HOJA BINAFSI-Maendeleo kindegendege

Muktasari:

  • Hali hii ya kuona kila kitu ni mashambulizi yanayohitaji difensi kali imetoka wapi? Duh! Maana yangu ilikuwa tofauti kabisa. Ukipanda ndege na kuruka juu juu juu zaidi, unajifunza pia shida ya maendeleo.

Ohooo! Acheni ushambenga nyie. Kwani nikitumia mfano wa ndege, lazima niongelee ndege yetu mpya bombailiyopokelewa kishujaa juzi? Na papohapo ni lazima watu waibuke kama kumbikumbi na kuanza kuteteatetea bila hata kujua mtu anamaanisha nini.

Hali hii ya kuona kila kitu ni mashambulizi yanayohitaji difensi kali imetoka wapi? Duh! Maana yangu ilikuwa tofauti kabisa. Ukipanda ndege na kuruka juu juu juu zaidi, unajifunza pia shida ya maendeleo.

Tuseme uko juu kati ya Dar es Salaam na Mtwara. Ukiangalia chini, upande mmoja unaona bahari lakini huoni meli, sembuse ngalawa, sembuse wavuvi. Upande mwingine unaona msitu mnene, lakini vijiji mara nyingi hata havionekani, sembuse watu, sembuse mizigo wanayoibeba, sembuse kisima kilichokauka. Utaona nchi yetu ni nchi inayopendeza kwelikweli. Na inapendeza si uongo, lakini hautaona jitihada za watu ndani ya mazingira yale, iwe katika kilimo, au tuviwanda, au shule n.k. Hauwezi kuona kwa sababu uko juu yao kwa mbali sana. Ndiyo maana ikiwa anayepanga mipango ya maendeleo yuko kwenye ndege atashindwa kupanga vizuri maana haoni, hapati picha halisi.

Lakini, walio wengi bado wako juu kwa mbali sana bila hata kupanda ndege. Tuseme, kwa mfano, umepanda 4x4 yako na kwenda kuhamasisha maendeleo huko kijijini, maendeleo kwa tafsiri yako. Unatimua vumbi kushoto na kulia hadi kufika huko (na kawaida tunafika kwenye vile vijiji ambavyo vinafikika kwa urahisi, vile vilivyoko karibu na mji mkuu wa wilaya. Hebu angalia miradi ya maendeleo hujikita wapi). Kwa vyovyote, utaongea kwanza na viongozi wa eneo lile, kisha labda na wazee mashuhuri na wachache walioalikwa na viongozi, yaani wale walio karibu nao. Kwa wale wote wengine, ni sawa na kwamba umepanda ndege kufika pale. Hata huwaoni, kama huwaoni, utawasikiliza saa ngapi.

Hebu nitoe mfano. Shirika moja lilipewa kazi ya kutathmini hali ya maisha katika wilaya fulani. Katika kufanya kazi hiyo, ilibidi kufika kwenye vile vijiji visivyofikika, hakuna barabara na mchanga ulivyo hata bodaboda shida, kwa hiyo lililobaki ni kutembea kwa saa mbili. Kufika huko, wakakuta zahanati imejengwa lakini haifanyi kazi. Ilikuwa imebaki pango la popo tu na nyufa zilikuwa zinashindana, ufa upi utaweza kupanuka haraka kuliko mwenzie. Katika kuongea na viongozi wa pale, wakasema walipewa pesa kibao na shirika fulani ili kujenga zahanati ile kwa hiyo walijenga … kubali yaishe bado ni mtindo wa kisasa mbele ya mitindo ya kisiasa elekezi lakini hawakuelewa kwa nini wajenge.

‘Hebu angalia. Daktari au muuguzi gani watakubali kuja kufanya kazi hapa? Kutembea saa mbili kwenda barabarani kisha utafute daladala ya kwenda wilayani. Thubutuuuu! Si bora tungetumia zile pesa kutengeneza barabara kwanza. Lakini hatukuulizwa.’

Si ndiyo. Waliopanga kwamba kijiji kile kiwe na zahanati walikuwa ni sawa na abiria wa ndege. Wako mbali mno kwa hiyo hawaoni.

Haya, katika kuendelea na kazi hii, shirika kama kawaida yake lilihakikisha kwamba linaongea na makundi mbalimbali, wanaume, wanawake, vijana wa kiume na wale wa kike, tena kwa kuchagua mhusika kutoka kila nyumba ya tano, badala ya kupangiwa wahusika wapendwa wa viongozi.

Kwa kweli walipata mengi na jambo ambalo lilijitokeza kabisa ni kwamba masuala ya wazee yalikuwa tofauti sana na yale ya vijana. Masuala ya wanaume hayakufanana na yale ya wanawake, na yale ya wenye ulemavu n.k, nayo yalikuwa tofauti.

Sasa kwa kuwa ule ulikuwa ni utafiti, shirika halikuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko lenyewe lakini, kama kawaida yake, watafiti wake walihakikisha kwamba wanatoa mrejesho kwa viongozi na wawakilishi wa vikundi vyote ili kujadili kwa pamoja nini kifanyike kwenye masuala ya makundi mbalimbali.

