Kibarua cha wabunge wa Tanzania Bunge la nne Eala

Wabunge wa Tanzania waliomaliza muda wao katika Bunge la Afrika Mashariki. Waliochaguliwa karibuni wana kibarua kigumu katika Bunge hilo. Picha na Philbert Rweyemamu

Muktasari:

Kumalizika kwa Bunge hilo la tatu, kunafungua mlango kwa Bunge la nne kuendelea, ingawa nalo litalazimika kuchelewa kuanza kutokana na vikwazo kadhaa vya kisiasa katika nchi wanachama.

Bunge la Afrika Mashariki (Eala), ambalo ni moja ya mihimili mitatu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mapema mwezi huu lilimaliza muda wake na kupitisha bajeti yake ya mwaka 2017/18.

Kumalizika kwa Bunge hilo la tatu, kunafungua mlango kwa Bunge la nne kuendelea, ingawa nalo litalazimika kuchelewa kuanza kutokana na vikwazo kadhaa vya kisiasa katika nchi wanachama.

Mojawapo ya vikwazo ni kutokamilika kwa uchaguzi wa wabunge wa Eala nchini Kenya kutokana na vikwazo kadhaa, kikiwemo cha kusubiri uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge utakaofanyika mwezi Agosti. Wabunge wa sasa wameshindwa kujumuika kufanya uchaguzi huo, na hivyo kuwepo uwezekano wa kusubiri kukamilika uchaguzi mkuu Agosti 8.

Kikwazo kingine ni kuwapo kwa kesi iliyofunguliwa na raia wa Sudan Kusini kupinga utaratibu uliotumika kuwapata wabunge wa Eala kulingana na mkataba wa EAC.

Kutokana na itifaki ya mkataba huo, kila nchi ilitakiwa kuchagua wabunge tisa na kufanya Bunge hilo kuwa na wajumbe 27 wa kuchaguliwa. Pia waliongezeka wabunge wanaoingia kwa nyadhifa zao (ex-officio) ambao ni waziri au naibu waziri anayehusika na Jumuiya ya Afrika kutoka kila nchi mwanachama.

Wengine wanaotakiwa kuingia, kwa mujibu wa mkataba, ni katibu mkuu wa EAC na Mwanasheria Mkuu wa EAC ambao hufanywa jumla ya wajumbe 52.

Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya nchi, wabunge hao wamekuwa wakiongezeka na Bunge lijalo litakuwa na wajumbe 62.

Awali, mkataba ulioanzisha Eala ulihusisha nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kabla ya mwaka 2007 wakati Rwanda na Burundi zilipojiunga na kuwafanya idadi ya wanachama kuwa watano na baadaye Sudan Kusini ikakubaliwa kuwa mwanachama 2016.

Majukumu ya Eala

Ibara ya 49 ya mkataba wa EAC inataja majukumu ya Bunge la Eala kuwa ni kushirikiana na mabunge ya nchi wanachama katika mambo yanayohusu jumuiya kujadili na kuthibitisha Bajeti ya Jumuiya.

Majukumu mengine ni kupitia na kujadili ripoti mbalimbali zinazohusu jumuiya, kujadili taarifa za mahesabu yaliyokaguliwa na mambo yote ya msingi ya Jumuiya na kutoa mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri kadiri itakavyoonekana inafaa kulingana na mkataba wa EAC.

Pia Bunge la Afrika Mashariki limepewa mamlaka ya kuunda kamati mbalimbali kadiri itakavyoonekana inafaa.

Kwa sasa zipo kamati tano zinazohusika na mambo mbalimbali ikiwemo Kamisheni, Kamati ya Hesabu, Kamati ya sheria na Kanuni na madaraka ya Bunge.  

       Kamati zingine ni ya Kilimo, Utalii na Maliasili, Kamati ya inayoshughulikia Kanda na utatuzi wa migogoro, Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji na Kamati ya Shughuli za Kawaida.

Majukumu ya kamati hizo ni kufanya kazi ya uangalizi wa utekelezaji wa mkataba ulioanzisha EAC na utekelezaji wa mkakati wa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa katika maeneo yanayohusu ushirikiano wa jumuiya na kutekeleza majukumu mengi ya Bunge.

Pamoja na shughuli hizo, kazi kubwa ya Bunge hilo ni kutunga sheria, kupitisha miswada mbalimbali, kufanya kazi ya usimamizi au uangalizi wa mihimili mingine ya EAC na kuwawakilisha wananchi wa eneo la jumuiya ili kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na mtangamano wa kisiasa.

Bunge la tatu

Bunge la tatu lilimaliza muda wake hivi karibuni likiwa limefanikiwa katika maeneo mbalimbali hasa kujadili na kupitisha miswada mingi ya sheria za jumuiya, ukilinganisha na awamu zilizotangulia.

Hata hivyo, Bunge hilo pia lilikutana na changamoto kubwa ya kumwondoa aliyekuwa Spika wake, Margaret Zziwa Desemba 2014, jambo lililochukua muda mrefu kufanya shughuli zake.

Kabla ya kumng’oa spika hiyo vikao vingi havikufanyika kwa ufanisi kutokana na malumbano.

Mbali na hilo, katika kutekeleza wajibu wake, kamati za Bunge hilo zilifanya ziara za kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi wanachama ili kukagua miradi inayotekelezwa na kuangalia ufanisi wake.

Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa kuona namna nchi wanachama zinavyoweza kushawishi mizigo kuondolewa haraka ili kurahisisha ufanyikaji wa biashara katika EAC.

