KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kufikiri hakuombewi ruhusa

Muktasari:

Sasa Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais John Magufuli amesema wanaoripoti au kujadili sakata la makontena ya mchanga wa madini linaloendelea, wasihusishe marais wawili waliopita – Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Kuna mahali ambapo hapahitaji ubishi. Kuanzisha, kukoleza na kuendeleza ubishi ni kutafuta kuulizwa, “Kwani huyu vipi? Haelewi au ana lake jambo?” Si ndivyo huwa tunaulizana mitaani?

Sasa Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe amesema Rais John Magufuli amesema wanaoripoti au kujadili sakata la makontena ya mchanga wa madini linaloendelea, wasihusishe marais wawili waliopita – Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Ni kweli. Rais aliishasema hayo na kwamba hata ripoti mbili za aliowatuma kuchunguza sakata hilo hazikutaja yeyote kati yao. Aidha, Rais amerejea kusema kuwa atawalinda marais wote waliotangulia.

Ukitaka kuweka hili katika lugha nyepesi, basi zungumza kama alivyokuwa akisema Rais mstaafu Kikwete: “Ee bwana ee! Achana nao hao; wamemaliza ngwe yao na Katiba ya leo inawalinda.” Basi!

Anachosema Rais kinaeleweka. Atawalinda marais waliotangulia, kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Hatabadili Katiba kwa lengo la kuwasakama. Atazuia tendo lolote linaloweza kukiuka Katiba aliyoapa kuilinda na linalohusiana na marais watangulizi.

Kwa ufupi, Rais atazuia yeyote kutenda kile kinachozuiwa na Katiba ya nchi. Hayo siyo tu maoni yake, ni jukumu na ahadi yake. Na vyote vinaimarisha kiapo chake cha kulinda Katiba. Asiyekubaliana na hilo anyooshe mkono juu! Hayupo. Tuendelee.

Katika mazingira ya kawaida, nani alitarajia Rais aseme tofauti au atumie lugha ya kupindapinda katika hili linalohusu waliomtangulia?

Lakini katika kauli, ahadi na jukumu la Rais, hakuna popote ambako inaelekezwa au anaelekeza yeye kuwa, watu wasifikiri au wasiwe na maoni. Vilevile, hakuna sehemu anaelekeza kuwa watu wasiwe na maoni tofauti.

Hii ni kwa sababu anajua kuwa, hata angependa iwe hivyo, kuwe na maoni sawa, yanayolingana, yasiyopingana au kupishana, hakika haitawezekana aslani.

Kama mahakama isivyopaswa kutoa hukumu ambayo haitekelezeki, ndivyo taasisi ya urais isivyostahili kutoa amri ambazo haziwezi kutekelezeka kwa mujibu wa Sheria na Katiba.

Kufikiri basi, hakuombewi ruhusa wala hakubembelezwi. Ushawishi wenye nguvu ya kupinda maoni na utashi wa mtu au watu wengine, sharti basi uwe umebeba zana zote za ukweli na usahihi usiotiliwa shaka.

Hii ndiyo maana hata baada ya Rais kusema kuwa watafiti wake hawakuwataja marais wastaafu mahali popote katika sakata la mchanga wa madini; bado kuna wanaoendelea kufikiri na kufikiri tofauti na kile ambacho Rais amesema.

Mmoja wa wasomaji wa gazeti hili ameniuliza: “Mhariri unazo hadidu za rejea za Rais kwa kamati zake mbili?” Nilijibu: Sina. Labda niulizie.

Hapo zamani za kale kulikuwa na mwanasheria mkuu nchini Kenya. Walimwita Charles Njonjo. Hawezi kusahaulika kwa kauli yake kuwa katili ni “mhaini”. Kwa mwana-Kenya yeyote hakuwaza hata kimyakimya kitandani kwake, kuhusu kifo cha rais.

Nchi hii haijafikia “nyakati za Njonjo’’ Kwahiyo, kufikiri hakuombewi ruhusa. Hata Njonjo alijua kuwa mtu anaposema usifikiri hiki; ndipo hasa unapoanzia kufikiri hichohicho au kingine. Bali Rais naye hajazuia watu kufikiri; ni kwa kuwa hawezi kufaulu katika hilo na hiyo siyo kazi ya mtu waliyemchagua kuwaongoza.

Bali watu wakiishafikiri hutamani, na hii ni tabia yao, kupeana maoni na taarifa kwa wawiliwawili kwa njia ya mdomo kwa mdomo, makundi na wenye vyombo vya kusambazia taarifa kufikia walio mbali kwa sauti na picha.

Siyo ajabu basi, hata baada ya Rais kusema marais wawili hawajatajwa katika ripoti zake; mijadala shuleni, vyuoni, katika mabasi, mabaa na vijiweni ndio imepamba moto ikiwataja walewale ambao “hawamo katika ripoti.”

Rais anapokomea ndipo wengi wanaanzia kufikiri. Hili halizuiliki. Bali mijadala haihukumu. Inataja waliokuwepo na wao wanajua walikuwapo na wanaweza kuwa wa msaada kwa Rais Magufuli na hata kuwezesha kuleta maridhiano na kuanza ukurasa mpya.

Hapa ndipo anaingia Waziri wa Habari, Dk Mwakyembe ambaye ameonyesha wepesi wa kuchukua hatua ya kulifungia gazeti. Tayari ameona nani “amekaidi” au amekwenda “kinyume cha maoni ya Rais.

Hapa ndipo wameingia wahariri na waandishi wengine wa habari; viongozi wa asasi za haki za binadamu; marafiki wa vyombo vya habari na wapigania uhuru wa maoni na uhuru wa kujieleza.

Katika mazingira haya, kuzuia maoni kutoka, yawe matamu au machungu, kutaonyesha kuwa kila anayetajwa amehukumiwa. Kumbe bado hajawa hata mtuhumiwa. Na hilo siyo sahihi.

Ni ushauri wangu.

Mwandishi ni Mhariri wa Jamii wa vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti na hili. Kwa maswali na hoja juu ya vyombo hivyo, wasiliana naye kwa simu: 0713614872 au 0763670229; e-mail: [email protected] au [email protected]