Wakati wanataka kuanzisha mrejesho huu, wakashtuka kwamba kundi kubwa la vijana limefika na kutaka kuingia kwenye mkutano kwa nguvu. Watafiti walishangaa kuona kwamba viongozi, badala ya kudhibiti ile hali, walikuwa wanaanza kutetemeka. Hivyo mtafiti mmoja alienda kuongea na vijana wale.

‘Sisi Bwana lazima tuingie kwenye mkutano. Wale wazee watawapotosha tu.’

‘Lakini si wawakilishi wa vijana wapo pia.’

‘Wawakilishi gani? Wanajiwakilisha tu. Kwanza yule anayejiita mwenyekiti wa vijana amepachikwa tu kwa kuwa ni mtoto wa dada yake mwenyekiti wa kijiji. Kazi yao kuunga mkono maneno ya wazee. Lazima tuingie.’

‘Ngoja, ngoja, ngoja. Kwani hamwamini kwamba tunaweza kuwasilisha maoni yenu.’

‘Hatuna shida na nyinyi. Nyinyi ni watu wa kwanza kujua kuongea na sisi. Wakija watu wengine wanaishia kuongea na viongozi wa kijiji na kutokomea. Ndiyo maana masuala yetu hayatiliwi maanani. Lakini, nyinyi kweli mlitutafuta na kuongea nasi.’

Basi baada ya mjadala mrefu, na vijana kuonyeshwa kwamba hata wao wanao uwezo wa kugombea uongozi, walikubali kuondoka. Lakini, bado funzo lilikuwepo. Iwapo wanaotembelea kijiji wanaishia kuongea na wazee tu, tena wazee wenye uwezo zaidi maana ndio wanaochaguliwa, si ni sawa na kupita juu kwa juu kwenye ndege?

Hali halisi ya wananchi na mitazamo na mahitaji mbalimbali hayatasikilizwa na kuzingatiwa. Labda kwenye jamii ile, wawepo viongozi ambao lengo lao kuu ni kuwashirikisha na kuwasikiliza na kuwazingatia watu wa makundi yote lakini hali hii hutokea mara chache. Popote uendapo vijana hulalamika kwamba hawashirikishwi hata kama wanataka.

Hebu nitoe mfano wa mwisho. Shirika lingine lilitaka kutumia mbinu shirikishi kweli katika kujua mahitaji na vipaumbele halisi kabla ya kufadhili kipaumbele kikuu cha kila jamii. Sasa katika kijiji fulani, wanaume walitaka kuweka kipaumbele kwa shule maana majengo hayakuwa ya kudumu lakini wanawake waling’ang’ania uchimbaji wa kisima kwa sababu, kila mwaka, wanawake kadhaa wanajeruhiwa na hata kuliwa na mamba wakitafuta maji. Sasa hapa utapanga kipaumbele gani?

Kwa kuwa kikao kilitawaliwa na wanaume wazee, kilitoa kipaumbele kwa shule, fedha zikatolewa lakini shirika lilipoenda baada ya miezi sita, bado kazi iliyofanyika ilikuwa ndogo tu hivyo ilibidi kufanya kikao tena kutathmini vile vipaumbele.

Kumbe wazee walitaka pesa za shule kwa sababu walikuwa wanaghasiwa na halmashauri lazima waboreshe shule lakini haikuwa kipaumbele kweli. Hivyo kikao kilipofanyika kilichoruhusu kila kikundi kushiriki sawasawa, ilionekana wazi kabisa kwamba kipaumbele kikuu ni kisima ili wanawake wasiendelee kuliwa au kupewa ulemavu wa maisha. Pesa zilihamishwa kwenye kisima na baada ya miezi sita, kikawa tayari.

Kwa hiyo tunaona nini hapa? Kwanza watu, serikali, wafadhili na mafedhuli, ‘maAZAKI’ na wengine wakitaka kuleta maendeleo kindegendege, daima tutaendelea kufanya makosa maana hatuoni. Hatuoni tukiwa juu, hatuoni tukiwa hata pale tukiongea na wachache wenye uwezo. Ni lazima kwenda na kusikiliza makundi yote, na kutoa nafasi kwa makundi yote kabla ya kupanga masuala gani yapewe kipaumbele. Najua hii ni sera ya taifa lakini hutekelezwa au hutelekezwa hivyo.

Pili, hata kwenye ngazi ya jamii, watu wana maoni na vipaumbele tofauti na si lazima maoni bora hutokana na mtendaji wa kata. Maendeleo ya jamii ile yatategemea kusikiliza na kuzingatia utofauti wote huo.

Mwenye kutoa wazo tofauti si mpinga maendeleo bali ni mwenye dukuduku inayoendana na hali yake halisi. Kitaifa ndiyo zaidi ya hapa mara dufu. Tukipanda ndege yetu tena, tunaona msitu tu. Msitu ni msitu lakini kumbe kuna miti ya kila aina, na wanyama, na wadudu. Wote wanachangia ustawi wa msitu ule na ukiwaondoa wengine, msitu unaweza kuharibika moja kwa moja. Ubora wa msitu hutokana na utofauti uliopo kila mmoja akitoa mchango wake.