Kabla ya kuifikia Tanzania ya viwanda tumalize Umasikini

Muktasari:

Hadi sasa Serikali hiyo inayoongozwa na Rais, John Magufuli imeshuhudiwa ikichukua hatua kadhaa kuhakikisha inafikia malengo hayo ya kukifanya kipato cha kila Mtanzania kiwe walau Dola 3,000 za Marekani kwa mwaka.

Miongoni mwa mambo ambayo Serikali ya awamu ya tano imeahidi kuyafanyia kazi ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025. Hilo litafanyika kwa kukuza pato la mwananchi (per capita income) na la taifa (GDP)

Hadi sasa Serikali hiyo inayoongozwa na Rais, John Magufuli imeshuhudiwa ikichukua hatua kadhaa kuhakikisha inafikia malengo hayo ya kukifanya kipato cha kila Mtanzania kiwe walau Dola 3,000 za Marekani kwa mwaka.

Kama waswahili wasemavyo, nyota njema huonekana asubuhi huenda ikawa hivyo kwa Tanzania kwani ripoti ya Shirika la Fedha la Duniani (IMF) iliyotazama masuala kadhaa ya kiuchumi na kutolewa Mei, imeonyesha dalili nzuri katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Tanzania inatarajiwa kusajili kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa uchumi wake mwaka huu katika kanda ya Afrika Mashariki na kati. Ukuaji wa asilimia saba mwaka 2016 hivvyo kuwa ya pili kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, nyuma ya Ivory Coast itakayokua kwa asilimia 8.5.

Kwa Afrika Mashariki, taarifa hiyo inaeleza kwamba uchumi wa Kenya ndiyo wa pili kwa kasi ya ukuaji. Hata hivyo, Tanzania bado ina kazi kubwa ya kufanya siyo kwa kukuza uchumi wake pekee bali hata kwa kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Moja ya juhudi hizo ni kuhakikisha inaondokana na umasikini kwa kundi kubwa la watoto nchini. Taifa la kesho litakaloshikilia uchumi huo unaojengwa kuanzia sasa.

Umasikini huo umebainishwa na ripoti ya hali ya umasikini kwa watoto iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa kuzingatia viashiria katika elimu, malazi, afya, maji, lishe na ulinzi kutathmini hali ya umasikini kwa kundi hilo. Imeonyesha, asilimia 74 ya watoto wenye umri chini ya miaka 17 ni maskini. Wanaishi kwenye umasikini.

Ripoti hiyo ilizinduliwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji Agosti 11, na kuonyesha takribani Watanzania milioni 25 ni masikini.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wadau wa uchumi na maendeleo wameeleza namna Tanzania inavyoweza kujiepusha na kizazi masikini kwa miaka ijayo na kubainisha kwamba ni lazima kundi hilo lipatiwe ufumbuzi.

 

Maoni ya wadau

Akielezea mchango wake katika kuondoa tatizo hilo Emilian Kalugendo kutoka NBS, anasema ni vyema zikatungwa sera zitakazotoa miongozo ya kuwasaidia watoto moja kwa moja kuliko kutoa pesa kwa familia masikini.

Kalugendo anasema wakati mwingine inakuwa vigumu msaada kuwafikia watoto endapo utapitia kwa wazazi, lakini kukiwa na sera hali itakuwa tofauti. Kauli hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri wa chuo cha takwimu Afrika Mashariki, (EASTC) Dk Camilius Kasala ambaye anasema Serikali inatakiwa kuongeza ruzuku kwa kaya maskini.

Dk Kasala anasema kiasi kinachotolewa sasa hakikidhi mahitaji ya familia hizo.

“…mipango bila takwimu, umaskini ndiyo hukumu,” anasema Dk Kasala.

Mkuu wa Elimu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Cecilia Baldeh anasema kundi hilo ambalo ni asilimia 50 ya Watanzania wote lisipofanyiwa kazi hakuna namna Tanzania inaweza kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Baldeh anasema lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iangalie jinsi itakavyowekeza kwenye kundi hilo. “Watoto wasiachwe nyuma katika mipango na mikakati ya kupunguza umasikini. Lazima tuwekeze kwa watoto sasa na kuhakikisha tunakidhi mahitaji yao muhimu,” anasema.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Yutaka Yoshino anasema kuwa matokeo hayo yanatoa angalizo kwa Tanzania kuchukua hatua sasa kwa sababu ni kiashiria cha kuwa na kizazi kijacho masikini.

Yoshino anasema endapo hatua hazitachukuliwa mapema, watoto watashindwa kujikwamua kiuchumi watakapokuwa wakubwa kwa sababu kwa kukosa msingi imara.

Mkuu wa Uhusiano wa EU, Eric Beaume anasema kundi hilo linahitaji kusaidiwa na kwa kutambua mchango wa takwimu kwenye masuala mbalimbali, umoja huo umetoa msaada wa Sh25.1 bilioni kuisaidia NBS kutekeleza majukumu yake.

Dk Kijaji anasema ripoti hiyo inatoa fursa kwa wazazi na walezi kuitumia vyema sera ya elimu bure ili kuhakikisha watoto wanapata maarifa yatakayowajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa anasema ofisi yake itaendelea kufanya kazi nzuri ili kuhakikisha Serikali inapata takwimu zitakazoiwezesha kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

 

Kuhusu ripoti

Utafiti huo ulijikita kwenye upatikanaji wa elimu, afya, maji, malazi, ulinzi, lishe na upatikanaji wa taarifa kuanzia mtoto anapozaliwa mpaka anapofikisha umri wa miaka 17.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Karugendo anasema, kupitia viashiria hivyo walihojia jinsi mama alivyojifungua mtoto; hospitali au nyumbani, lishe ya mtoto kwa maana ya idadi ya milo anayopewa kwa siku, kama ni miwili au mitatu, malazi na hapo ndipo walipobaini kuwa kundi hili liko kwenye umaskini kutokana na malezi hayo.

Pia maji wanatumia na umbali unaotumiwa kupata maji hayo. Karugendo anasema viashiria hivyo viliwawezesha kupata matokeo hayo ambayo yanaonyesha kundi kubwa la watoto nchini ni masikini.

Hata hivyo anasema baadhi ya watoto hao wanatoka kwenye kaya zenye uwezo kimapato na kwamba umaskini wao ni ule utokanao na kukosa mahitaji muhimu kama elimu, afya na lishe.