Hawa wanaweza kucheza ligi popote duniani

Muktasari:

  • Nyota wa Tanzania Mbwana Samatta ametajwa katika wachezaji hao akiwa sambamba na wakina Mohammed Salah na Sadio Mane wa Liverpool ya Uingereza na nyota wengine wengi wanaocheza Ulaya.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wiki iliyopita lilitangaza majina ya wachezaji ambao wanacheza Ulaya ila ni wa Afrika kwa maana ya kumtafuta mmoja ambaye atakuwa mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka huu.

Nyota wa Tanzania Mbwana Samatta ametajwa katika wachezaji hao akiwa sambamba na wakina Mohammed Salah na Sadio Mane wa Liverpool ya Uingereza na nyota wengine wengi wanaocheza Ulaya.

Samatta anaweza kuwa chachu kwa wachezaji wa Tanzania kupenda kucheza nje kama ilivyo kwa wakina Saimon Msuva, Farid Mussa na wengine wengi waliotamani zaidi mafanikio ya kisoka.

Gazeti hili linakuletea wachezaji ambao unaweza kufikiria kuwa kama wakikaza na wakiwa na roho ya kutaka mafanikio katika soka na kuacha kufikiria zaidi klabu za Simba, Yanga na Azam wanaweza kufika mbali.

Aishi Manula, Simba

Unaweza kusema ndiye golikipa namba moja kwa sasa hapa nchini kwani bila shaka ndio kipa ambaye amecheza katika kiwango chake cha juu bila ya kushuka kwa wakati wote akiwa katika klabu yake na timu ya Taifa.

Manula ndio kipa namba moja wa Simba na timu ya Taifa alisajiliwa na kikosi hiko akitokea Azam, mwanzoni mwa msimu huu lakini amedumu katika kiwango kilele licha ya kucheza timu yenye presha kubwa ya mashabiki.

Ukweli usiopingika Manula kwa uwezo wake, umbile lake, na umri wake ni wazi kwamba anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wasipolewa sifa za mashabiki wa Simba na kufikiria kucheza nje na wakafanikiwa.

Erasto Nyoni, Simba

Ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi kama baki, kiungo mkabaji na mshambuliaji na kadumu katika kikosi cha timu ya Taifa katika makocha wote waliowahi kufundisha tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza na Mbrazil Marcio Maximo.

Japo umri umemtupa mkono, na kama haitoshi, Erasto ameendelea kuwa mahiri na kudumu katika kiwango chake kile kile tangu alipokuwa na Azam na sasa Simba na ameweza kuwa mchezaji mwenye mchango mkubwa katika kikosi hiko na amehusika katika nusu ya magoli ambayo wamefunga.

Sababu kubwa ambayo Erasto anaingia katika wachezaji ambao wanaoweza kucheza popote duniani, ni uwezo wake wa kutumia miguu yote miwili bila shaka na kuweza kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani jambo ambalo kwa dunia ya sasa kuna wachezaji wachache sana kama yeye.

Mohammed Hussein, Simba

Hakuanza vizuri msimu huu kwani ameanza na majeraha katika kikosi chake cha Simba jambo ambalo alikuwa na nafasi ya kusuasua katika kikosi chake lakini mambo yameanza kukaa sawa na ameanza katika mechi tatu zilizopita katika kikosi cha kwanza.

Ana uwezo mzuri wa kucheza katika eneo la fulubeki wa kushoto jambo ambalo anaingia katika wachezaji wenye uwezo wa kucheza katika nchi yoyote Ulaya na kwa umahiri wake mkubwa wa kukaba na kushambulia anaweza kupata mafanikio zaidi kama atapata nafasi ya kucheza huko.

Tshabalala ana uwezo pia wa kupiga krosi ambazo straika hawezi pata tabu ya kumalizia na kuweka kambani jambo ambalo tunaona wapo wachezaji Ulaya wanacheza kama yeye kwahiyo kama atakubali kuziacha kelele za mashabiki wa Simba anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanacheza nje.

Kelvin Yondan, Yanga

Beki kisiki mkongwe wa kati wa Yanga. Ana uwezo wa kucheza mipira ya juu na chini lakini kama haitoshi ni hodari kuwazuia mastraika wote wasumbufu, pia anauwezo wa kucheza mpira wa nguvu na wa kistarabu.

Uzoefu na uwezo wa Yandon ni wazi kwamba ana uwezo mkubwa wa kucheza ligi yoyote Ulaya kwani ni miongoni mwa mabeki wa kati waliokuwa imara tuliokuwa nao hapa nchini takribani miaka mitano sasa.

Aggrey Morris, Azam

Si mwongeaji sana lakini kazi yake inatosha kabisa kumwelezea vya kutosha kwani msimu huu ametengeneza ngome ngumu ya ulinzi na Yakub Muhammed, lakini si hiyo tu amekuwa bora wakati wote katika kikosi cha Azam.

Morris amehimili mikikimikiki ya Ligi Kuu kwa uwezo mkubwa kabisa kwani amewazuia mastraika wote wasumbufu raia wa kigeni na wazawa pia, na kwa uwezo huo anaingia katika wachezaji ambao wanaweza kucheza ligi nje ya Tanzania.

