HISTORIA ILIYOTUKUKA: Afrika iligomea Kombe la Dunia 1966

Muktasari:

Ni miaka 50 imepita tangu mashindano ya Kombe la Dunia yasusiwe na bara zima la Afrika.

Ni miaka 50 imepita tangu mashindano ya Kombe la Dunia yasusiwe na bara zima la Afrika.

Unajua ni kwa nini Afrika, bara ambalo wakati ule lilikuwa na nchi chache zilizokuwa huru ilifikia uamuzi huo mgumu?

Hata hivyo, fainali za mwaka  huo zilizoandaliwa Uingereza, ushindi wa nchi mwenyeji, England ulikuwa wenye utata. Pia, ni fainali  zilizoshuhudia  bao la ajabu la Mreno mwenye asili ya Afrika (Msumbiji), Eusebio alilolifunga dhidi ya Korea Kaskazini.

BBC Focus ilimwangalia mtu aliyeandika historia ya kususwa kwa mashindano hayo yaliyoleta mabadiliko ya kufanya soka kuwa mchezo wa ushindani zaidi duniani.

Raia huyo wa Ghana, Osei Kofi alishawahi kujumuishwa na mkongwe George Best kama mmoja wa watu muhimu Afrika na Gordon Banks, mshindi wa Kombe la Dunia 1966.

Banks, ambaye alipewa heshima ya kutengenezewa sanamu ya Ireland Kaskazini kama mmoja wa nyota wakubwa wa soka, hapo ndipo kulipoibuka kwa maneno.

Lakini, kuna mambo ambayo huenda hujawahi kuyafahamu kuhusu Kofi, aliyemfunga Banks mabao manne wakati walipokutana katika michezo miwili ya kirafiki ya klabu zao.

Hili linaweza kuwa kubwa kwa sababu mchezaji aliyejulikana kwa jina la utani kama ‘One Man Symphony Orchestra’, ama ‘Wizard Dribbler’ hakuwa na nafasi ya kucheza katika mashindano ya Kombe la Dunia.

Alinyimwa nafasi hiyo wakati Bara la Afrika lilipofanya mgomo wa ajabu katika fainali za mashindano hayo za  mwaka 1966.

Wakati huo, kikosi cha Ghana maarufu, Black Stars kilitwaa mfululizo ubingwa wa Mataifa ya Afrika kati ya mwaka 1963 na 1965.

“Tulikuwa na Black Stars iliyokamilika kwa wakati huo,” Kofi, ambaye sasa ni kiongozi wa kanisa, aliuambia mtandao wa BBC katika mji mkuu wa Ghana, Accra. “Tulikuwa na watu, ambao walikuwa na nguvu na uthubutu.

“Ndiyo sababu tulifanikiwa kuingia katika mashindano ya Kombe la Dunia wakati wowote.”

Lakini, wakiwa juu katika kiwango chao, Black Stars walijikuta wakisukumwa chini katika ‘shimo lenye kiza’.

Januari 1964, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliamua kuanza kwa mfumo wa kutumika timu za mataifa 16 kucheza fainali za Kombe la Dunia, mgawanyo ulikuwa kama ifuatavyo;  Ulaya ilipewa nafasi ya kuingiza timu 10, ikiwamo wenyeji England, nne kutoka mataifa ya Amerika Kuisni na moja kutoka Amerika ya Kati na Karibiani.

Hilo lilifanya nafasi moja kubaki ikipiganiwa na mabara matatu ya Afrika, Asia na Oceania.

Ndani ya mwezi mmoja, aliyekuwa mkurugenzi wa michezo wa Ghana, Ohene Djan, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa, aliamua kupaza sauti kupiga hatua hiyo.

“Nawasilisha pingamizi langu zito kwa uchaguzi usio na usawa wa mashindano ya Kombe la Dunia kwa mabara ya Afrika, Asia na Oceania, hili lisimame,” alilalamika katika ujumbe wake wa telegram alioutuma kwenda Fifa.

“Mataifa ya Afro-Asian yanapitia katika kipengele kigumu cha maumivu kutokana na mlolongo mrefu wa kufuzu kwa taifa moja na hii ni mbaya inayotakiwa kupigiwa kelele, Afrika kuwa na mwakilishi mmoja, hili baya.”

 

Nguvu ya kisiasa

Malalamiko ya Djan yalichagizwa na Kwame Nkrumah, Rais wa Ghana  aliyechaguliwa mwaka 1957, likiwa taifa la kwanza la ukanda wa Sahara kupata uhuru wakati huo.

Nkrumah alitaka kutumia soka kwa ajili ya kuiunganisha Afrika na alimwambia mshirika wake, Djan kufanya lolote litakalofaa kuliweka soka la Afrika katika uso wa dunia.

