Iliposhangaza makocha walipopishana ‘Airport’

Muktasari:

  • Msimu wa 2017/18, Simba iliuanza msimu chini ya Jackson Mayanja kabla ya kuletwa Mcameroon, Joseph Omog lakini Jackson Mayanja akabakia kuwa kocha msaidizi.

Alikuwepo kocha Dylan Kerr na Jackson Mayanja msimu wa 2015/16. Baada ya Kombe la Mapinduzi, Kerr akatimuliwa akabakia Jackson Mayanja hadi msimu wa 2016 ukamalizika.

Msimu wa 2017/18, Simba iliuanza msimu chini ya Jackson Mayanja kabla ya kuletwa Mcameroon, Joseph Omog lakini Jackson Mayanja akabakia kuwa kocha msaidizi.

Baada ya muda vuguvugu la kutimuliwa likaanza. Kila mmoja akashangaa, Jackson Mayanja akatema kibarua, ilikuwa Oktoba mwaka jana huku akidai anakwenda kuangalia familia Uganda, lakini papo hapo anapishana na Masoud Djuma aliyekuwa Rayon Sport Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Maswali yakawa mengi, imekuwaje, ina maana mipango ilishafanyika! Mayanja hakurudi na Simba ikawa chini ya Djuma.

Mara akaletwa Pierre Lechantre, Masoud akabakia msaidizi.

Kuja kwa Lechantre ni baada ya Simba kumfungishia virago kocha wao mkuu, Omog baada ya kuvuliwa rasmi taji la FA na Green Worriors.

Lakini kabla ya Lechantre kutua, mikoba ya Omog ilibebwa na Masoud ambaye aliibadili Simba na kutumia mfumo wa kisasa, mabeki wa kati watatu, viungo watano na mastraika wawili (3-5-2).

Hata baada ya Lechantre kufika, kikosi hicho hakikuwa na mabadiliko ya uchezaji kimfumo zaidi ya maboresho machache.

Mfumo huo umeifanya Simba kuwa na uwiano wa uchezaji kuanza nyuma hadi kwenye safu yao ya ushambuliaji na ndiyo iliyoipa ubingwa.