Hatifungani za halmashauri chanzo kipya mapato kwa miradi ya maendeleo

Muktasari:

  • Likiwa na miaka 22 tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, kampuni zilizoorodheshwa sokoni hapo imefika 27; saba zikiwa ni kampuni na zinazobaki za ndani. Kampuni za nje zilizoorodheshwa DSE zimefanya hivyo kwenye masoko mengine pia.

Wakati idadi ya kampuni zinazoorodheshwa katika soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ikiendelea kuongezeka, wawekezaji na bidhaa zinazopatikana sokoni hapo zinaongezeka pia.

Likiwa na miaka 22 tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, kampuni zilizoorodheshwa sokoni hapo imefika 27; saba zikiwa ni kampuni na zinazobaki za ndani. Kampuni za nje zilizoorodheshwa DSE zimefanya hivyo kwenye masoko mengine pia.

Kutokana na wawekezaji waliopo sokoni hapo, mtaji wa DSE umefika Sh23 trilioni huku kampuni mpya iliyooroshwa wiki iliyopita, Kampuni ya Uwekezaji wa Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA Investment) yenye mtaji wa zaidi ya Sh30 bilioni ukitarajiwa kuongeza wawekezaji 3,400.

Tangu hatifungani za Serikali zilipoanza kuuzwa kwa mara ya kwanza sokoni hapo mwaka 2002, bidhaa nyingine inatarajiwa kuanzishwa ama mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwakani.

DSE linajipanga kuzindua uuzaji wa hatifungani za halmashauri au ‘municipal bonds’ kama zinavyofahamika kimataifa ili kuzijengea Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mfumo wa soko.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ilitangaza kuanza kuuzwa kwa hatifungani hizo za halmashauri.

Mkakati huo ulibainishwa na Mwenyekiti wa CMSA, Dk John Mduma na kuthibitishwa na Meneja wa Fedha na Utafiti wa DSE, Ibrahim Mshindo.

“Moja kati ya mikakati ya mamlaka kwa mwaka huuwa fedha 2018/2019 ni kusaidia uanzishwaji na utoaji wa hatifungani za Serikali za Mitaa. Mpango huu unatarajiwa kuimarisha masoko ya mitaji kwa kuzileta pamoja sekta zote muhimu hivyo kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema Dk Mduma.

CMSA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango. Ilianzishwa mwaka 1994 ili kusimamia na kuendeleza masoko ya mitaji nchini.

Miongoni mwa majukumu ya mamlaka hiyo ni kuidhinisha uanzishwaji wa masoko ya hisa na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, kutoa leseni kwa wataalamu wa masoko wakiwamo madalali, wachuuzi, wawakilishi na washauri wa uwekezaji.

Mengine ni kuishauri Serikali masuala yote yahusuyo masoko ya mitaji na dhamana. Kwa sasa, CMSA inachangia asilimia 30 kwenye Pato la Taifa na lengo lililopo nikuongeza mchango wake ufike asilimia 60 mwaka 2025.

Hatifungani za halmashauri

Meneja wa fedha na utafiti wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Ibrahim Mshindo anasema wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha hatifungani hizo zinaanza kuuzwa katika robo ya mwisho ya mwaka huu (kati ya Septemba na Desemba) au robo ya kwanza mwakani (Januari mpaka Machi).

“Ni bidhaa ambayo tumeiandaa kwa miaka minne sasa. Tukifanikiwa kuiingiza sokoni, Tanzania itakuwa nchi ya pili Afrika kuwa nayo. Kwa sasa ni Afrika Kusini pekee walionayo,” anasema Mshindo.

Kama zilivyo hatifungani nyingine, wamiliki wa hatifungani za halmashauri watakuwa wanalipwa riba mara mbili kila mwaka ndani ya muda wa dhamana hiyo.

Kwa kawaida, kuna aina mbili za hatifungani za halmashauri; za muda mrefu au muda mfupi. Za muda mrefu huweza kuwa za miaka 10 na kuendelea wakati za muda mfupi huwa kati ya mwaka mmoja mpaka mitatu.

Wawekezaji wa hatifungani za halmashauri wana uhakika wa kulipwa riba kwani mara nyingi mamlaka hizo hutumia fedha inazokusanya kutoka kwenye chanzo chake cha uhakika au mapato yatokanayo na kodi au tozo za aina tofauti.

Kwa muda wa uhai wa hatifungani husika, mwekezaji anaweza akaiuza kama anazo sababu za msingi kufanya hivyo.

