Hamahama hii ya wanasiasa ni balaa kwa demokrasia

Muktasari:

  • Wanachama, viongozi na makada wa kuaminika wamekuwa wakipishana kutoka chama kimoja kwenda kingine huku ikishuhudiwa hata wale waliodhaniwa ni makada kindakindaki wa chama fulani au kingine, nao ‘wakiruka ukuta’ na kuhamia ng’ambo ya pili.

Ingawa wanasiasa kuhama vyama imekuwapo na hutokea duniani kote tangu miaka ya zamani, kasi ya hamahama katika nchi yetu ya Tanzania katika majuma na mawili ya karibuni inatisha.

Wanachama, viongozi na makada wa kuaminika wamekuwa wakipishana kutoka chama kimoja kwenda kingine huku ikishuhudiwa hata wale waliodhaniwa ni makada kindakindaki wa chama fulani au kingine, nao ‘wakiruka ukuta’ na kuhamia ng’ambo ya pili.

Ingawa jambo hili limekuwa likitokea katika nchi yetu na nyinginezo, imezoeleka kuwa mambo haya hutokea mwaka mmoja au miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu. Matukio ya hivi karibuni ya wanasiasa, viongozi na makada wa vyama mbalimbali kuanza kuhama vyama vyao kwenda kwingine ni matukio yanayoleta maswali mengi, ingawa baadhi yao wamejaribu kutoa sababu za kwa nini wanahama vyama vyao, tena wakati huu, majibu yao yanaonekana kutoka midomoni mwao zaidi kuliko mioyoni.

Kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kusema wakati wa uhai wake, ukitaka kujua ukweli wa mtu mtazame usoni wakati akizungumza na unapaswa kuona macho, uso na moyo vikiongea lugha moja. Sioni hilo katika nyuso, nyoyo na macho ya waliojiengua katika vyama vyao katika siku, wiki na miezi michache iliyopita.

Hii ndiyo sababu nimeamua kufanya uchambuzi wa kina kidogo juu ya hamahama hii inayoendelea.

Wimbi la kuhama limeshamiri kutoka kila kona ya vyama, hasa vile vikubwa – Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT - Wazalendo na Chadema vinaonekana kukumbwa zaidi na sakata hili.

Wakati fulani, CCM imedai kupokea maombi ya wanachama 200 kwa siku moja kutoka vyama mbalimbali kutaka kujiunga nacho. Kati ya wanaohama, wapo ambao wameshakuwa wanachama wa vyama vingine viwili hadi vitatu katika miaka ya karibuni, huku wengine wakiwa wamesharudia vyama walivyotokea zaidi ya mara moja.

Inaendelea uk 26

Hii imetukumbusha Richard Tambwe Hiza ambaye wakati fulani amewahi kuondoka NCCR-Mageuzi kwenda CUF na baadaye kurejea tena CCM kabla hajahamia Chadema aliko sasa.

Wengine wamewahi kuwa na kadi mbili au tatu kwa wakati mmoja kwa sababu ya kukosekana kwa utaratibu madhubuti na wa wazi wa kurejesha kadi wakati wa kujiunga na chama kipya cha siasa. Ilifika wakati fulani, wanachama na mashabiki wa Chadema na CCM waliwahi kuhoji iwapo katibu mkuu wa Chadema wa wakati huo (2015), Dk Willibrod Slaa aliwahi kurejesha kadi ya CCM au la. Katika pita pita yangu, niliwahi kukutana na watu walioamini kuwa Dk Slaa alikuwa wakati wote ni mwanachama wa Chadema na CCM pia.

Ingawa ilikuwa ni vigumu kuamini jambo hilo kwa wakati huo wa umachachari wa Dk Slaa, imekuja kuwa rahisi kwa sasa watu kuamini kuwa yamkini hajawahi kuachana na CCM.

Kujiuzulu kwake kutoka nafasi ya ukatibu mkuu mwaka 2015, na kujiengua katika siasa za vyama ni vitendo vilivyoleta wasiwasi na shaka kubwa juu ya uanachama na ukada wake wa Chadema.

Aidha, kuteuliwa kwake hivi karibuni na Rais John Magufuli kuwa balozi akisubiri kupangiwa kituo cha kazi kumezidi kuchagiza imani kuwa Dk Slaa anaweza kuwa alibaki na uanachama wa CCM hata wakati akiwa Katibu Mkuu wa Chadema.

Vivyo hivyo, kujiengua kwa baadhi ya viongozi wazito wa vyama katika siku na wiki za hivi karibuni kumezua gumzo. Hivi nani alijua kuwa mtu kama Lazaro Nyalandu, mbunge wa Singida Kaskazini kwa miaka 17 na waziri wa Maliasili na Utalii angefikia kujiengua kutoka chama CCM na kujiuzulu nafasi zake zote za kibunge na kichama ?

