natosha kabisa kuingia katika taaluma hii.

Starehe: Kwa hiyo safari yako kwa ujumla ilikuwaje mpaka kufikia hapa ulipo?

Dj Sinyorita: Kwanza niseme tu mimi nimekulia na kusomea Dodoma na ili kutimiza ndoto yangu nilihisi kuna ulazima wa kutoka kule kwenda Dar es Salaam. Nilipofika nikaunganishwa na bosi mmoja wa ‘Maisha Club’, nikamueleza shida yangu kwamba nahitaji kujifunza u-Dj, na akanisaidia kwa kunikabidhi kwa Dj wa hapohapo ili anifundishe. Nakumbuka mtihani wa kwanza kupewa niliambiwa nikatafute nyimbo zisizopungua 200 niziweke kwenye CD na nilipewa mtihani huu kama kipimo cha kwamba najua muziki kwa sababu Dj yeyote silaha yake ni nyimbo nzuri.

Baada ya pale nikaendelea kufundishwa jinsi ya kuchanganya nyimbo na vitu vingine muhimu. Kipindi hicho nilikuwa naishi Ubungo na Maisha Club ipo Masaki, kwahiyo nilikuwa naenda kila siku kujifunza. Baada ya kuweza kidogo nikajiunga na kundi moja la ma-Dj. Huko walikuwa wanafundisha lakini pia walikuwa wanapiga muziki kwenye kumbi za starehe kila mwisho wa wiki, kwa hiyo na mimi nilikuwa nazunguka nao na kuna wakati nilikuwa napata fursa ya kupiga. Baada ya pale nikaingia kwenye mashindano ya u-Dj ya Street Music, huko nilikuwa Dj wa kike peke yangu na nakumbuka nilifika mpaka fainali lakini sikufanikiwa kushinda. Kisha baadae nikapata kazi Samaki Samaki na hapo sasa watu ndiyo wakaanza kunijua, na chaneli zangu zilipokomaa nikapata ajira ‘East Africa Radio’; nilipotoka hapo ndo nikapata nafasi hapa Clouds Fm.

Starehe: Wazazi wako wana maoni gani kuhusu hiki unachokifanya?

Dj Sinyorita: Mimi kwanza wazazi wangu wametengana na hata kule Dodoma nilikuwa naishi na mama tu; baba yangu yupo huku Dar. Na nikushangaze tu kwamba mpaka leo hii, baba yangu anasikia juu juu tu kwamba mimi ni Dj, sijawahi kumwambia. Mama yangu yeye anafahamu kwa sasa lakini mwanzo ilikuwa ni ngumu sana kunielewa.

Starehe: Unamaanisha nini unaposema hujawahi kumwambia baba yako kuhusu kazi unayofanya; kwani huna mawasiliano naye?

Dj Sinyorita: Nina mawasiliano naye lakini hatuna ukaribu namna hiyo, si unajua tena haya mambo ya wazazi kutengana?

 Starehe:  Katika konakona zote ulizopitia kuelekea ndoto yako, umekutana na changamoto gani kama Dj wa kike?

Dj Sinyorita: Kuwa Dj mwanamke kuna changamoto kwa kweli na moja kubwa niliyokumbana nayo ni kutoheshimiwa na baadhi ya watu. Yaani kuna mtu mwingine kwa sababu wewe ni mwanamke na unafanya u-Dj basi anakuchukulia poa tu, anakuwa na mtazamo hasi juu yako. Lakini changamoto nyingine ni kwamba kwa Tanzania bado u-Dj haujawa kazi ya kuthaminiwa, ingawa kuna baadhi ya watu na makampuni wanafahamu umuhimu wetu ikiwemo Clouds Media, lakini wengi wanatuchukulia kama watu wa kawaida tu wakati sisi ni watu muhimu kwa ajili ya kukuza muziki.

Starehe: Je unafikiria kwenda shule kuongeza utaalaamu zaidi juu ya hiki unachokifanya?

Dj Sinyorita: Ndiyo nina mpango huo, lakini nikienda sitasoma u-Dj pekee, nafikiria kwenda kusoma muziki kwa ujumla kwa sababu nina mpango wa kuwa mtayarishaji wa muziki.

Starehe: Jina la Sinyorita limetoka wapi?

Dj Sinyorita: Sinyorita ni neno kutoka katika lugha ya Kihispaniola na linamaanisha ‘mwanamke’;  kwa hiyo mimi niliamua kuongezea Dj hapo mbele ili limaanishe Dj Mwanamke.

