Jinsi ya kulea vifaranga bandani

Picha zinaonyesha umuhimu wa banda la vifranga wa kuku kuwa na vifaa kama taa au majiko yanayoweza kutoa hali ya ujoto kwa vifaranga. Picha zote na mitandao

Muktasari:

  • Hatua hii ya ufugaji ambayo ni ya awali kabisa ilijumuisha muhtasari wa ufugaji, ujenzi wa mabanda, koo na aina za kuku, kiasi cha mtaji na namna ya kutotolesha kwa haraka imechukua wiki 13.
  • Tukiwa kwenye wiki ya 14, ambayo ni sawa na miezi mitatu na wiki mbili, ninayo furaha ya kuendelea kupata nafasi ya kuwaelemisha Watanzania wenzangu kupitia kijarida cha Mbegu ya Dhahabu.

Wiki iliyopita nilihitimisha hatua ya kwanza ya uanzishaji wa kufuga kuku wa asili na wale wa kisasa, kibiashara.

Hatua hii ya ufugaji ambayo ni ya awali kabisa ilijumuisha muhtasari wa ufugaji, ujenzi wa mabanda, koo na aina za kuku, kiasi cha mtaji na namna ya kutotolesha kwa haraka imechukua wiki 13.

Tukiwa kwenye wiki ya 14, ambayo ni sawa na miezi mitatu na wiki mbili, ninayo furaha ya kuendelea kupata nafasi ya kuwaelemisha Watanzania wenzangu kupitia kijarida cha Mbegu ya Dhahabu.

Katika wiki hizo 13 safu hii imeweza kutoa mchango wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja kwa wasomaji wake kimawazo na kimatendo.

Hatua hiyo inanipa nguvu ya kueleza wazi kuwa wapo wasomaji wengi waliofaidika na makala hizi, wengine wameweza kunialika kwenye maeneo yao ili angalau nikatoe ushauri au hata kuelekeza ikibidi.

Bila kusita nimekuwa nikifanya hivyo bila hiyana. Hatua hii ya kufanikisha dhamira ya kusaidiana na Watanzania wenzangu imenifariji na kunipa morali wa kuhakikisha naendelea kuutumia ujuzi na uzoefu nilionao kwenye ujasiriamali kusaidiana nao.

Baada ya utangulizi huo, sasa tujielekeze moja kwa moja kwenye hatua ya pili ya ufugaji wa kuku wa asili na wale wa kisasa kibiashara.

Ulezi wa vifaranga wa kuku wa asili

Baada ya kufanikiwa kuingiza viranga bandani, hatua inayofuata ni kuwalea ili watuletee tija tunayoihitaji.

Kumbuka, kuwa na vifaranga hakukupi jeuri ya moja kwa moja ya kufikia malengo. Ili uwe na jeuri hiyo ni lazima uwalee kwa ustadi wa hali ya juu ili wafikie kiwango stahiki cha kuwaingiza sokoni.

Ukweli ulivyo ni kwamba jukumu la kulea vifaranga hufanywa na kuku mtetea ambaye ndiye mmiliki halali wa mayai.

Hata hivyo, ili kuhakikisha kuku mtetea anaendelea kufanya kazi ya kutaga bila kikomo, ipo namna ya kumsaidia kuvilea.

Lakini pia uleaji wa vifaranga unawahusu hata wale vifaranga waliototoleshwa na mashine maalum za utotoleshaji (Incubator).

Kutokana na uamuzi huo wa mfugaji kulea vifaranga. Upo ulazima wa mfugaji kuhakikisha anatekeleza vitu vya muhimu na lazima kwa vifaranga ili kuwaepusha na vifo.

Kumbuka vifaranga husumbuliwa sana na hali mbaya ya hewa, magonjwa mbalimbali, kukosa chakula kisichofaa na kukosa uangalizi wa karibu.

Ni lazima vifaranga waangaliwe kwa kuwapatia nyumba yenye joto, chakula kinachofaa, maji safi, kuwakinga dhidi ya magonjwa nyemelezi kwenye eneo husika na kuwapa chanjo mara kwa mara.

Mfugaji wa kuku kibiashara ni yule mwenye utayari wa kuwalea vifaranga kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu. Mtu anayeacha vifaranga vijitafutie, huyo anaishi na kuku.

Ili ujihakikishie kupata faida, unapaswa kufuga vifaranga wenye afya nzuri ambao hatima yake ni kutoa mazao mengi, pale wanapokuja kuanza uzalishaji.

Idadi kubwa ya wafugaji hasa wale wa kuku wa asili huwaacha kuku walee wenyewe vifaranga wao, njia hii humchelewesha kuku kurudia kutaga hali inayosababisha kupata vifaranga wachache zaidi kwa mwaka.

Lakini vifaranga vikiondolewa kwa kuku mapema, upo uwezekano wa kuku kutaga tena ndani ya kati ya wiki tatu hadi tano hali inayoweza kuongeza idadi ya kuku. Njia hii ya kumpokonya kuku vifaranga wake husaidia kuongeza wingi wa kuku kwa mfugaji, ingawa njia ya utotoleshaji huongeza tija zaidi.

Ukubwa wa kiota

Mara nyingi vifaranga havihitaji eneo kubwa katika muda wa wiki nne za kwanza. Nafasi inayohitajiwa kwa kukadiria ni mita moja ya eneo kwa kila vifaranga 16.

Hii inamaanisha kiota chenye mita za mraba 10 kina uwezo wa kubeba vifaranga 160 vyenye umri wa siku moja hadi wiki nne.

Vipimo vya nyumba yenye eneo kama hili inaweza kuwa na hatua tano kwa hatua nne au hatua tatu kwa 3.25. Utajenga kulingana na eneo ulilonalo.

Baada ya wiki nne wa umri wa vifaranga unaweza kuwaongezea nafasi ili wapate eneo la kutosha.

Sakafu nzuri katika nyumba ya vifaranga inapaswa kuwa ya mbao au saruji. Lakini pia inashauriwa kuweka maranda, pumba au makaratasi ili kuwaepusha vifaranga na baridi inayotoka chini.

Itaendelea, 0789063838-Barua pepe [email protected]