Kiswahili kisiachwe nyuma kuelekea uchumi wa viwanda

Muktasari:

  • Kiswahili ni lugha inayotumika hapa nchini. Watu wengi wanaifahamu na ndio asili ya watanzania na pengine hutumika kama utambulisho nje ya nchi.
  • Wataalamu wa lugha wameandika Kiswahili kuwa inayokadiriwa kutumiwa na watu zaidi ya milioni 100 duniani kote.

Mawasiliano ni nyanja muhimu katika kupiga hatua ya kimaendeleo endapo watu au jamii ya sehemu moja kuzungumza lugha wanayoielewa.

Kiswahili ni lugha inayotumika hapa nchini. Watu wengi wanaifahamu na ndio asili ya watanzania na pengine hutumika kama utambulisho nje ya nchi.

Wataalamu wa lugha wameandika Kiswahili kuwa inayokadiriwa kutumiwa na watu zaidi ya milioni 100 duniani kote.

Katika sehemu mbalimbali duniani vipo vyuo vinafundisha lugha hii. Pia vipo vituo vingi vya utangazaji vya redio na runinga vinavyotumia Kiswahili.

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya viwanda na uchumi wa kati Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) wamekuja na mikakati katika kufikia azma hiyo ya Serikali kupitia Kiswahili kwa kuanzisha miradi mbalimbali yenye lengo la kusukuma ukuaji na matumizi yake.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dk Ernesta Mosha anasema lugha ya Kiswahili ni rahisi kwa kutolea maarifa na kuwafanya wanafunzi kukumbuka na kufikiri kwa haraka zaidi.

Dk Mosha anasema mara baada ya wanafunzi kujiunga na shule za sekondari hutumia lugha ya Kiingereza huwalazimisha kukariri kuliko kuelewa kutokana na kukosa misamiati mingi ya lugha hiyo.

“Maarifa ya kukariri hayawezi kutufikisha mbali hasa tunapoelekea katika mapinduzi ya viwanda na uchumi wa kati,” anasema Dk Mosha.

Dk Mosha anasema kufikia Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati lugha ya Kiswahili itarahisisha ubunifu, kufikiri kwa haraka na namna gani tutapiga hatua ya maendeleo.

Anasema kwa kuwa tayari wawekezaji wanaingia kwa wingi nchini lazima sera za nchi ziwaongoze kutumia lugha yetu kwani itasaidia kukua na kusabaisha mawasiliano kuwa rahisi sana pindi wanapozalisha kuwe na mawelewano baina ya wazawa na wenyeji.

Tataki katika kutekeleza sera ya viwanda na uchumi wa kati mwaka huu katika utafiti wa lugha ya Kiswahili ambao uliendeshwa na kauli mbiu “Utafiti wa Lugha ya Kiswahili kwa Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati” iliandaa miradi mitano katika kufikia azma hiyo.

Miradi hiyo ni kukuza istilahi zitakazo ongeza maneno, kufundisha wageni wanaoingia nchini, simu, kamusi, kupakua vitabu mitandaoni na kuweka wazi Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutumia Kiswahili katika vikao vyake vyote vya Baraza na kufundishia.

Dk Mosha anasema mwaka jana miradi hiyo ilikua mitatu lakini mwaka huu imeongezeka hivyo ni njia ya kupiga hatua katika matumizi na pengine hata mwakani miradi itaongezeka Zaidi.

Hata hivyo, Profesa Kulikoyela Kahigi anasema nchi yoyote iliyopata maendeleo au mapinduzi ya viwanda imetumia lugha yake.

Anasema bila ya kutumia lugha yako maendeleo hayatapatikana kwa urahisi kama watu wanavyodhani kwani silaha moja wapo ya ushindi lugha.

“Watu wanakuwa wabunifu na waelewa zaidi maarifa kwa kutumia lugha wanayoifahamu, kama tutaitumia lugha yetu vizuri tutafika huko kama walivyofanya waingereza na mataifa mengine makubwa,” anasema Profesa Kahigi.

Kuhusu sera ya elimu nchini Profesa Kahigi anasema bado ina makengeza kwani ni moja ya kitu cha kushangaza kuona inaruhusu lugha mbili za kufundishia yaani Kiswahili na Kingereza.

“Sera ya elimu bado ina matatizo hivyo ni lazima tuibadilishe kwanza kama watu wanataka kufundishia lugha nyingine kuna utaratibu wa kufuata,” anasema.

Profesa Kahigi anasema sera zote msukumo wake ni kutoka ngazi za juu hivyo tunasubiri kuona utekelezaji wake japo hata watu wa chini tunapaswa kuisukuma.

Profesa Kahigi anasema juhudi ziongezeke za kupinga wanaokataa kutumika kwa Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia, kutunga na kuandaa vitabu,na kuwashawishi viongozi wetu na majirani kuwa Kiswahili kina uwezo wa kuwaulisha maarifa na kufundishia mashuleni.

Profesa Kahigi anasema juhudi zinaendelea vizuri kwa serikali nahata kwa upande wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kwa upande wake Profesa Mugyabuso Mulokozi anasema suala la viwanda ni uzalishaji na katika uzalishaji kuna uhitaji wa mawasiliano baina ya wazalishaji na wawekezaji.

Anasema katika kila hatua ya uzalishaji kunahitajika mawasiliano hata wageni mwanzoni huitaji wakalimani kutafsri pindi wanapozungumza na wafanyakazi wao ambao wengi ni wazawa na hutumia Kiswahili kama lugha wanayoifahamu.

“Kwa hiyo lugha ni sehemu ya uzalishaji viwandani na ujenzi na inaleta mawasiliano hivyo kuwezesha kufanya kitu wakati mkitumia lugha mnayoelewana,” anasema Profesa Mulokozi.

Profesa Mulokozi anasema kwa kutumia Kiswahili ajira zipo nyingi sio ndani hata nje ya nchi kwani ndani ya Afrika Mashariki zipo nchi sita zinahitaji wataalamu na walimu wa Kiswahili kwa mfano Sudan Kusini.

“Hata kipindi cha aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Gaddafi, aliwahi kuomba walimu 1,000 kwenda kufundisha Kiswahili,” anasema Profesa Mulokozi.

Profesa Mulokozi anasema ndani ya Afrika Mashariki vyuo vikuu ni karibu 130 hizo ni fursa za ajira kwa wataalamu na walimu wa Kiswahili kwenda kufundisha na kufanya tafiti.

Anasema tatizo lipo kwenye elimu hasa shule za sekondari na elimu ya juu bado wanang’ang’ania kutumia kiingereza wakati mazingira yote wanayotumia yako Kiswahili.

“Kwa hiyo elimu inakuwa kama kisiwa ambapo ndani ya mazingira ya Kiswahili ndio unakuta makundi ya watu wanaojiita wasomi hawatumii Kiswahili,” anasema Profesa.

Ni kitu ambacho ni kinyume cha hali popote duniani kwamba una lugha inayotumika kote ila ukiingia darasani unaambiwa haitakiwi lugha ambayo ni yako hapo tatizo ni sera ambayo utekelezwaji wake bado una ukakasi.

Mwaka jana na juzi Serikali kupitia Wizara ya elimu ilitoa sera ya mafunzo ambayo inahitajika kutekelezwa ili kuleta tija na kufikia malengo ya uchumi wa kati na viwanda kwa kutumia ipasavyo lugha ya Kiswahili.