Starehe: Kila binadamu ana uwezo na mapungufu katika kazi anayoifanya. Wewe uwezo wako katika u-Dj upo kwenye nini na mapungufu yako yapo kwenye nini?

Dj Sinyorita: Mapungufu yangu ni kwenye baadhi ya ujuzi tu, yaani kuna mambo ma-Dj wenzangu wanafanya lakini mimi bado sijayaweza. Na uwezo wangu ni kwamba najua kuchagua nyimbo nzuri, najua kuchanganya nyimbo lakini pia nina muonekano mzuri.

Starehe: Vipi kuhusu uhusiano?

Dj Sinyorita: Aaah! Mimi sina mchumba wala sijaolewa, ila nina mpenzi na tupo katika uhusiano kwa muda mrefu, karibu miaka mitano sasa.

Starehe: Huyu mpenzi uliyenaye anaichukuliaji kazi yako?

Dj Sinyorita: Hana tatizo kwa sababu hata yeye ni Dj pia na ndiye aliyepewa kazi ya kunifundisha kipindi nilipofika Dar es Salaam kutoka Dodoma.

Starehe: Nje ya u-Dj unafanya nini kingine cha kukuongezea kipato?

Dj Sinyorita: Sifanyi kwa kweli, lakini nina mipango ya kujaribu ujasiriamali siku za usoni.

Starehe: Mtaani kuna ma-Dj wa kike ingawa ni wachache, Je wewe umeshawahi kufikiria kuwasaidia labda kwa kuanzisha lebo ya ma-Dj wa kike?

Dj Sinyorita: Nimewahi kufikiria lakini kwa sasa hivi hicho kitu siwezi kukifanya kwa sababu kwa mtazamo wangu hata mimi bado sijawa imara kiasi cha kuweza kuwabeba wengine. Labda tu ninachokifanya kwa sasa ni kuwasaidia ushauri.

Swali: Madj wa Tanzania mnalalamikiwa kwamba mnapiga nyimbo nyingi za nje hasa Nigeria kuliko mnavyopiga za nyumbani. Wewe unalizungumziaje suala hili?

Dj Sinyorita: Tatizo letu Watanzania hatupendi kuukubali ukweli; na naomba nisieleweke vibaya katika hili. Hivi kama wimbo wa Nigeria umetengenezwa vizuri kuzidi wa Tanzania kwa nini mimi kama Dj nisiucheze wa Nigeria? Katika hili dawa si kulalamika, ni wasanii kujituma ili kazi zao zivutie. Lakini kwa kuongeza ni kwamba, Dj mwenye maadili hapigi nyimbo kwa upendeleo, anapiga nyimbo yoyote nzuri.

Swali: Je, una mtoto au labda umeshawahi kubeba ujauzito?

Dj Sinyorita: Sina mtoto, ila nilishawahi kupata ujauzito zamani. Lakini kwa bahati mbaya sikufanikiwa kujifungua, mimba ilitoka.

Swali: Mikono yako ina uwezo wa kufanya kazi gani mbali na u-Dj?

Dj Sinyorita:  Kusuka siwezi  ila nafanya kazi zote za nyumbani. Nafua, naosha vyombo na napika pia. Tena hapa kwenye kupika ndio usiseme, naweza kupika pilau, biriani, wali, chapati, maandazi, dagaa, mlenda na ninaposema kupika namaanisha kupika, yaani nikiingia jikoni vinanukia si mchezo.

Swali:  Unaweza kueleza jinsi unavyokumbana na usumbufu kutoka kwa wanaume wanaokutaka kimapenzi?

Dj Sinyorita: Ishu ya mtoto wa kike kusumbuliwa na wanaume  ni jambo la kawaida, si kwa ma-Dj wa kike tu, kila mwanamke mzuri. Na kwa taarifa yako mtoto wa kike usipokuwa unatongozwatongozwa unaweza kujikuta unakwenda kwa babu ukidhani labda una gundu. Binafsi nasumbuliwa lakini najua jinsi gani ya ‘kudeal’ nao.

Starehe: Mashabiki walikuwa wanamshindanisha Diamond na Alikiba, lakini mara wakamletea Diamond mpinzani mwingine ambaye ni Darassa. Kwa mtazamo wako unahisi nafasi ya Diamond inafikika?

Dj Sinyorita: Inafikika kabisa  lakini ni lazima huyo msanii anayetaka kumfikia Diamond aongeze juhudi mno kwa sababu Diamond ni msanii mkubwa  na kila siku anazidi kufanya vitu vikubwa, anazidi kwenda juu, hashuki, kumfikia ni kazi ngumu lakini inawezakana kwa asilimia mia moja.