Jinsi wasanii wa kike wanavyoweza kutoboa

NYANGE

Muktasari:

  • Kwa mfano msanii wa kike anaweza kuwa amerokodi wimbo mzuri, lakini shida ikaja kwamba hana ‘connection’ ya kuweza kuifikisha kazi yake

Inafahamika kwamba miongoni mwa vikwazo vikubwa wanavyokumbana navyo wasanii wa kike hasa wanaochipukia ni kuombwa rushwa ikiwamo ya ngono ili waweze kusaidiwa katika jambo fulani linalokwamisha kufikia ndoto zao katika sanaa.

Kwa mfano msanii wa kike anaweza kuwa amerokodi wimbo mzuri, lakini shida ikaja kwamba hana ‘connection’ ya kuweza kuifikisha kazi yake kwenye vyombo vya habari,. Hapa sasa ndio unakuta anajitokeza mtu mmoja anayejifanya ni meneja, anatengeneza mazingira ya kumdanganya msanii kwamba atamsaidia  lakini kumbe lengo lake kuu huwa huwa tofauti kabisa na kazi.

Suala hili limeshawahi kutolewa ushahidi na wasanii wa kike wenyewe; akiwemo Dayna Nyange ambaye amethibitisha kwamba hata yeye alikutana na kasumba ya kuombwa ‘penzi’ ili asaidiwe jambo fulani kuhusu muziki wake.

Hata hivyo, hilo haliwezo kukwamisha ndoto, bado msanii wa kike ana nafasi kubwa ya kufanikiwa bila kutoa rushwa ya ngono endapo tu ataamua kufanya mambo haya muhimu.

Fuata kipaji chako

Iko hivi; kuna wasichana wanatamani kuwa waigizaji ilihali hawana kipaji. Watu wa aina hii wanapolazimisha kuingia kwenye tasnia hujikuta wanaangukia kwenye 18 za watu kama ‘waongozaji wa filamu’ ambao huwarubuni kwa kuwapa nafasi katika filamu zao lakini kwa lengo la kuwatumia kimwili tu.

Hivyo ili kuepuka kudhalilishwa namna hii ni vyema msichana kabla ya kuamua kuwa msanii, ukachagua sanaa ambayo una uhakika ni talanta yako.

Jitengenezee muonekano wa kuheshimika

Wasichana wengi hudhani kwamba kuvaa nusu uchi ndiyo usanii wenyewe, lakini laiti kama hilo lingekuwa na ukweli basi kuna baadhi ya wasanii hapa Tanzania wangekuwa wanamiliki tuzo hata ya Grammy.

Unapovaa hivyo unafanya watu wakuone huna maadili na hujiheshimu hivyo kutengeneza nafasi kwa ‘majangili’ kukutamani na kukudhalilisha.

Ni vyema msichana ukajijengea mwonekano wa heshima kwa kuvaa vizuri. Huna haja ya kuvaa viguo vya  ajabu kwa sababu usanii unaoufanya siyo wa kuonesha maungo ya mwili yako.

Jiwekee muda wa kutosha

Tatizo kubwa walilonalo wasanii wengi ni kupenda mafinikio ya haraka. Msanii anatoa wimbo leo jioni, anataka kesho asubuhi aamke akiwa ‘supa staa’, nyumba kubwa Madale, gari kali la gharama na huku akiuuza sura katika magazeti na televisheni zote.

Msanii wa kike mwenye utamaduni wa kupenda mafanikio ya ghafla namna hii huwa ni mwepesi sana kunaswa kwa ‘majangili’, kwa sababu ni rahisi kudanganyika.

Kushikana mikono wenyewe kwa wenyewe

Ikiwa wanaume wanatumia mwaya wa shida za wasanii wa kike kuwarubuni na kuwatumia, kwa nini wanawake wasiungane wakawa kitu kimoja?

Yaani badala ya msanii kuangukia kwenye mikono ya mtayarishaji tapeli, wakawa wanamsaidia hata kwa kumsogeza kwa  yule anayefahamu misingi ya kazi yake. Bila shaka hii ingesaidia kupunguza tatizo la rushwa ya ngono kwa wasanii wa kike.

Jitambue

Msanii wa kike hana tofauti na wasichana wengine wasio wasanii, hii ni sawa na kusema kwamba naye hutongozwa kama ambavyo wanawake wote hutongozwa.

Hata majangili wanaowaomba rushwa ya ngono wasanii kike si kwamba hutumuia nguvu, bali maneno matamu na ahadi nyingi kama ambavyo hufanya kwa wanawake wengine.

Jambo pekee linaloweza kumsaidia msanii wa kike kukwepa kutoa rushwa ya ngono ni kujitambua yeye ni nani na ana malengo gani?

Ajitambue kuwa yeye ni mwanamke hivyo hawezi kuwazuia wanaume kumtongoza isipokuwa tu ana uwezo wa kufanya uamuzi sahihi na hili linaweza kumpa nguvu ya kusema ‘hapana’ pale panapostahili kwa kudhumuni la kuokoa ndoto na malengo yake.

Jiamini

Kujiamini ndiyo nguzo mama wa mafanikio unayoyaona kwa mtu yeyote yule. Unapojiamini unakuwa siyo mtu wa kuyumbishwa na vitu visivyo na msingi.

Msanii  wa kike anayetaka ‘kutusua’ kwenye ‘muziki bila kutoa mwili wake  kama dhamana ya kupewa msaada fulani ni lazima ajiamini na aamini kwamba mafanikio hayaji kwa kupewa msaada na mtu fulani bali ni kipaji na uwezo mkubwa wa kufanya  kile anachotaka kukifanya. Unapojiamini kwa kiasi hiki ni kwamba huwezi ukajirahisisha kwa director kwa  kumpa  ‘uroda’ ilihali tu upate nafasi ya kucheza kwenye filamu yake.