Kwa wasiofahamu, wabunge wana nafasi ya kibunge, kichama na kiserikali na ndiyo maana wanasafiria pasi za kidiplomasia ambayo maana yake ni kuwa wao ni wakala wa Serikali. Kwa kung’atuka kwake chamani, Lazaro Nyalandu amepoteza ubunge, ujumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa, ujumbe wa Kamati za kudumu za Bunge na amepoteza pia hadhi na pasi ya kidiplomasia.

Katika waraka wake wa kuachia ngazi, Nyalandu anataja sababu zilizomfanya afikie maamuzi hayo kuwa ni pamoja na kuchoshwa na tabia na mwenendo wa Serikali ya CCM kunyanyasa raia, kuvunja haki za binadamu, dhuluma na mapungufu ya kidemokrasia.

Kwa mtazamo wa Nyalandu, CCM kimepoteza dira na mwelekeo kama chama cha Mapinduzi, cha wakulima na wafanyakazi kiasi kwamba yeye haoni haja ya kujihusisha nacho. Akiwa ametoa tamko zito la kiasi hicho, Nyalandu akatulia kwa muda mfupi lakini ndani ya wiki moja akaamua kujiunga na Chadema. Kwa faida ya wanaoweza kuwa wamesahau, Nyalandu pia aliwahi kutumikia kama naibu waziri wa Viwanda na Biashara katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 kabla ya kuwa Waziri kamili wa Maliasili na Utalii.

Aidha, kwa wakati tofauti alitumikia kama mjumbe wa Kamati za Kudumu za Mambo ya Nje na baadaye katika Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) hadi mwaka 2015. Wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita, Nyalandu alijitosa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais katika ngazi ya ndani ya chama, lakini jina lake lilitupwa katika hatua za awali hadi kupelekea ushindi wa Rais, John Magufuli.

Hii ndiyo sababu imewashangaza wengi, nikiwemo mimi kusikia tamko la chama tawala kuwa kuondoka kwa Lazaro Nyalandu hakuna wala hakutaleta madhara yoyote katika siasa ndani na nje ya CCM.

Vinginevyo, Chadema imeathirika sana na kinachoendelea na utabiri wangu ni kwamba kwa jinsi mambo yanavyokwenda itazidi kuathirika na hamahama kwa sababu nitakazozieleza katika makala hii.

Baada ya pigo la kuondokewa na Katibu Mkuu mwaka 2015, Chadema imepoteza hivi majuzi wanachama muhimu sana. Kwanza, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha amerejea kwa mbwembwe akitumia fursa ya mkutano wa ndani wa CCM uliofanyika Ikulu kueleza ya moyoni. Imenishtua kwa kweli, kusikia Masha akitamka kuwa yeye tangia hapo ni zao la CCM kwa damu.

Katika kuthibitisha hilo, Masha alileta hadithi ya wazazi wake hasa baba yake ambaye anakiri kuwa alimlaumu alipoondoka CCM akimwambia mimi nilifukuzwa wewe umeondoka mwenyewe. Kwa tunaotaka kujifunza kitu, hili linamaanisha nini?

Masha ni mwanasheria na wakili nguli wa mahakama. Katika medani ya siasa, aliwahi kuwa mjumbe wa NEC wa CCM na mbunge wa Nyamagana katika Mkoa wa Mwanza kwa muda wa kutosha. Baada ya misukosuko kadhaa ikiwemo kukamatwa na kufikishwa mahakani kwa makosa kama kuzuia polisi wasifanye kazi zao na mengine kama hayo, Masha ameona kuwa amechoshwa na shida na anarejea nyumbani.

Mara ya mwisho kwa Masha kujaribu bahati yake ndani ya Chadema ilikuwa ni Machi mwaka huu alipojitosa kujaribu kugombea ubunge wa Afrika Mashariki (EALA).

Hata hivyo, hila zilizofanywa dhidi yake, na madhila mengine yalimfanya aone kila rangi na kuchoshwa kabisa na kuwa mpinzani. Bila shaka mizengwe kwake wakati ule mwingine vimechangia sana kumkatisha tamaa na kuamua kuachana na siasa za upinzani.

Kwa sasa, wako wanaojiuliza juu ya hatma ya kuondoka kwa Masha, Chadema ikizingatiwa kuwa yeye ni mmoja kati ya waliohama CCM pamoja na Edward Lowassa ambayo inaanza kuwatia hofu wanachama wa Chadema na Ukawa endapo kuondoka kwa washikirika kama hao hakutamtisha Lowassa pia na kuamua naye ‘kurejea nyumbani’ pia.

Mtu mwingine ambaye kuondoka kwake kumekuwa pigo kubwa kwa Chadema ni aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana Bavicha, Patrobas Katambi. Nimjuavyo, Katambi alifanya ushujaa mkubwa kabla ya kujiunga na Chadema wakati alipoamua pamoja na kuwa mfanyakazi wa Sahara Media wakati huo inayomilikiwa na Mwana CCM, Anthony Diallo kujiunga na chama cha upinzani. Wako wanaojiuliza, hivi Katambi aliondoka CCM? Lakini mpaka wiki chache zilizopita alikuwa jukwaani akikitetea Chadema, Ukawa na sera zake.