Kuanzishwa kwa hatifungani hizi kunatokana na ushauri wa kitaalam uliotolewa. Mshindo anasema Benki ya Dunia itoa ushauri huo baada ya kuona uwezekano wa kuongeza chanzo hicho cha mapato endapo mabadiliko madogo yatafanyika kwenye uendeshaji wa halmashauri nchini.

Baada ya kufanya tathmini ambayo sasa imefika miaka minne, mwaka jana, anasema walianza kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kuendesha mafunzo ya kuzijengea uwezo halmashauri nane na nne zikakidhi vigezo.

Halmashauri hizo zilizoalikwa kwenye warsha iliyofanyika Juni mwaka jana ni Arusha, Tanga, Mwanza, Ilemela, Nyamagana, Ilala, Temeke na Dar es Salaam. Baada ya mafunzo yaliyotolewa kwa maofisa waandamizi wa halmashauri hizo; Arusha, Mwanza, Tanga na Ilemela ndizo zilizoonyesha shauku ya kuitumia fursa hiyo.

“Hatifungani ya kwanza itakuwa ya Halmashauri ya Mwanza. Tutanza na hiyo moja itakayokuwa ya mfano. Kuna mabadiliko kadhaa ya kimuundo yanahitaji kufanyika ili kuendana na matakwa ya soko,” anasema Mshindo.

Mara kadhaa, halmashauri zimeshindwa kukamilisha ama miradi yake ya maendeleo au kiradi ya kijamii kutokana na kukosa fedha za kufanya hivyo. Kushindwa huko, pamoja na sababu nyingine, kunaelezwa kuchangiwa na utegemezi wa fedha kutokana na ruzuku ya Serikali au zitolewazo na wafadhili.

Baada ya kuona changamoto hiyo, anasema kamisheni ya mipango inayowahusisha makatibu wakuu wote iliridhia kuongezwa kwa chanzo hicho cha mapato kwa halmashauri.

“Kila halmashauri ina nafasi sawa ya kutumia fursa hii kutekeleza mradi utakaokuwa na ushawishi wa wawekezaji kutoa fedha zao,” anasema Mshindo.

Kuimarika kwa DSE kutaboresha sekta ya fedha kwa ujumla. Mshindo anaamini: “Upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya maendeleo ya wananchi na mfumo wa fedha uliopo katika nchi husika.”

Muundo halmashauri

Kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Serikali ya Marekani (USAid), Mshindo anasema UNCDF imekubali kuzisaidia halmashauri kufanya mabadiliko ya kimuundo.

Mabadiliko hayo ni muhimu kwani, Mshindo anasema kuna mambo mawili ambayo ni lazima yafanyike kabla halmashauri husika haijauza hatifungani zake sokoni hapo.

Eneo la kwanza linalohitaji mabadiliko, anasema ni muundo wa halmashauri kutokana na sheria ilizoziunda pamoja na uwezo wa rasilimaliwatu inayoandaa miradi husika.

Mmiongoni mwa watu muhimu wanaopaswa kujengewa uwezo kutoka kwenye kila halmashauri ni pamoja na mkurugenzi, ofisa mipango, baraza la madiwani, ofisa tawala na mkuu wa mkoa au wilaya.

Wadau

Kuongezwa kwa vyanzo vya mapato vya halmashauri ni fursa inayoshauriwa itumike kwenye taasisi au mamlaka nyingine za umma kufanikisha malengo yao kwa wakati.

Mhadhiri mwandamizi wa uchumi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema si halmashauri pekee bali hata taasisi nyingine za umma.

“Kitu kizuri ni kwa wawekezaji ni kupata fixed rate (riba isiyobadilika kwa muda wote wa uwekezaji). Kinachozingatiwa ni uwezo wa taasisi inayokopa kulipa kiasi husika kwa wakati,” anasema.

Kutokana na watu wengi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na mwenendo wa soko la hisa, Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob anasema wajumbe wa baraza la madiwani wanahitaji kuelimishwa kabla hawajaidhinisha matumizi ya hatifungani hizo.

“Masuala ya soko la hisa na bidhaa zake yanahitaji utulivu. Kumbuka, kigezo cha kuwa diwani ni kujua kusoma na kuandika ila uwekezaji kwenye soko hilo unahitaji maarifa zaidi ya hayo. Madiwani wanahitaji kuelimishwa,” anasema Meya Jacob.