Hatujachelewa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji

Muktasari:

Ni kweli kuwa kuna mgogoro wa kiitikadi kati ya wakulima na wafugaji. Kila mmoja anaamini kuwa na haki na ardhi kuliko mwingine. Kila mmoja akionyesha kuhitaji ulinzi wa sheria kuliko mwingine. Ama kuhitaji utetezi wa jamii kuliko mwingine.

Mgogoro wa wakulima na wafugaji umeendelea kupata sura mpya kila kukicha, uhasama wa makundi haya mawili kinzani unazidi kuongezeka, kupanuka na kuhusisha makundi mengine ya jamii. Angalau katika hili tumeona sura halisi ya tatizo ikilenga uhalisia wa tatizo lenyewe bila kuhusisha siasa.

Ni kweli kuwa kuna mgogoro wa kiitikadi kati ya wakulima na wafugaji. Kila mmoja anaamini kuwa na haki na ardhi kuliko mwingine. Kila mmoja akionyesha kuhitaji ulinzi wa sheria kuliko mwingine. Ama kuhitaji utetezi wa jamii kuliko mwingine.

Ukweli utabaki siku zote kuwa wakulima na wafugaji ni raia wa Tanzania na kwa hiyo changamoto zao, shida zao, adha zao na fadhaa zao ni sehemu ya maisha yetu sote. Ni kwa sababu hiyo hatuwezi kukaa mbali na ndugu zetu hawa wakiumizana, wakiharibu mifumo ya maisha yao na hata wakiuana na kupotezeana maisha, mali na thawabu zingine.

Siku za hivi karibuni jamii hizi zimepata ama zimesababishiana simanzi kubwa maeneo mbalimbali nchini. Ninafikiri wakati unatosha kusema imetosha sasa, tufikishe jambo hili mwisho wake. Tuweke juhudi zetu zote kuhakikisha hakuna mfugaji atapigana na mkulima tena kwa sababu ya malisho, upungufu wa ardhi ama malisho.

Jambo hili linahusu wizara moja mama na wizara zingine. Wizara mama hapa ni Wizara ya Ardhi, mipango miji na sheria ya aridhi ya vijiji. Inaonekana ufugaji wa kutembea kutafuta malisho umepitwa na wakati. Hauna mashiko tena.

Wafugaji wanahitaji kwanza wao wenyewe kuangalia mbinu mpya za ufugaji. Kupunguza mifugo pengine si suala la msingi, isipokuwa kwa matumzi mengine. Ufugaji ni uwekezaji. Upewe fursa kukua na kuchangia pato la taifa, kuondoa umaskini, kutoa ajira kwa vijana na wazee.

Ufugaji ni biashara kubwa tu. Siyo nchi zote ama jamii zote zimejaliwa mifugo tuliyo nayo sisi. Ni fahari kuwa na mifugo mingi. Ni fahari zaidi kuwa na sera ya kulinda na kuhifadhi ufugaji wa faida. Na hii si kazi ya wafugaji peke yao. Ni kazi yetu sote.

Ni kazi ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na hata kazi ya uongozi wa mila kusaidia kuonyesha njia kuzuia migogoro iliyopo. Inashangaza kuwa tuna uongozi ngazi hizi zote, lakini bado tumeshindwa kabisa kutumia fursa hizi kutatua jambo hili.

Katika uchanga wa uchumi, kila fursa ya kuongeza kipato ama chakula ama lishe kina umuhimu wake. Kila eneo dogo la mkulima ni sehemu ya maeneo mengine madogo madogo yanayohitajika kufanya mashamba makubwa yanayotunza mamilioni ya Watanzania mijini na vijijini.

Na kila mfugo mmoja ni sehemu ya mifugo mingine michache inayofanya idadi ya mifugo inayotupa maziwa na nyama, ngozi, kwato na mifupa yenye matumizi mengi siku hizi. Vyote vina thamani. Vyote vipewe umuhimu na kipa umbele kwa manufaa ya taifa zima.

Wafugaji wanahitaji ardhi. Wakulima pia. Ardhi ipi bora kwa kilimo na ipi kwa kufuga? Wizara ya ardhi wametenga maeneo gani kwa kila matumizi? Wafugaji wanatakiwa wapi na hawatakiwi wapi?

Kiteto ni eneo la wafugaji kwa asili, lakini ardhi ile inakubali kilimo pia. Mgawanyo umewekwaje kuhakikisha usawa wa makundi haya ndani ya jamii moja?

Ngorongoro ni eneo la wafugaji na linafaa pia kwa kilimo na kwa uhifadhi wa wanyama pori. Tumeweka utaratibu gani sahihi kuhakikisha kuwa ikolojia ya msitu inatunza wanyama na wanadamu bila bugudha? Kwa vyovyote vile mwanadamu hajawahi kuwa tishio kwa mnyama wa pori, licha ya mnyama kuwa tishio kwa usalama wa binadamu.

Kwa namna ya uumbaji wa asili, wanyama na wanadamu wa maeneo ya hifadhi humudu kuishi pamoja katika mazingira ambayo taifa linafaidika na uwapo wa wote wawili, unahitajika utaratibu wa kuwalinda na kuwahifadhi wote.

Wanyama na wanadamu kule kuishi kwao pamoja kutunufaishe sisi wote. Hii ni kazi yetu na ni wajibu wa haki kuutimiza. Hapa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili, Wizara ya huduma za jamii, elimu na utamaduni zote zinaingia kila moja ikisimamia kundi lake na kuhakikisha linapata kutoka kwa jamii hifadhi stahiki.

Ni kwa nini mpaka leo hatupati suluhu ya mgogoro huu wa rasilimali, inashangaza na hasa ikizingatiwa kuwa makundi haya yote kwa pamoja yana watu wengi wenye ushawishi na uelewa mkubwa wa jamii.

Kwa kuwa nchi yetu ina ardhi ya kutosha Wizara ya Ardhi iwagawie wafugaji maeneo yanayofaa kwa ufugaji wa ndani usiohitaji kutembea kupata malisho.

Wizara ya Maji ihakikishe wafugaji wana maji ya kutosha kwa malisho na mifugo yao ili wafugaji waamini miundombinu hiyo ya maji ya mabwawa, malambo ama mifereji ya umwagiliaji wa malisho ya wanyama wao ama ya aina yoyote watakayochagua wao na kuthibitisha kuwa inafaa.

Kampuni za bima ziwasaidie wafugaji kukata bima ya mifugo yao na kupata fidia yao kunapotokea uharibifu.

Hatuwezi kukimbia majukumu ama dosari za kimaamuzi yaliyotokea nyuma na kutusababishia uharibifu uliopo sasa. Hata hivyo, hatuwezi kukwepa tukishindwa kuwa wabunifu kiasi cha kutosha na kubaki kulalamika.

Baraza la wafugaji na baraza la wakulima na viongozi wengine wakae pamoja kuweka maelekezo kwa kila idara ya umma inayohusika na suala hili.

Ushirikishwaji uonekane ukifanyika na kutumiwa bila upendeleo wala ubaguzi. Wanawake kwa wanaume wakulima na wafugaji washiriki na kuweka hatima ya maisha yao mikononi mwao, waweke mipaka na uaratibu wa kuishi pamoja bila kumsababishia hasara mwingine.

Mwandishi ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]