Emmanuel na ndoto ya kuongoza mtihani wa Taifa

Emmanuel John akiwa na baba yake John Buseme, baada ya kuibuka mwanafunzi bora katika mahafali ya kuhitimu darasa la saba Shule ya Kwema Modern ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Shija Felician

Muktasari:

  • Mbele ya umati wa wazazi, walimu na wageni waalikwa waliofika shuleni hapo kwa ajili ya mahafali hayo, jina la Emmanuel John lilisikika kwa zaidi ya mara tano.

Kila aliyekuwapo katika hafla ya mahafali ya miaka 16 Shule ya Msingi Kwema Morden iliyopo mjini Kahama, Shinyanga alitamani kumuangalia pale jina lake lilipokuwa likitajwa mara kwa mara.

Mbele ya umati wa wazazi, walimu na wageni waalikwa waliofika shuleni hapo kwa ajili ya mahafali hayo, jina la Emmanuel John lilisikika kwa zaidi ya mara tano.

Awali mwanafunzi huyo aliitwa kwa ajili ya kupokea zawadi baada ya kuongoza katika somo la Hisabati kisha ikafuata Maarifa ya jamii, Kiswahili na masomo mengine. Mwishowe akaibuka mshindi wa jumla katika masomo yote.

Haikuishia hapo hata ilipotajwa zawadi ya mwanafunzi bora aliyefanya vizuri katika michezo, jina lake likachomoza tena na kuitwa jukwaani baada ya kushika nafasi ya kwanza.

Wakati sherehe hizo zikiendelea, nilishangazwa na kipaji cha mwanafunzi huyo ambaye wakati huu tena alipanda jukwani na kucheza ngoma nzuri akishirikiana na wanafunzi wenzake.

Ngoma hiyo ya Kisukuma maarufu kwa jina la gobogobo ilitoa burudani nzuri, lakini kivutio kikubwa ilikuwa ni kwa Emmanuel ambaye alionekana kucheza kwa ustadi mkubwa.

Jambo hilo lilinusukuma na kutaka kujua historia ya mwanafunzi huyo kwa undani, lakini pia anawezaje kufanya vizuri katika masomo na hata masuala nje ya taaluma.

Kwake, siri ni hii: ‘’… siri ya kukufanya vizuri ni kufanya kila kitu kwa kikamilifu na kutopuuzia ninachojifunza. Lakini kubwa zaidi ni kumtanguliza Mungu katika kila kitu,’’ anasema mwanafunzi huyo kwa uso wa bashasha.

Lakini Emmanuel anasema jambo lingine linalosababisha kufanya vizuri ni uwepo wa miundombinu bora ya kujisomea shuleni hapo, huku walimu ambao wamekuwa msaada mkubwa kwake wakichochea mafanikio hayo.

“Hapa shuleni mazingira ni rafiki , walimu wapo wa kutosha, lakini wamekuwa wakitufundisha kwa upole na urafiki mkubwa jambo linalotuongezea hamasa ya kupenda shule.

Akizungumzia historia yake, Emmanuel anasema tangu alipoanza masomo ya chekechea amekuwa akishika nafasi ya kwanza na mara moja tu alianguka na kushika nafasi ya pili jambo lilomkosesha furaha.

“Nakumbuka nilikuwa darasa la tatu baada ya matokeo nikajikuta nimeshika nafasi ya pili, roho iliniuma sana sikuwa na amani hata kidogo na wakati wote nilikua mnyonge nikitafakari namna ya kurudi katika nafasi yangu.”

Anakiri kwamba kufanya kwake vibaya kwa mwaka huo ni matokeo ya kutozingatia masomo na baada ya kugundua hilo alihaidi kubadilika mpaka atakapo maliza elimu yake.

“Lengo langu ni kuongoza katika mtihani wa kitaifa na naamini kwa uwezo wa Mungu nitafanikisha kwani ni jitihada na nimejiandaa vyema kwa hilo,”anasisitiza.

Baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Jonh Buseme anasema anaamini palipo na nia pana njia na kwamba anachofanya kwa sasa kumuombea kwa Mungu ili ndoto za mwanawe zitimie.

“Siku zote amekuwa akiamini katika kufanya vizuri, lengo lake ni kuongoza kitaifa ndiyo maana anafanya juhudi ili kufanikisha hilo.”

Hata hivyo, Buseme anasema Emmanel ambaye ni mtoto wake wa pili ni tofauti na watoto wake wengine wanne. Huyu amekuwa na tabia tofauti za kupenda kusoma na kusali sana.

“Huyu bwana kabla hajaanza kufanya chochote ni lazima asali, nafurahishwa na tabia yake ya kupenda kumtanguliza Mungu kabla ya kitu chochote na ndiyo maana naamini atafanikisha ndoto zake.”

Ratiba yake ya kila siku

Kutumia ratiba kwa usahihi ni siri nyingine ya mafanikio kwenye masomo yake darasani. Anasema kila siku huamka saa 11.00 asubuhi.

“Nikiamka tu jambo la kwanza ni kusali ili kumshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kumuomba aniongoze siku nzima kisha najiandaa na ikifika saa 11.30 naingia darasani kusoma kwa muda mchache kabla ya kuungana na wenzangu kufanya usafi wa kawaida wa asubuhi,”anaelezea.

Awapo darasani, anasema humsikiliza mwalimu na kufanya kazi zote anazoachiwa kufanya.

Hajawahi kumiliki simu

Kwake Emmanuel simu na mitandao ya kijamii ni adui mkubwa wa maendeleo yake na kwamba hatarajii kuimiliki mpaka pale atakapofikisha umri wa utu uzima.

‘’Unajua wanafunzi wengi wanashindwa kufanya vizuri kutokana na kumiliki simu za mikononi, hivyo muda mwingi badala ya kuutumia kusoma wanautumia katika mitandao ya kijamii na kujikuta wakipotea,”anasema na kuongeza:

“Mitandao ya kijamii ina faida, lakini pia ina hasara kubwa kwa wanafunzi maana wengi hawajui jinsi ya kuitumia na kujikuta wakitumbukia katika masuala ya kuiga mambo yasiyofaa.’’

Mkurugenzi ataja siri ya mafanikio

Mkurugenzi wa Shule hiyo, Paulini Mathayo anasema siri kubwa ya kufanya vizuri kwa shule yake ni uwepo wa miundombinu bora ya kufundishia. Lakini pia mwanafunzi anapougua, hupata huduma bora.

“Niliamua kujenga kituo cha afya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanafunzi wangu, lakini pia motisha kwa walimu na wanafunzi wangu ni jambo la msingi,’’ anaeleza.

Anatoa mfano wa matokeo ya mwaka jana ambapo shule hiyo ilitoa wanafunzi wanane kati ya 10 walioingia katika 10 bora kitaifa.