Himid Mao, Azam

Kiungo mkabaji wa Azam na Taifa Stars huwezi kutaja kiungo mkabaji kwa sasa hapa nchini ukaacha jina na Himid ambaye amekuwa akiimarika kila inapoitwa leo katika kila mechi ambayo anacheza unaweza kusema ni mchezaji mpya.

Himid ndio kiungo bora kwa sasa hapa nchini kuliko kiungo yoyote yule na kabla ya msimu huu kuanza alikwenda nchini Denmark ambako alifanya majaribio katika klabu ya Randers FC, kufuzu lakini masuala ya kimaslahi yalikwamisha dili hiyo.

Shiza Kichuya , Simba

Msimu mmoja na nusu tu alichokuwa katika kikosi cha Simba ametosha kuonyesha kuwa ni mchezaji mwwa aina gani. Amefunga magoli 12, msimu uliopita kwenye ligi kuu Bara.

Kichuya pia msimu huu licha ya kikosi cha Simba kutawaliwa na wachezaji nyota kama Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi amekuwa katika kiwango chake kile kile kwani hadi sasa ameshafunga mabao matano huku akiifunga Yanga katika mechi tatu mfululizo.

Mkataba wa Kichuya unamalizika mwisho wa msimu huu na kiwango alichoonesha ndani ya Simba ni wazi kwamba kutakuwa na timu nyingi ambazo zinahitaji huduma yake kutoka nje na huu ndio wakati wake wa kwenda kucheza nje na nchi yoyote anaweza kucheza.

Said Ndemla, Simba

Kiungo fundi wa Simba mwenye nidhamu nje na ndani ya uwanja bila shaka kwa uwezo wake wa kucheza mpira wa kupiga pasi ndefu na fupi ndio kiungo ambaye anahitajika katika timu yoyote ile duniani na sina shaka kusema kuwa anastahili kwenda kucheza soka Ulaya na kutia ufundi zaidi.

Ndemla ana uwezo wa kupiga mashuti makali nje ya 18 pia ana uwezo wa kutoa pasi za mwisho na kupiga mipira ya azabu na huko Sweden ambako anakwenda kufanya majaribio, hakuna shaka ni wazi atafanya vizuri na kusajiliwa katika klabu ya AFC Eskilstu anayokwenda kujaribiwa.

Mzamiru Yassin, Simba

Kiungo wa Simba mwenye kipaji kikubwa cha kupiga pasi za mwisho na uwezo mkubwa wa kukaba ni wazi kwamba ameonyesha uwezo kwani kila inapoitwa leo amezidi kuimarika anapokuwa katika kila mechi hata katika kikosi cha Stars pia.

Mzamiru amekuwa muhimili katika kikosi cha Simba na ni sehemu ya mafanikio ya kikosi cha timu hiyo, mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu bila ya kupepesa macho ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kucheza nje kwani amukuwa na kiwango kinachoimarika kila wakati.

Mbaraka Yusuf, Azam

Straika wa Azam ambaye walimsajili kutoka Kagera Sugar msimu uliopita alifunga magoli 12, na kuisaidia timu yake kumaliza katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Ameanza msimu mpaka sasa ameshafunga mabao matatu na kwa uhodari wake wa kufunga na kusumbua walinzi. Ana uwezo wa kucheza soka nje ya Tanzania na kakubalika, kasi, nguvu na upigaji mashuti na zaidi ya yote ni umbo lake.

Mbaraka amekuwa msumbufu kwa mabeki mahiri kama Yondani, ambaye mbele yake aliweza kufunga mabao mawili, Juuko Murshid ambaye alimsumbua na kufunga bao mbele yake, ni moja ya sababu ambayo inanipa nguvu kubwa ya kuona kuwa ana uwezo kwa kwenda kucheza nje ya Tanzania kwani walinzi wa huko ni kama hawa wakina Juuko, Yondani na Mwanjali.

Raphael Daud, Yanga

Kiungo mpole wa Yanga aliyesajiliwa akitokea Mbeya City, si muongeaji wala mambo mengi lakini kazi yake ni kubwa anapokuwa kiwanjani kwani ni fundi wa kupiga pasi za mwisho na hata kwenye kukaba pia.

Raphae kabla ya kwenda Yanga alikuwa hakiitajika na baadhi ya timu kutoka Afrika Kusini lakini pengine maslahi yalikuwa madogo kuliko ya alipochagua kwenda lakini bado hajatoka kwenye orodha ya wachezaji ambao wanaweza kucheza nje.

Ibrahim Ajib, Yanga

Straika fundi wa Yanga mwenye uwezo mkubwa wa kuchezea mpira na kufunga alisajiliwa na timu hiyo akitokea Simba mwanzo wa msimu huu, na amekuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho kwani mpaka sasa ameshafunga mabao matano.

Ajib ameshakwenda nchini Misri na Afrika Kusini kufanya majaribio mara kwa mara jambo ambalo linanipa imani kuwa kama ataamua kuacha sifa ambazo anapata hapa nchini anastahili kwenda kucheza kwenye nchi yoyote Ulaya.

Hakuna mpenzi wa soka asiyefahamu shughuli ya Ajib ni miongoni mwa wachezaji tuliojaliwa Tanzania anakipaji kikubwa ila anayelewa sifa za mashabiki wa hapa Bongo lakini anauwezo mkubwa wa kwenda kucheza soka hata kwenye mataifa yaliyopiga hatua za soka.