Fursa hiyo kwa wakulima wa pilipili kichaa

Muktasari:

Pilipili kichaa kutoka katika bara la Afrika maarufu kama ‘African Bird’s Eye Chilli’ ndizo zinazoonekana kupendelewa zaidi katika anga za kimataifa.

Pilipili kichaa ni zao lililoanza kushika kasi ya mauzo na kufanya vizuri sokoni miongoni mwa mazao ya biashara katika soko la dunia.

Pilipili kichaa kutoka katika bara la Afrika maarufu kama ‘African Bird’s Eye Chilli’ ndizo zinazoonekana kupendelewa zaidi katika anga za kimataifa.

Cha ajabu ni kwamba wakulima wengi wa Tanzania hawajachangamkia fursa hiyo adhimu ambayo kwa sasa imefunguka zaidi barani Ulaya.

Mkurugenzi wa kampuni yaVegrab Organic Farming inayojihusisha na kilimo cha mboga mboga na matunda, Gladness Nyangi anasema soko la zao hilo lipo vizuri na sasa nchi za Ujerumani na Uingereza zimeonyesha uhitaji.

“Tuliona kuna fursa katika kilimo hiki lakini kabla ya kuanza tulifanya utafiti kujua ni wapi hasa tutapata soko na kuona kama mkulima atapata faida,”

“Matokeo yalionyesha kuwa faida ipo na kwa kuanzia soko la Kenya lilikuwa wazi; tukawaomba waje kutusaidia kutuelekeza namna ya kulima pilipili hizo kisasa hilo likafanyika sasa mambo yanakwenda vizuri zaidi,”

“Tatizo ni kwamba bado Watanzania wengi hawajaamka na kuona faida ambayo inaweza kupatikana kupitia kilimo hiki, ila ninachoweza kuwaambia kuwa kina manufaa makubwa na biashara nzuri,”anasema Nyangi

Mtaalamu wa kilimo wa kampuni hiyo Josephat Lingodo anasema bei ya pilipili kichaa kwa sasa imefikia Sh 4500 kwa kilo moja huku katika shamba la ukubwa wa ekari moja zinaweza kuvunwa hadi kilo 150.

Kwa mujibu wa Lingoda, shamba la ekari moja linaweza kupandwa miche 10,000 ya pilipili aina hiyo.

Anasema tofauti na wanavyofikiria wengi kuwa huenda kuna masharti makubwa kujiunga na kampuni hiyo, Lingodo anasema mkulima akishanunua mbegu anakuwa tayari mwanachama.

Anasema. “Mkulima akishakuja kununua mbegu kwetu tunaanza kumpatia mafunzo ya namna sahihi ya kulima pilipili zinazohitajika katika soko la kimataifa na tunakuwa tunafualia maendeleo ya zao hilo hadi pale linapofungashwa,”

“Wakulima wachangamkie fursa hii, soko lipo tayari kazi inabaki kwetu tunahitaji pilipili za kutosha hakuna namna ya kuzipata zaidi ya wakulima kujikita kwenye zao hilo, tukaachana na masuala ya kulalamika,”

Matumizi ya zao hili

Ingawa wengi hutumia pilipili kama kiungo kwenye chakula, yapo matumizi mengine ya zao hilo ikiwa ni pamoja na kutumika kama mojawapo ya malighafi ya kutengenezea dawa za kuchua misuli na dawa nyingine za hospitali.

Pilipili hutumika pia kama malighafi katika kutengeneza bidhaa za viwandani.

Unga unga unaotokana na pilipili kichaa unatumika katika utengenezaji wa mabomu ya machozi.

Lingoda anasema zao hilo pia ni malighafi katika rangi za midomo maarufu kama lipstick.

Faida za pilipili kichaa kwa afya ya binadamu

Pilipili kichaa ni zao lenye wingi wa vitamini A na limebarikiwa pia kuwa na virutubisho vya vitamini B, vitamini E, vitamini C, Riboflavin, Potassium na Manganese.

Virutubisho hivyo vyote vina manufaa katika mwili wa mwanadamu na ndiyo sababu ulaji wa pilipili hizi unatajwa kuwa na faida kiafya.

Ndani ya mwili wa binadamu zinafanya kazi ya kusafisha damu, kutoa sumu , kusisimua mzunguko wa damu na kuweka sawa uwiano wa tindikali(acid)mwilini.

Pilipili kichaa pia husaidia kufungua kwa haraka na kwa ufanisi pua zilizoziba kwa mafua na kukufanya upumue kwa urahisi.

Aidha, mlaji wa pilipili kichaa anajiondolea uwezekano wa kupatwa na saratani ya utumbo.

Kilimo cha pilipili kichaa

Zao hili lina sifa kubwa ya kuvumilia hali yoyote ya hewa ikiwamo ukame, joto na mvua za kiasi kati ya mililimita 600 hadi 1200 kwa mwaka.

Pamoja na sifa hiyo, mkulima unapaswa kuwa makini ukame unapozidi sana unasababisha kuanguka kwa maua hivyo ni muhimu kunyunyuzia maji.

Pilipili huhitaji joto la kiasi cha nyuzi 20 hadi 30 na udongo tifutifu wenye kiwango cha tindikali yaani Ph 6.0 hadi 6.5.

Zao hili linapaswa kuoteshwa kwanza kwenye vitalu kabla ya kuipeleka shambani. Tengeneza vitalu vya upana wa mita moja.

Tumia mbolea ya kinyesi cha ng’ombe au mboji

Weka mistari ya mbegu upana wa sentimita 10 kwa kila mstari hadi mstari.

Baada ya kuweka mbegu weka udongo kiasi na weka nyasi kutunza unyevu nyevu na mwagilia maji mara kwa mara.

Mbegu zikiota toa nyasi na nyunyizia dawa ya kuua wadudu, iache iendelee kukua hadi kufikia unene wa sentimita 2-3 kwa urefu sentimita 8-10 ndipo uipeleke shambani.

Ndani ya miezi mitatu zikiwa shambani pilipili zitakuwa zimebadilika rangi na kuwa nyekundu hapo zinakuwa tayari kwa ajili ya kuvunwa na huvunwa mfululizo kwa miezi mitatu hadi minne.

Inashauriwa uvunaji huu ufanyike kila baada ya wiki mbili na haitakiwi kuvunwa pamoja na vikonyo vyake.

Changamoto

Lingodo anasema pamoja na mafanikio makubwa yanayotokana na kilimo hicho, uwepo wa wadudu waharibifu ni kikwazo kikubwa kwao.

Anasema kuna wadudu wadogo wadogo ambao ni nadra kuonekana kwa macho, wao hufanya kazi ya kuharibu maua ambayo yanategemewa kuzalisha pilipili.

Utitiri ni changamoto nyingine pamoja na uwepo wa wadudu wanaoshambulia mizizi.

Kukabiliana na changamoto hizo mkulima anashauriwa kupalilia mapema kukabiliana na na maficho ya wadudu ambao wanaonekana kwa macho.

Mkulima anashauriwa kabla ya kujitosa kwenye kilimo hiki awe na uhakika wa soko, hivyo ni muhimu kuingia mkataba wa makubaliano ili mazao yakitoka shambani moja kwa moja yaende sokoni.