HEKAYA YA MLEVI : ‘Buta nikubutue’ si suluhu

Muktasari:

  • Mpira ungeweza kuanzishwa Januari pale Keko ukaenda kuisha Desemba huko Kitonga kwa kutumbukia korongoni. Najua mnashangaa. Lakini ni lazima muelewe kuwa hakukuwa na timu; Wewe uliye Msamvu unaupokea kutoka Chalinze, ambako waliupokea kutoka Ubungo. Tuache hayo.

Kabla sanaa na michezo kuwa kazi ilikuwapo kwa ajili ya burudani tu. Ilifanywa wakati wa mapumziko ya kazi au baada ya kazi. Hakukuwa na viwanja maalumu, hivyo mchezo uliweza kuanzishwa kondeni, shambani kiwandani muda ambao watu wanapumzika. Wanaporudi kazini waliuacha mchezo ukiendelezwa na watu wengine.

Mpira ungeweza kuanzishwa Januari pale Keko ukaenda kuisha Desemba huko Kitonga kwa kutumbukia korongoni. Najua mnashangaa. Lakini ni lazima muelewe kuwa hakukuwa na timu; Wewe uliye Msamvu unaupokea kutoka Chalinze, ambako waliupokea kutoka Ubungo. Tuache hayo.

Ukitaka kuwa mshindi usiwaze kupaa, ila fuata nyayo za washindi. Yeyote aweza kuwa nyota kwenye jambo kama ataiga mafanikio ya waliomtangulia. Muhammad Ali alimfuata Sugar Ray na alifanikiwa kumkaribia kama si kumzidi. Michael Jackson alimkopi Elvis Presley kuanzia kuimba hadi kujikoboa sura. Lakini alifanikisha malengo yake.

Sijawahi kusikia kiongozi yeyote anayefuata nyayo za Adolf Hitler. Hata yeye sijui alifuata nyayo za nani, kwa maana hata kama angezaliwa upya, asingekubali kuzifuata nyayo zake mwenyewe. Huyu jamaa alikuwa hafai hata kwa kulumagia. Hafai hata senti.

Yeyote anayetaka kufanikiwa kwenye uongozi huyaiga mafanikio ya viongozi walioweka historia za uadilifu na uongozi uliotukuka. Tangu kuumbwa kwa dunia kulikuwa na viongozi; lakini walitofautiana sana katika njia zao. Vitabu vya dini vinatusimulia nyakati za Adam, Nuhu na Musa kama viongozi waadilifu. Lakini pia Farao (Firauni) na wenzake waliokuwa viongozi wabadhirifu. Vitabu hivi vinahitimisha ukweli juu ya unyenyekevu kushinda kiburi.

Kutoka wakati huo hadi sasa hakuna yeyote anayependa kuongozwa kifirauni. Viongozi wa dini na wa Serikali kwa pamoja wanasisitiza maridhiano. Ili kutia mkazo, wanasheria pia wameshirikishwa kuyahariri na kuyaweka kwenye kumbukumbu kama herufi zilizochongwa juu ya mawe, si kuandikwa juu ya mchanga.

Kiongozi apende au asipende huwajibika na maandiko hayo. Hulazimika kutoa haki na fursa sawa kwa wote bila kujali tofauti zao. Mwalimu Nyerere alisema akipita mtaani na kukuta ombaomba, majambazi na makahaba, alijua kwamba ni wa kwake hao. Kazi yake ni kubeba shida hizo pamoja nao na kuuelekea unafuu.

Nchi ni sawa na mwili wa binadamu. Ina mchanganyiko wa ngurumbili wa kila aina. Hivi karibuni mitandao ya kijamii ilionyesha picha za marais wa Marekani wakati wakiapishwa, na wakati wakistaafu. Wote waliingia wakiwa vijana watanashati, lakini miaka minane ya uongozi iliwatoa wakiwa wamechoka hasa! Uongozi ni mgumu jamani.

Endapo ungeweza kuona timbwili linalofanywa kila siku mwilini mwako ungekufa kwa mshtuko. Kuna zaidi ya debe la minyoo iliyo bize kwelikweli usiku na mchana. Kama ukikasirika na kuua minyoo wote, bila shaka nawe ungekufa saa hiyo. Kwani kuna minyoo yenye kazi ya kumeng’enya chakula mwilini ili uendelee kuishi.

Mgonjwa hupata tiba. Lakini kuna wakati tiba zote zinakataa. Hapo kwa kujijali mgonjwa hutafuta tiba mbadala. Atakwenda kwa matabibu wa asilia, wanasaikolojia, wazee wa mila ama kwenye maombezi.

Anaweza kuwa ameshakunywa dawa zenye ujazo wa kontena mbili bila nafuu. Lakini siku moja akakutana na mzee anayetibu kwa ushauri tu, na akapona.

Kwa mfano, mmoja baada ya kuhojiwa aligundulika kuwa anafanya kazi zinazotumia akili nyingi kiasi cha kumchosha akili.

Sasa ili kesho aweze kuendelea na kazi, alikunywa pombe nyingi kwa lengo la kupunguza misongo akilini mwake. Siku alipoumwa alikwenda kutibiwa na tiba haikufanya kazi. Alirudia na kurudia dozi bila nafuu. Madaktari wakasema ana ugonjwa mpya, waombezi wakasema kapandwa na pepo na masangoma wakadai amerogwa…

Kwa bahati alikutana na daktari anayetibu kwa ushauri. Akaisikiliza hadithi yake kwa makini sana, kisha akamwambia: “Dawa yako ni maji. Kunywa maji glasi moja kila baada ya dakika tano.” Jamaa akang’aka: “Mi nshakunywa hadi mkojo, maji kitu gani!” Mtaalamu akabaki kimya akimtazama.

Kwa vile mgonjwa hakatai dawa, alikunywa maji kwa fujo sana na maradhi yakaisha. Wenye akili tunajua kuwa mapombe makali aliyotumia yalimtia sumu nyingi mwilini, alipoumwa na kumeza dawa zilikutana na sumu ile navyo kushindwa kufanya kazi au kugeuzwa sumu. Usione mganga akikuchanganyia dawa, pengine ni maji tu hayo.

Dawa ya aina hii ndiyo niliyotaka kuwashauri Wizara ya Mambo ya Ndani.

Tumeambiwa kuwa polisi hawapati ushirikiano kutoka kwa raia juu ya sakata linaloendelea mkoani Pwani. Kabla ya mganga kutoa dozi ni lazima atazame historia ya mgonjwa, hivyo uchunguzi wa kadhia hii ungeanza na “kwa nini hatupati ushirikiano wa raia?”

Bila shaka hakuna askari Polisi anayefurahia kuua. Pia, hakuna raia hata mmoja anayeshangilia kuuawa kwa mlinzi wake. Hivyo, basi ni lazima kuna pazia linalotakiwa kufunuliwa ili pande zote zionane. Ushauri wangu mkubwa ni viongozi kwenda kukaa na wazee, akinamama na kisha vijana wa kule.

Hiyo ndiyo gharama ya uongozi, lakini ikumbukwe kuwa ukivaa shati la masikini utajua sehemu ya shida zake. Na hii ndiyo moja ya silaha kubwa iliyotumiwa na muasisi wa Tanzania katika kudumisha mshikamano.

Kwa mtindo huu wa ‘Buta Nikubutue’ nyasi zote zitaungua.