Gesi asilia inavyofungua njia kwa Watanzania kuagana na umaskini

Mitambo ya umeme

Muktasari:

Huo ni mradi mkubwa wa umeme ambao haujawahi kuwepo nchini tangu tupate uhuru, hivyo unalihakikihsia Taifa kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa haina chanzo cha uhakika cha nishati ya umeme, jambo ambalo limekuwa likiirudisha nchi nyuma kimaendeleo.

Miongoni mwa athari za kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya umeme ni kuongeza gharama za uzalishaji wa bidhaa, kupanda kwa gharama za maisha, kudumaa kwa viwanda vidogo na vya kati, kuathirika kwa wajasiriamali wanaouza vinywaji baridi na kuongezeka kwa gharama za uwekezaji.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linasema tatizo hilo linatarajia kuwa ni historia hapa nchini baada ya kukamilisha mkakati wa ujenzi huo wa mradi wa umeme.

Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asilia katika maeneo ya Madimba-Mtwara Vijijini, Songo Songo, Wilayani Kilwa pamoja bomba la kusafirishia gesi asilia hadi Dar es salaam kupitia Somanga Fungu.

Hali hiyo sasa inafungua mlango kwa Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kwa kuhamasisha ukuaji wa viwanda, kuongeza nafasi za ajira, kupunguza umaskini na kuongeza pato la Taifa.

Mkurungenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio anasema tayari kazi ya kufungulia valvu kuruhusu gesi asilia kutoka Mtwara kuiingiza katika mitambo ya Tanesco kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa gesi katika kituo kipya cha Kinyerezi I na Ubungo II imekamilika.

“Kukamilika wa mradi huu wa gesi kutaokoa dola za kimarekani 1 bilioni zilizokuwa zikitumika katika ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya Tanesco, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2011,” anasema Dk Mataragio.

Mradi huu unaunganisha maeneo yanayozalisha gesi asilia ambayo ni Mnazi Bay - Mtwara, Songo Songo, Kiliwani, Mkuranga, Ntorya na gesi iliyogunduliwa katika eneo la bahari ya kina kirefu cha baharí ya Hindi. Dk Mataragio anasema tayari TPDC imekamilisha kazi ya kuingiza gesi kutoka mitambo ya kuchakata gesi ya Mtwara hadi kituo kipya cha kupokea gesi cha Kinyerezi I, ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme megawati 150.

 

Gharama za mradi kwa ujumla:

Dk Mataragio anasema  gharama za ujenzi wa mradi huu wa gesi ni Dola za Marekani 1.225 bilioni  ambazo asilimia 95 ni mkopo na asilimia 5 ni mchango wa Serikali.      

Anasema mradi huo umetekelezwa kwa kutumia fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya China.

“Dola 151.7 milioni za Marekani zimetumika kwa ajili ya mtambo wa kusafisha gesi asilia wa Songo Songo, Dola 197.9 milioni za Marekani kwa mtambo wa Mnazi Bay na Dola  875.7 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia,” anasema Dk Mataragio.

Hasara ya umeme wa mafuta

Dk Mataragio anasema kuwa mitambo iliyokuwa inafua umeme kwa kutumia mafuta badala ya gesi asilia imekuwa ikiisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2011.

“Umeme huu ulikuwa ghali na ulikuwa ukigharimu Serikali kati ya Dola senti 35 hadi 42 kwa uniti, wakati ule unaozalishwa kutokana na gesi asilia ulikuwa kati ya senti 6 hadi 8. Hivyo kuna unafuu mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ikilinganishwa na mafuta.”

 

Serikali inasemaje?

Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene anasema kukamilika kwa mradi huo mkubwa umeme ni mafanikio kwa taifa na dunia kwa sababu sasa nchi itauza umeme wake nje ya nchi baada ya kujitosheleza.

“Hili ni jambo kubwa na la kihistoria kwa nchi yetu kuanza kutumia umeme wa gesi badala ya mafuta. Tulipaswa kusimama hata kwa dakika tatu kusherehekea mafanikio haya kupitia mradi mkubwa wa Serikali uliogharimu Dola 1.22 bilioni za Marekani, sasa wale ndugu zangu wanaosema Rais Kikwete anaondoka madarakani anawaachaje! Mimi nasema anawaachia umeme huu wa gesi,” anafafanua Simbachawene .

Anasema huo ni mradi mkubwa wa umeme ambao haujawahi kutokea tangu Tanzania ipate uhuru hivyo unaihakikishia nchi kuingia katika uchumi wa kati ifikapo kipindi cha mwaka 2020/2025.