Ni kwa namna hiyo, kuondoka kwa kiongozi wa Bavicha kunaweza kuzorotesha hamasa ya vijana ndani na nje ya chama na Ukawa na kuwafanya wasimwanini mtu tena ndani ya siasa za upinzani.

Hili likitokea linaweza kuathiri vibaya siasa za ushindani nchini, ikizingatiwa kuwa kama ilivyo dini, siasa ni imani. Nini kitapaswa kufanyika ili imani ya vijana wapenda mabadiliko irejeshwe ni kazi ambayo wana Chadema, Ukawa na wapinzani wote watapaswa kuiwekea mikakati madhubuti na ya haraka.

Kwingineko, sura nyingine zilizojiunga na CCM kutoka upinzani zimetokea ACT- Wazalendo. Hawa nao wanakidhi vigezo vya ‘kukatwa mkia’ kama Mwenyekiti wa CCM alivyowahi kutania wakati akiwapokea baadhi ya wanachama wa upinzani wanaorejea CCM. Hawa ni pamoja na Samson Mwigamba, Profesa Kitila Mkumbo na wakili Albert Msando.

Wakati Profesa Kitila hajashangaza sana watu kwa kuwa alishakuwa serikalini kama katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Mwigamba ameshangaza wengi. Ni mmoja wa walioanzisha ACT-Wazalendo baada ya hali ya hewa kuchafuka Chadema kutokana na jaribio la mageuzi ndani ya chama hicho miaka michache iliyopita.

Kwa anayemjua Mwigamba, ilikuwa ni vigumu kuamini kuwa anaweza kujiunga na chama chenye kanuni, sheria, taratibu na miongozo mikali kama CCM. Kwa ujumla, amejipambanua kama mwanasiasa jasiri, mwenye msimamo na ambaye hawezi kuimba wimbo wa “Ndiyo Mzee”, jambo ambalo linatia shaka kama anaweza kudumu ndani ya CCM kama ya wakati huu. Pamoja na hayo, wako wanaojipa muda na kusema “ngoja tuone”.

Pamoja na Profesa Kitila na Mwigamba, wamekuwapo wasindikizaji kutoka ACT Wazalendo. Jina la Edna Sunga si jina linalofahamika sana masikioni mwa Watanzania. Wako watu walionitumia ujumbe wakiniuliza, eti “Edna Sunga anafananaje?”

Ili kuepukana na umbea niliamua kuwatuliza kwa kuwajibu mtamfahamu zaidi sasa kwa kuwa amepata na atazidi kupewa fursa ya kutumikia taifa. Hivi ndivyo alivyowahi kusema rafiki yangu mmoja alipoteuliwa miaka michache iliyopita. Aidha, yupo mwingine, Wakili Msando ambaye pamoja na kufahamika sana, umaarufu wake ni kwa sababu tofauti na siasa, bali ni muunganiko wa uwakili wake mahakamani na harakati zake mbalimbali nchini.

Nako nje ya ACT-Wazalendo, kumekuwa na sura za vishindo zikiwa mstarini kuingia chama tawala. David Kafulila (NCCR – Mageuzi, Chadema) ni mwanasiasa aliyejizolea umaarufu mkubwa katika Bunge lililopita ambalo alilitumikia kwa miaka mitano kama mbunge wa Kigoma Kusini hadi 2015 huku akipambana na misukosuko mikali ndani na nje ya chama chake wakati huo, NCCR Mageuzi.

Wakati fulani, Kafulila alishambuliwa sana na mbunge mwenzake wa chama hicho, Moses Machali, ambaye pia alikuwa ni katibu mwenezi wa NCCR-Mageuzi huku akimfananisha kama kansa ndani ya chama hicho.

Wakati hayo yakitokea ndani ya chama, nje nako kulikuwa kukimwakia moto huku mapambano yake dhidi ya kashfa za ufisadi ndani ya Serikali ya CCM zikimgonganisha na vigogo mbalimbali akiwemo mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Jaji Frederick Werema, aliyediriki kumwita mbunge huyo tumbili.

Pamoja na kuitwa hivyo kama tusi, Kafulila hakuonekana kukata tamaa kabisa dhidi ya mapambano ya ufisadi, kitu kilichomfanya kuendelea kujizolea sifa lukuki ndani na nje ya nchi. Kwa kazi yake hiyo, Kafulila alitunukiwa ziara ya kimafunzo kwenda Marekani kujifunza zaidi masuala ya kupambana na rushwa, hongo na ufisadi jambo analolikumbuka mpaka sasa.

Imekuja kama mshangao kuwa Kafulila ameamua kuachana na vyama vya upinzani na kujiunga na CCM, chama ambacho pamoja na mabadiliko katika nyanja zake mbalimbali za uongozi, bado ni kilekile, rangi ileile. Imekuwa ni faraja kumsikia Kafulila akijitetea kuwa sababu kubwa ya kujiunga na CCM ni Rais Magufuli, ambaye kwa maoni yake ndiye mpambanaji mahsusi wa vita dhidi ya ufisadi.