Hii ndiyo nafasi ya michezo na utalii

Muktasari:

  • Pengine wapo mashabiki na wadau wa soka ambao bado hadi sasa hawajapata ufahamu wa umuhimu wa tukio hilo kubwa ambalo linakwenda kufanyika hapa nchini siku chache zijazo.

Ni bahati na fursa ya kipekee ambayo Tanzania imepata kutokana na kupata nafasi ya kuandaa mkutano huo hasa ukizingatia ukweli kwamba imekuwa ni nadra kwa nchi za Afrika hasa zile za ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati kuandaa matukio makubwa ya kisoka kama mkutano huo.

Pengine wapo mashabiki na wadau wa soka ambao bado hadi sasa hawajapata ufahamu wa umuhimu wa tukio hilo kubwa ambalo linakwenda kufanyika hapa nchini siku chache zijazo.

Kwa kulitambua hilo, Spoti Mikiki linakuletea tathmini ya jinsi Tanzania inavyoweza kunufaika kutokana na Mkutano wa Mwaka wa Fifa ambao utafanyika hapa jijini, Februari 22.

Kukuza Utalii

Ujio huo wa Infantino utahusisha maofisa na viongozi wa vyama na mashirikisho ya soka kutoka nchi mbalimbali duniani ambao siku chache watakazokuwepo zinaweza kutumiwa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kama Mbuga na Hifadhi za Wanyama, maeneo ya kihistoria pamoja na utamaduni wa jamii mbalimbali za Kitanzania.

Fursa ya kiuchumi

Ni wazi pato la nchi litaongezeka kwa siku hizo chache ambazo ujumbe wa Fifa utakuwepo hapa nchini kwani ujio wao utaimarisha na kufungua fursa za kibiashara pamoja na kuongeza fedha za kigeni ambazo watazitumia katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali katika siku zote watakazokuwepo Tanzania.

Wafanyabiashara wa hoteli ndio wanaonekana watanufaika zaidi kupitia mkutano huo kwani wao ndio watalazimika kutoa huduma za malazi na vyakula kwa wageni hao.

Mtazamo chanya

Sekta ya michezo hasa mpira wa miguu imekuwa haipewi kipaumbele kikubwa hapa nchini tofauti na kwingineko ambako michezo inatazamwa kama moja ya sekta muhimu za kukuza uchumi na pato la nchi.

Pengine ujio huo wa Fifa na wajumbe wake unaweza kubadilisha mtazamo uliopo kwa sasa kwa sekta ya michezo na kufungua zama mpya za kuthamini na kuitazama nyanja hii kama miongoni mwa mambo yanayoweza kuleta maendeleo kwa Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangala alisema mbali ya kuongeza imani ya nchi mbalimbali kwa Tanzania pamoja na kuongeza fedha za kigeni, pia utasaidia kuitangaza nchi.

“Ujio wa ndugu zetu wa Fifa kuja kufanya mkutano mkuu wa kimataifa nchini maana yake tunafaidika kwa kiasi kikubwa sana kwenye sekta hii ya utalii. Faida kubwa ya kwanza ambayo tunaipata ni kwamba, ujio wa Fifa unaitangaza nchi yetu.

Tutafaidika na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa, wakiwa hapa watalala kwenye hoteli, watakula vyakula vya hapa lakini pia wanaweza wakatamani kwenda kwenye mbuga za wanyama na kadhalika.

Nimeona niwaalike kutembelea mbuga za wanyama na vivutio mbalimbali vya utalii kama fukwe na maeneo mbalimbali ya kumbukumbu na historia tuliyonayo hapa nchini maeneo ya utamaduni ili wakienda huko kwao wawe mabalozi kwa wenzao. Nitatengeneza ‘package’ maalumu kuwapa kama ofa endapo watapenda kwenda kutembea kwenye maeneo hayo ya utalii,” alisema Waziri Kigangwala.

Ushawishi kwa Fifa

FIFA imekuwa ikitoa fedha kwa mashirikisho na vyama vya mpira wa miguu kwa nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kusaidia maendeleo ya mchezo wa soka hasa ukizingatiwa na ukweli kwamba uendeshaji wa mchezo wa soka umekuwa ni wa gharama kubwa.

Mara kwa mara fedha hizo hutolewa kwa ajili ya kuendeshea miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundominu ya soka, soka la ufukweni, vijana na wanawake sambamba na kuimarisha masuala ya utawala kwenye mpira wa miguu.

Kadri FIFA inavyopata ripoti chanya za utekelezaji wa miradi ambayo imekuwa ikitoa fedha zake, ndipo inaposhawishika zaidi kuipatia nchi husika fedha nyingine kwa haraka zaidi pindi inapoomba.

Kama FIFA itapata nafasi ya kuona kwa macho miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa kutokana na fedha zake, kuna uwezekano mkubwa ikawa fursa muhimu kwa Tanzania kunufaika zaidi na fedha kutoka Fifa.