“Mradi wa kufua umeme kwa Gesi umekamilika nchini na ndani ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu mitambo yote yenye uwezo wa kuzalisha megawati 335 itakuwa imewashwa na hivyo kuondoa tatizo la umeme hapa nchini,” anasema Simbachawene

Waziri huyo anasema Septemba 17 pekee walipitisha gesi katika bomba lenye ujazo wa futi 20 milioni na kwamba bomba hilo lina uwezo wa kupitisha futi za ujazo 784milioni na kwamba hadi Desemba mwaka huu bomba hilo litakuwa limepitisha futi 130 milioni za Gesi, sawa na wastani wa ujazo wa futi 20 milioni kila siku.

 

Matarajio ya mradi

Simbachawene anasema baada ya kukamilishwa kwa uzalishaji wa megawati 335, mdhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) atafanya tathmini ya gharama kuona kama kutakuwa na unafuu wa bei za umeme nchini.

Mbali na uzalishaji wa mitambo hiyo, pia serikali itapeleka mtambo mmoja wa kuzalisha umeme unaotembea kwa kutumia magurudumu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 katika mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kutatua tatizo la umeme katika mikoa ya Kusini.

“Malengo yetu ya baadaye ni kuzalisha tena megawati 600 mkoani Mtwara na kusambaza mabomba ya gesi katika mikoa yote nchini na tayari mipango ya gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani imeshaandaliwa ili kuweza kuunganisha wateja wa majumbani na kuweka gesi katika vifungashio kwa ajili ya kuuza,” anafafanua.

Vilevile wana mpango wa kuuza gesi hiyo nje ya nchi katika nchi ambazo zinakabiliwa na uhaba wa umeme.

 

TANESCO wanasemaje?

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchism Mramba, anasema kwa sasa Watanzania wategemee umeme wa uhakika kutokana na mtambo wa Kinyerezi (I), Ubungo (II) kupokea gesi kutoka Mtwara.

Anasema mtambo wa Kinyerezi (I) ni mpya na utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme megawati 150 kwa kutumia gesi huku mtambo wa Ubungo ( II) utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 200 na mtambo wa Symbion ambao ulisitisha huduma za kuzalisha umeme kwa miezi mitano, sasa utakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawatt 112 kwa kutumia gesi.

“Kuunganishwa kwa mitambo yetu kutoka mtambo mpya wa Kinyerezi (I) matatizo ya umeme yataisha iwe Bwawa la Mtera au Kidatu limejaa maji au halijajaa, umeme utakuwapo wa uhakika,” anasema Mramba.

Mramba anasema mtambo wa Ubungo I utaendelea kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya Songosongo na kwamba Ubungo II inatumia gesi ya Mtwara kwa kuwa inatosha kuendesha mitambo hiyo.

Profesa Benedict Mongula kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema gesi itasaidia kukuza uchumi, kupunguza gharama za uzalishaji kwa wafanyabiashara, hivyo kuna haja ya Tanesco kuangalia namna ya kupunguza bei ya umeme kwa watumiaji ili hata wale wenye kipato cha chini waweze kunufaika na umeme huo..

“Kuanza kutumika gesi asilia nchini kutaongeza shughuli za kiuchumi kwa watu wa kawaida kupata ajira mpya, kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme unaotumia gesi kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kuwa na vyanzo vingi mbadala” anafafanua Profesa Mongula

Kuanzia mwaka 2005 hadi Juni mwaka huu, jumla ya visima 45 vimechorongwa sawa na asilimia 56 ya visima vyote 90 vilivyochorongwa nchini hadi sasa na kati ya hivyo, visima 35 viligundulika kuwa na gesi.

“Idadi hii ni kubwa kwa kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya utafutaji wa mafuta na gesi hapa nchini kwani wastani wa uchimbaji visima kati ya Mwaka 1952 ulikuwa ni kisima kimoja kwa mwaka lakini wastani huo kwa kipindi cha Mwaka 2005 na Mwaka 2014 ulifikia visima 5 kwa mwaka,” anasema.

“Kupitia kukamilika kwa miradi hii nchi itaondokana na utegemezi wa kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ambapo Tanesco ilikuwa ikipata hasara kila wakati na pia tutaanza uzalishaji wa umeme kwenye mashine zilizopo Ubungo zenye uwezo wa megawati 200 ambazo zilikuwa hazipati gesi ya kutosha” anasema

Vilevile kuongezeka kwa shughuli za utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi nchini na utunzaji wa mazingira kwa kutumia gesi ukilinganishwa na aina nyingine za nishati.

Tanzania inaamini baada ya nchi kujitosheleza kwa umeme, itatafuta masoko ya nishati hiyo katika nchi jirani, kama vile Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Congo (DRC).