MAONI YA MHARIRI: Kamanda Sirro waandishi ni muhimu

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro

Muktasari:

Ni tabia ya kuahirisha majibu kwa waandishi wa habari pale wanapotaka kufahamu jambo fulani. Kimsingi tabia hiyo haikubaliki ndani ya vyombo vya habari kwa kuwa inakwaza utendaji wa kazi na inawanyima Watanzania haki ya kupata habari.

Hivi karibuni kumekuwa na tabia inayokwaza utendaji wenye weledi kwa vyombo vya habari inayofanywa na baadhi ya wasemaji serikalini, hasa kwenye taasisi zake kama Jeshi la Polisi.

Ni tabia ya kuahirisha majibu kwa waandishi wa habari pale wanapotaka kufahamu jambo fulani. Kimsingi tabia hiyo haikubaliki ndani ya vyombo vya habari kwa kuwa inakwaza utendaji wa kazi na inawanyima Watanzania haki ya kupata habari.

Tunaamini Serikali nayo haipendi tabia hiyo na ndiyo maana ukiisoma Sera ya Habari na Utangazaji, kuna kipengele kimetamka kuwa sekta ya habari inatoa huduma ambayo ni haki ya msingi ya raia kama inavyotamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 18 ya Katiba.

Ukiisoma kwa umakini sera hiyo kuna sehemu inatamka kuwa lengo lake ni kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa habari serikalini na taasisi zake.

Pia, maelezo ya sera yanakazia kuwa Serikali iondoe vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa habari za manufaa kwa wananchi.

Lakini, pamoja na juhudi za Serikali za kuweka sheria na sera ya kuviongoza vyombo vya habari, baadhi ya wasemaji waliowekwa kwenye idara na taasisi wamekuwa kikwazo cha utendaji wenye weledi kwa wana habari nchini.

Tunasema haya kwa kumtolea mfano Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro ambaye tangu ameshika wadhifa huo amekuwa na ushirikiano unaotia shaka na vyombo vya habari.

Hatuna nia ya kumfundisha Kamanda Sirro namna ya kutekeleza majukumu yake ya kazi, lakini afahamu kwamba Jeshi la Polisi analolitumikia linagusa maisha ya kila siku ya wananchi ndiyo maana wanafanya kazi kwa saa 24.

Kamanda Sirro amekuwa akiahirisha mambo yanayoweza kupata majawabu ndani ya dakika mbili, mfano alipokamatwa Masogange waandishi walimpigia simu kumuuliza kama ni kweli, jibu alilotoa nitaongea kesho lakini siku hiyo ikifika haongei.

Hata jana alipoulizwa kuhusu suala la Mbunge Freeman Mbowe alisema ataongea kesho (kwa maana ya leo), kuna wakati aliwahi kutamka kwamba amejiwekea utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari kila Jumatatu.

Lakini, tatizo letu kwa Kamanda Sirro ni kutotimiza ahadi maana ya kuongea kesho huwa hatimizi na hata hiyo Jumatatu imekuwa ni shida na hatoi maelezo ya kwanini hatimizi.

Tunaamini Kamanda Sirro kwa utaalamu alionao ndani ya Jeshi la Polisi, anaelewa umuhimu wa nafasi yake, hivyo kushindwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari wakati ni miongoni mwa kazi zake, ajue anakwamisha utendaji kazi wa taasisi nyingine.

Ni ukweli kwamba Jeshi la Polisi na vyombo vya habari wanategemeana katika utendaji kazi, hivyo si vema kwa upande mmoja kujiona ni muhimu kuliko mwenzake.

Tunamshauri Kamanda Sirro na makamanda wengine wenye tabia kama yake, wafahamu bila waandishi wa habari na wao kazi itakuwa ngumu, ndiyo maana wana watu wanaoitwa wasemaji wa Polisi.

Kamanda Sirro bado tunakuamini katika utendaji wako wa kazi, badilika pale panapohitaji, dunia imebadilika watu wanataka kufahamishwa na hasa mambo ambayo hayaingilii upelelezi wa polisi.