KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kinachoweza kuua uandishi wa habari

Muktasari:

Hapa sitajihusisha na eneo la sarufi kuanzia kwenye kichwa ambako ninaogopa kuibua mzozo juu ya mtu mmoja “kunyonyana… ndimi;” bali nitajielekeza kwenye ujumbe katika taarifa – ukweli, usahihi na matakwa ya taaluma.

Ijumaa iliyopita gazeti hili lilibeba taarifa (uk. 6), iliyopewa kichwa kisemacho “Anyofolewa ulimi akinyonyana ndimi.”

Hapa sitajihusisha na eneo la sarufi kuanzia kwenye kichwa ambako ninaogopa kuibua mzozo juu ya mtu mmoja “kunyonyana… ndimi;” bali nitajielekeza kwenye ujumbe katika taarifa – ukweli, usahihi na matakwa ya taaluma.

Kichwa cha taarifa kinasema: “Anyofolewa ulimi;” aya ya kwanza ya taarifa hiyohiyo inasema ulimi upo lakini umeng’atwa “theluthi tatu.” Hapa ujumbe sahihi ni upi?

Katika mtiririko wa taarifa hii ya aya nane, tunasoma kuwa kuna daktari wa hospitali ya Mkoa wa Singida. Anatajwa na mwandishi kuwa ni daktari wa meno.

Meno na ulimi ni zana za binadamu zilizo katika mdomo. Kila kimoja kina kazi zake. Zinakaa katika ghala liitwalo kinywa. Wataalamu wanaoshughulikia eneo hilo huitwa madaktari au wataalamu au mabingwa wa kinywa.

Mtu aking’atwa ulimi na mwandishi akaandika kuwa mng’atwa ameonwa na “daktari wa meno,” – kama ilivyoripotiwa; msomaji mwenye uelewa wa kawaida haoni haraka uhusiano wa meno na ulimi.

Bali mwandishi akiwa mbele ya daktari, aweza kumuuliza ni daktari, bingwa au mtaalamu katika eneo lipi. Maelezo hayo yaweza, tena kwa ufupi, kuondoa ukungu – kwa upande wa mwandishi na msomaji – juu ya aliyetoa huduma kwa mng’atwa.

Katika andishi hili mwandishi “anaripoti” kuwa mng’atwa hawezi kuongea. Msomaji anajiuliza: Je, ni kwa kuwa anaumwa? Ni taabani? Ni kwa kuwa moja ya zana zake imekatwa?

Haya ni maswali yanayotokana na mwandishi kutomhoji daktari juu ya hali hiyo. Anaandika anavyotaka. Anavyofikiri. Kumbuka yeye siyo mtaalamu katika eneo hili.

Mwandishi anaandika kuwa Said Mamba (mng’atwa), amelazwa hospitalini baada ya kung’atwa theluthi tatu za ulimi wake…”

Haelezi kawaida ulimi wa mtu una urefu gani. Haelezi chanzo chake cha kitaaluma kilichompa vipimo vya ulimi wote, uliong’atwa na uliosalia.

Lakini taarifa inaeleza kuwa yupo karibu na daktari. Mwandishi angemuuliza maswali hayo. Hakumuuliza. Wasomaji wamebaki na maswali vifuani. Bila majibu. Bila taarifa. Bila uelewa.

Mwandishi anamnukuu daktari akisema ulimi “hauwezi kutibika.” Hamuulizi kwa nini. Lakini baadaye anaandika kuwa daktari anasema anaweza kuusafisha ili “usipate maabukizi.” Hapa kuna maswali lakini mwandishi hakumuliza daktari. Kwa mfano: Kwa nini daktari anasema ulimi hauwezi kutibika? Ni maambukizi gani mng’atwa anaweza kupata kinywani? Kwani kuosha na kukausha ulimi siyo kutibu?

Katika hatua nyingine mwandishi ananukuu daktari akisema hata kipande cha ulimi kilichong’atwa kingepatikana “kisingeweza” kushonewa pale kilipokatwa.

Pia, mwandishi huyu; hakumuuliza daktari kwa nini kipande cha ulimi hakiwezi kushonewa. Kwa hiyo wasomaji wanabaki gizani.

Mwandishi anaandika kuwa mng’atwa, kwa vile “… Alikuwa hawezi kusema,” alitoa maelezo “kwa maandishi.” Hapa kuna njia mbili za kuelewa haya. Ama maandishi kuhusu tukio hilo yaliishaandaliwa mapema na kila anayekuja anakuta bango; au mng’atwa alikuwa akiandika kila alipokuwa akiulizwa. Mwandishi hakueleza.

Aidha, wasomaji hawamuoni mng’atwa kupitia andishi hili. Kutaja miaka 24 hakutoshi kueleza muhusika alivyo. Kumbuka kinachomsibu hakihusiani na taratibu na kanuni za “kusetiri” mgonjwa na maradhi yake.

“Maradhi” yanayomkumba yamezingirwa na tuhuma za kufanya uhalifu – kudhuru mwili wa mtu. Mwandishi ana fursa ya kueleza anafananaje – sura ya uso, umbile, hali alimokuwa ndani na nje ya hospitali.

Mwandishi haoni yote haya. Kama anayaona hayaelewi. Kama anayaelewa, basi hajui kuwa ni sehemu ya taarifa muhimu juu ya tukio hili; na hajui kuwa ni wajibu wake kuandika kinachoeleweka.

Mwanamke kung’ata ulimi wa mwanaume na kuondoka na king’atwa – cha urefu wowote ule – au mwanaume kufanya hivyo, hakuhitaji mwandishi kuweka vionjo vya nyongeza.

Tukio lenyewe ni makao makuu ya vionjo na limeshiba michomo ya hisi. Unaweza kupata njia nyingi za kulisimulia, tena bila kuweka mihemuko binafsi. Maswali yote niliyouliza hapo juu yanathibitisha kuwapo upungufu kitaaluma. Yanaonesha uandishi wa “kutupia-tupia” na bila kina na ukame wa fikra. Vilevile, maswali hayo yanaonesha kuwa mwandishi ama amedharau, amepuuza au ameshindwa kutumia hojaji ili kupata elimu na maarifa kwa ajili yake na walengwa.

Badala yake ameandika anachotaka mahali palipohitaji kauli ya mtaalamu. Amepoteza fursa ya kuvuna na kusambaza mbegu sahihi. Yote haya ni matunda ya kuandika na kufanya uamuzi bila kufikiri. 0763 670 229