Hekima, busara ni chachu ya mafanikio yako kiuchumi, kijamii

Muktasari:

  • Kwa hekima mtu hupanga mikakati yake ya muda mrefu na mfupi na kwa busara alizojaliwa huomba ushauri na kutafuta taarifa zote muhimu kabla ya kuanza kutekeleza anachokiamini. Kwa utaratibu huu, uwezekano wa kupata mafanikio ni mkubwa.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya hekima na busara za mtu na mafanikio yake kwenye shughuli anazozifanya ili kujiletea maendeleo na uhuru wa kiuchumi.

Kwa hekima mtu hupanga mikakati yake ya muda mrefu na mfupi na kwa busara alizojaliwa huomba ushauri na kutafuta taarifa zote muhimu kabla ya kuanza kutekeleza anachokiamini. Kwa utaratibu huu, uwezekano wa kupata mafanikio ni mkubwa.

Hili ni kwa masuala yoyote ambayo mhusika anakusudia kuyatekeleza. Iwe kazini, kwenye biashara zake au kwenye masuala yanayohusu jamii inayomzunguka. mipango sahihi na ushawishi uliopangiliwa hufanikisha jambo hata liwe gumu kiasi gani.

Mapema miaka ya 1990 kulifanyika mkutano kule Burkina Faso; “mkutano wa wenye hekima.” Hili lilikusa kundi la watu kutoka nchi na nyanja mbalimbali za maisha waliokuwa na lengo la kuisukuma mbele hekima katika utamaduni wa Kiafrika.

Ili kuwa mtu mwenye hekima huna budi kujenga mienendo anayotakiwa kuwa nayo mtu mwenye hekima, upeo mwafaka, maadili na kupanuka kwa akili. Hivi vyote viwe mali iliyo mwilini na maishani mwako. Hebu tujaribu kuangalia nyenzo zinazoweza kusaidia kuwa mtu mwenye hekima.

Kwanza, kuelewa kinaganaga maana halisi ya neno ‘hekima.’ Kuna mawazo mengi kuhusujambo hili. Yasome. Elewa jinsi gani mtu mwenye hekima anatakiwa kuwa. Anza kujifunza kuwa mtu mwenye hekima na hatimaye zitumie hekima hizo katika maisha yako ya kila siku.

Pili, ushauri nasaha. Kuwa mtu mwenye hekima ni mazoezi ya kujiendeleza ndani kwa ndani; ndani ya moyo wako! Na kwa kweli kuna shughuli ambazo ukizifanya zinakupeleka ilikojificha hekima.

Mafunzo kutoka kwa wataalamu na washauri nasaha yatakufikisha mahali pa kuanzia kuelekea kwenye hekima yenyewe.

Ukishafika hapo utaanza kupanda ngazi kuelekea juu zaidi. Hatua hii tunaweza kuiita hatua ya mtu mkomavu. Mtu aliye katika hatua hii amefikia kiasi cha kuweza kudhibiti hisia zake.

Anakuwa anaweza kuyajua mateso, kwa kiasi chake, ayapatayo mwenzie kama yale anayoyapata yeye.

Kuna aina nyingi za ushauri nasaha; namna ya kuyatawala maisha yako, kuondokana na hofu, namna ya kuweza kuitawala hasira, kuachana na ‘uteja’ wa jambo fulani na mambo mengine mengi kama hayo.

Tatu, kusoma kunaweza kutupeleka ilipo hekima. Kusoma mambo yanayohusu maendeleo ya ndani mwako kwaweza kuwa msaada mkubwa kwako kama unataka kuwa mtu mwenye hekima. Anza kujisomea mambo yatakayopanua upeo wako.

Masomo hayo yatakuongoza kufanya mazoezi mwenyewe ukiwa peke yako, kutuliza akili, kujijua undani wako au ya kupaisha uwezo wako kiasi cha kufanikisha mipango na mikakati uliyojiwekea maishani.

Riwaya, tamthilia na vitabu vinavyoelezea maisha ya watu maarufu ni rasilimali muhimu ziwezazo kukuelimisha kuhusu hekima kwa vitendo. Kwa kuwa vitabu hivi vinakupa mifano halisi ya tabia za hekima na tabia zisizo za hekima; utatuzi wa mambo ya kimaisha bila kutumia nguvu.

Vitabu vinavyoelezea maisha ya watu maarufu vinaweza kuwa vya msaada mkubwa, kuelewa namna tabia za watu hawa zinavyotofautiana na watu wa kawaida na maadili yanayoongoza maisha yao au upeo wa maisha wanaotumia.

Kama tunataka kuwa katika kundi la watu wenye nia ya kuibadilisha dunia, hatuna budi kuchagua rasilimali zitakazotusaidia kufikia mabadiliko tuyatakayo. Moja ya ni maarifa mapya kuhusu sayansi, mabadiliko ya ulimwengu au afya.

Nyingine ni kujifunza zaidi kuhusu utamaduni, mifumo ya uchumi na undani kuhusu ardhi na kuelewa maadili na mbinu za kubadili upeo wa kimaadili.

Inaweza kujulisha ujuzi wa kutatua migogoro, uwezo wa kuongea kwa mvuto na kujua mambo yote yanayotokea kwa lengo la kuibadili dunia.

Nne, uzoefu wa maisha. Kama tumejitolea kujifunza, maisha yenyewe ni mwalimu! Kwa kuwa na uzoefu wa mambo mengi tunakuwa tumetanuka kiupeo. Siyo tu tunatakiwa kuyagawa maisha yetu ili tuwe na uzoefu wa aina nyingi, bali kufungua akili zetu ili tuweze kufaidi uzoefu uliotamalaki dunia.

Katika kukuza uzoefu wako kwenye masuala tofauti ya maisha, ni busara kujuana na watu wenye ujuzi tofauti na wako kwa kufahamiana na watu wenye mtazamo tofauti na wako pia.

Juana na watu wenye maadili tofauti na yako bila kuwaacha wanaofanyakazi tofauti na yako na usiache kushiriki michezo na matukio mbalimbali yanayofanyika kwenye jamii inayokuzunguka. Mambo haya yote uongeza upeo katika maisha yetu na kutuongoza kwenye njia ya kuelekea kwenye hekima.

Tano, ushauri wa kujifunza kutoka kwa watu wenye hekima. Kaa karibu na watu ambao ungependa wawe mashujaa wako. Ni jambo jema kukaa na watu ambao ni waumini wa maadili unayoyataka. Kuna mijadala ya kukuza upeo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Jaribu kujifunza kutoka kwenye vikundi hivyo.

Sita, chunguza tabia zako na za wengine. Watu wote wanaotuzunguka wapo katika harakati za kutaka kuishi maisha bora zaidi ya wengine.

Tunaweza kutambua mikakati na tabia nzuri na mbaya kwa kujifunza na kujijua tulipo kimaadili. Kwa kufanya hivi tunaweza kujua kiundani zaidi kuhusu maadili.