MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Fasihi na dhima ya utunzaji wa historia ya jamii

Muktasari:

  • Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na masimulizi kutoka kwa waliopata kuwapo katika kipindi husika na kusoma vitabu vya historia. Fasihi ni njia mojawapo iwezayo kumjuza mtu historia ya jamii bila kujali ni fasihi simulizi au fasihi andishi. Katika makala haya leo, tuangalie mchango wa tamthilia ya Kiswahili katika kutunza historia ya jamii ya Watanzania.

Jamii yoyote hupitia katika vipindi mbalimbali vya kihistoria. Aghalabu, tunapotaka kuifahamu historia ya jamii huwa tunatumia njia mbalimbali kupata taarifa husika.

Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na masimulizi kutoka kwa waliopata kuwapo katika kipindi husika na kusoma vitabu vya historia. Fasihi ni njia mojawapo iwezayo kumjuza mtu historia ya jamii bila kujali ni fasihi simulizi au fasihi andishi. Katika makala haya leo, tuangalie mchango wa tamthilia ya Kiswahili katika kutunza historia ya jamii ya Watanzania.

Tunaweza kuigawa historia ya jamii ya Watanzania katika vipindi mbalimbali ambavyo wanajamii wamepitia. Vipindi hivyo ni pamoja na kipindi cha kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni, wakati na baada ya uhuru, kipindi cha kukata tamaa ambacho hujulikana pia kama kipindi cha giza na wakati wa kushamiri kwa utandawazi.

Katika vipindi hivi vya kihistoria kuna matukio mbalimbali yaliyojili. Matukio hayo huakisiwa vyema na kazi mbalimbali za kifasihi kupitia vipengele vyake mbalimbali. Katika kuonyesha dhima hii ya fasihi, tutatumia utanzu wa tamthilia kudhihirisha inavyoakisi historia ya jamii.

Kabla ya ukoloni, jamii nyingi zilikuwa zikienzi mila na desturi zao. Zilijishughulisha na kazi mbalimbali kwa lengo la uzalishaji mali na kuzienzi mila na desturi zao kupitia mivigha, jando na unyago vikiwamo; matambiko. Tamthilia faraguzi ya wakati huo, ilijikita katika kuakisi shughuli zilizokuwa zikifanywa na wanajamii.

Katika kipindi cha ukoloni (1885-1960), shughuli za kijamii hazikuweza kufanyika ipasavyo kwa kuwa jamii ilikuwa katika migogoro mbalimbali na wakoloni, awali Wajerumani na baadaye Waingereza. Hata hivyo, tamthiliya ya wakati huu ililenga katika kuliburudisha tabaka tawala la kikoloni.

Baada ya uhuru, maudhui ya kazi ya fasihi yalibadili mwelekeo. Katika kipindi hiki kulikuwa na wasomi wazawa walioandika. Tamthilia za wakati huu zililenga katika kusherehekea uhuru uliopatikana, kuwakejeli wakoloni, kuwakejeli wasomi wazawa waliobeza utamaduni wao na kushadidia ule wa kikoloni. Zililenga pia kuwakweza wapigania uhuru wa kizalendo ambao kati yao walijitoa hata kufa. Tamthilia za “Mkwava wa Uhehe” (M.M. Mulokozi), “Kinjeketile” (E. Hussein), “Mkwawa Mahinya” (F. Nkwera) na “Martin Kayamba” (G. Uhinga) ni miongoni mwa kazi zinazoingia katika kundi hili. Kupitia hizi mtu huweza kujua matukio mbalimbali yaliyojili.

Wakati uhuru ukipatikana, watu walikuwa na mategemeo makubwa sana kwamba maisha yangekuwa bora kwa kuwa wakoloni walikuwa wameondoka na wazawa kushika utawala. Katika kipindi hiki (1971-1981), maisha yalikuwa magumu kuliko ilivyotarajiwa. Tamthilia kama “Giza Limeingia” (E. Mbogo), “Mashetani” (E. Hussein), “Kilio cha Haki” (A. Mazrui), “Bwana Mkubwa” (J. Mbonde) na nyinginezo ziliandikwa kuakisi ubaya wa wakati huo.

Aidha, katika kipindi cha kushamiri kwa utandawazi (miaka ya 1980 mpaka sasa), kuna matukio mengi yaliyojitokeza. Hayo ni kama vile kuwapo kwa mwingiliano mkubwa wa kijamii, kushamiri kwa mfumo wa kibepari na mengineyo. Hayo yanaakisiwa na tamthiliya kama vile “Wakati Ukuta” (E. Hussein), “Kwenye Ukingo wa Thim” (E. Hussein), “Nguzo Mama” (P. Mhando), “Mkutano wa Pili wa Ndege” na nyinginezo.

Tamthilia hizi humwezesha mtu kujua matukio mbalimbali ya kihistoria akizisoma. Pamoja na kuandikwa kwa lugha ya kisanaa, matukio yanayojadiliwa ni bayana. Hivyo, msomaji huweza kujifunza au kujikumbusha mambo mengi yaliyotokeza katika jamii.