Pia Bunge la tatu lilikutana na wananchi wa kawaida na kufanya nao mazungumzo kuhusu fursa zinazopatikana katika nchi wanachama hasa katika utekelezaji wa Itifaki ya Ushuru wa Forodha na ile ya Soko la Pamoja.

Mbunge aliyemaliza muda wake kutoka Tanzania, Shyrose Bhanji pamoja na mambo mengine alipigania na kufanikiwa Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi zinazopaswa kutumika katika mawasiliano rasmi.

Kutokana na muswada wake binafsi kupita, kwa mara ya kwanza Tume ya Kiswahili ya EAC ambayo ina makao yake Zanzibar imetengewa Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh3.1 bilioni).

Bhanji anasema lugha hiyo itasaidia kuwafanya wananchi wengi katika nchi za EAC kuwasiliana na kutangama na hivyo kufanikisha lengo la jumuiya la kuifanya kuwa ya wananchi badala ya kuwa ya viongozi zaidi.

Wabunge wapya

Miezi miwili iliyopita, Tanzania kupitia Bunge lake iliwachagua wabunge wapya wa Afrika Mashariki ambao wataiwakilisha nchi katika Eala. Ni matarajio ya wananchi kuwa wabunge hao wataisaidia nchi kusukuma ajenda zake kwenye Jumuiya na hatimaye kuisukuma EAC mbele kimaendeleo.

Licha ya upya wa wabunge saba kati ya tisa baada ya wawili tu – Adam Kimbisa na Maryam Ussi, kuingia kipindi cha pili, matarajio ya nchi kwa wabunge hao ni makubwa, ukiacha siasa za vyama zilizozingira uchaguzi wao mjini Dodoma.

Katika Bunge la nne wabunge wapya wa Tanzania ni Happiness Lugiko, Fancy Nkuhi, Abdullah Makame, Habib Mnyaa, Dk Ngwaru Maghembe, Josephine Lamoyan na Pamela Maasay.

Wabunge hao pamoja na mambo mengine, watapaswa kuwa mabalozi wazuri wa lugha ya Kiswahili jambo litakalofungua fursa kwa kurahisisha mawasiliano kibiashara na kusaidia walimu wa somo hilo kupata ajira katika nchi wanachama kulingana na Itifaki ya Soko la Pamoja ambayo tayari imesainiwa.

Wakati wabunge hao wanakabidhiana vijiti, mbunge aliyemaliza vipindi viwili katika bunge la Eala, Abdullah Mwinyi anawataka wabunge wapya wa Bunge la nne kuonyesha uwezo wao wa kusimia Sekretariati ya EAC na taasisi zake kikamilifu.

“Ni wajibu ambao wabunge wa Bunge lijalo wanatakiwa waufanye kwa nguvu zote. Naamini Tanzania ina wabunge makini wakishirikiana na wengine katika nchi wanachama, walinde na kutetea maslahi mapana ya jumuiya,” anasema Mwinyi.

Mwinyi ambaye katika Bunge lilipopita kwa nyakati tofauti amekuwa mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kikanda na utatuzi wa migogoro, anasema wabunge hao wana jukumu la kuhakikisha fedha za jumuiya zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Katika siku za hivi karibuni Bunge hilo limekuwa likiibua matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na Sekretariati ya EAC na taasisi zake, wakidai kuwa hali hiyo inakwamisha wahisani kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo na wakati mwingine kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi wa Jumuiya.

Tanzania ikiwa ni nchi kubwa kwa eneo na kuwa na idadi kubwa ya watu, wabunge wake wanatakiwa kuonesha uwezo wa kujenga hoja zenye mashiko ya kutetea misimamo ya Serikali katika EAC inayolenga kulinda maslahi mapana ya nchi na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.

Wabunge hao pamoja na mambo mengine wanapaswa kuwa na muono mpana na kufikiri nje ya vyama vyao vya siasa vilivyowapa nafasi, kufikiri namna ya kuipa nchi hadhi kwa kuonesha nia njema na michango yenye manufaa kwenye kamati watakazochaguliwa, bungeni kwenye vikao na nje ya Bunge.

Kwa mantiki hiyo, wanatakiwa waonyeshe uwezo wa kuwasilisha hoja zenye mtazamo chanya na ushawishi kwa makundi mbalimbali ya kitaaluma na kibiashara waweze kuvuka mipaka kwenda nchi wanachama kufanya biashara na kutafuta ajira.

Fursa kwa Tanzania

Kutokana na hali ya kutokuwapo uhakika wa chakula katika nchi nyingi zinazoizunguka Tanzania, wabunge hao wanatakiwa kuona fursa hiyo na kuhamasisha viongozi na wananchi kunufaika kiuchumi kupitia jumuiya hii kwa kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko kubwa la EAC.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mazao jijini Arusha, Philemon Mollel anawashauri wabunge wachagize taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja na Ushuru wa forodha nchini ziwatendee haki Watanzania.

“Hii ni fursa nzuri ambayo inatoa nafasi kwa wafanyabishara kuitumia EAC kama soko kubwa lakini kwa upande wa Serikali yetu kumekuwa na changamoto za vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje kuchukua muda mrefu hadi wiki mbili, wakati kwa nchi jirani vinachukua saa chache tu, tunatakiwa kubadilika sana,” anasema

Anashauri mfumo mzima uwaunge mkono wabunge wa bunge la nne kutekeleza wajibu wao katika kuhakikisha Tanzania haiwi msindikizaji katika EAC bali mnufaikaji.