Djan, ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa pia mjumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF),  aliyejulikana kama mmoja kati ya watu wawili wa shirikisho hilo wenye nguvu katika kupigani haki ya Kombe la Dunia, mwingine alikuwa Tessema Yidnekatchew, raia wa Ethiopia.

Wawili hao walianzisha mjadala wa ushawishi juu ya uamuzi wa Fifa, ambao Tessema aliuita, ‘harakati za kiuchumi, kisiasa na kijiografia’.

Kwanza, walilalamika kwamba kiwango cha soka la Afrika kilishapanda kwa miaka kadhaa bila mataifa mengine kuliangalia hilo kama sababu ya msingi.

Baadaye waliibuka na kipengele cha gharama za michezo ya timu za Afrika kufuzu kwa Kombe la Dunia ni kubwa ukilinganisha na wenzao wa Asia na Oceania ambayo ni mataifa makubwa kiuchumi.

Pia, kukaingia suala la siasa, wakati huo hali ilikuwa ngumu kwa CAF kufanya kazi na Fifa kutokana na hali ilivyokuwa nchini Afrika Kusini kulikokuwa na vita ya ubaguzi wa rangi.

Baada ya kuanzishwa  mwaka 1957, CAF kilikuwa chama cha kwanza kilichokuwa na nguvu ya kukusanya watu na kupigania haki zao kabla ya baadaye kuzaliwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU sasa AU) miaka sita baadaye.

 

CAF katika ukombizi

Ikiwa na makao yake makuu jijini Cairo, Misri, CAF kilikuwa chama cha kwanza cha michezo kushughulika na hali ya amani ya Afrika Kusini na kusaidia kutungwa kwa sheria ya ubaguzi wa rangi 1960.

“Baada ya mataifa ya Afrika mengi kupata uhuru, yalijiunga na Umoja wa Mataifa (UN) na baadaye kuingia CAF, hakukuwa na chama kingine,” alinukuliwa Fikrou Kidane, mtu aliyefanya kazi kwa muda mrefu na Tessema, ambaye alifariki 1987.

Mwanahistoria wa soka, Alan Tomlinson anasema: “Ukianzia mwanzo wa hili, utagundua kuwa huu ulikuwa mwanzo wa siasa za utamaduni wakati wa ukoloni.”

Lakini, baada ya vurugu nyingi, katika fainali za 1966, Fifa waliamua kuipanga Afrika Kusini katika kundi lililokuwa na timu za  Asia wakisingizia kutotaka timu za Afrika kukutana zenyewe katika hatua ya mwisho ya kufuzu.

Wakiwa tayari walishawahi kuifungia Afrika Kusini kwa mwaka mmoja na CAF, Fifa waliipa nafasi  mwaka 1963 ili kupanga kuwakutanisha timu za watu weupe katika fainali za 1966 na moja ya watu weusi icheze fainali za 1970.

“Hilo lilikuwa suala lisilowezekana na halikukubalika, lilikuwa gumu katika vichwa vya watu,” alisema Kidane,  aliyehudhuria mkutano mkuu wa Fifa wa 1960 kama mwakilishi wa Ethiopia.

Julai 1964, CAF  ialitishia kususia mashindano ya Kombe la Dunia 1966, vinginevyo Afrika ipewe nafasi ya peke yake.

Wakati ikiwa ni Misri pekee iliyowahi kucheza fainali za Kombe la Dunia hadi wakati huo, ambayo ilikuwa mwaka 1934, huu haukuwa mjadala mdogo.

 

Fifa walegea

Miaka miwili baada ya fainali hizo zilizokuwa na figisu nyingi kupita, ikatambulishwa rasmi kuwa Afrika itakuwa na nafasi yake katika Kombe la Dunia. Asia nayo ikapata moja.

“Nadhani ilikuwa moja ya hatua muhimu ya maendeleo ya uhusiano mwema,” anasema mwanahistoria wa soka, Tomlinson.

“Kama Fifa wangeendelea kuwa na mtazamo wa kizamani, nadhani soka duniani kote ingekuwa katika mtazamo tofauti kwa sasa.”

Leo, Afrika ina nafasi tano za ushiriki wa Kombe la Dunia yanayochukua mataifa 32 katika fainali zake, wakati Afrika Kusini likiwa taifa la kwanza kuwa mwenyeji wa mashindano haya, 2010.

Rais wa sasa wa Fifa, Gianni Infantino anafikiria kuongeza idadi ya washiriki kufikia 40 katika miaka michache ijayo, huenda Afrika na Asia wakapata nafasi nyingi zaidi. Ni jambo la kusubiri na kuona!