Kuanguka ANC funzo kwa vyama tawala Afrika

Rais Jacob Zuna akiwa na viongozi wenzake wa chama cha ANC. Picha na Maktaba

Muktasari:

Eneo hilo, lenye jina la shujaa wa ukombozi wa Afrika Kusini litatawaliwa siku zijazo si tu na chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), lakini, zaidi ya hayo, litakuwa na meya wa Kizungu.

Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kimeanguka katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa eneo la Nelson Mandela Bay.

Eneo hilo, lenye jina la shujaa wa ukombozi wa Afrika Kusini litatawaliwa siku zijazo si tu na chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), lakini, zaidi ya hayo, litakuwa na meya wa Kizungu.

DA katika eneo hilo, kikiongozwa na Athol Trollip, kilinyakua asilimia 46.5 ya kura zilizopigwa katika Port Elizabeth, jina la zamani la Nelson Mandela ANC kilipata asilimia 41.

Kitu kilichowachoma zaidi makada wa ANC ni Port Elizabeth na Mkoa wa Cape ya Mashariki ni maeneo yaliyokuwa chimbuko la upinzani dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.                                

Kitu kilichowachoma zaidi makada wa ANC ni kwamba Port Elizabeth na mkoa wa Cape ya Mashariki ni maeneo yaliyokuwa chimbuko la upinzani dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Viongozi mashuhuri wa ANC, kama vile Oliver Tambo, Govan Mbeki (ambaye mwanawe, Thabo Mbeki, aliwahi kuwa Rais wa Afrika Kusini) na Raymond Mhlaba, wanatokea huko. Ni katika mkoa huo ndiko alikozikwa Mandela.

Cape Mashariki ndikó wanakoishi watu wa Kabila la Xhosa ambao wengi wao wamekuwa wanachama wa ANC tangu enzi na dahari.

Kwa ghafla Alhamisi iliyopita alichomoza kaburu kwa jina la Trollip mbele ya wapiga kura na akatangaza kwa Kixhosa fasaha kwamba ndiye mshindi wa uchaguzi katika mji huo wa Port Elizabeth.

Alishangiliwa na wapiga kura. Msemaji wa chama cha ANC, Jessie Duarte alielezea kuhuzunika kwake kwa matokeo hayo, lakini alijitoa kimasomaso na kusema kwamba, hata hivyo, ANC imepata asilimia 54 ya kura katika miji na mita yote Afrika Kusini.

Tangu kumalizika mfumo wa ubaguzi wa rangi katika Afrika Kusini mwaka 1994 Chama cha ANC hakijawahi kupata chini ya asilimia 60 ya kura kwenye uchaguzi.

Jambo la kushangaza ni kwamba chama hicho sasa kitakuwa upande wa upinzani katika mabaraza ya miji ya Cape Town, Port Elizabeth, Pretoria na huenda na Johannesburg.

Mji mkuu wa Pretoria, DA iliongoza kwa kupata asilimia 43.5 ya kura, huku ANC ikifuata kwa asilimia 42.2. Katika Jiji la Johannesburg vyama hivyo viwili vilipishana chupuchupu, kila kimoja kikinyakua asilimia 42 ya kura.

Mjini Pretoria, DA kinaweza kuunda mseto na chama cha siasa kali cha “Economic Freedom Fighters” (EFF) ambacho kimejipatia karibu asilimia 10 ya kura. Japokuwa kuna wachunguzi wanaosema kwamba uwezekano huo hauko kwa vile vyama hivyo viwili vinatafautiana katika mambo mbalimbali.

 Katika jiji la Johannesburg, sura itakayochomoza yaweza ikawa mfano wa hiyo ya Pretoria. Katika mji wa Cape Town lengo la ANC la kumuondosha kutoka madarakani meya wa Chama cha DA halijafua dafu. Kwa hakika mara hii DA imeongeza kura zake ukilinganisha na uchaguzi uliopita.

 Umaarufu wapotea

Kwa ngazi ya kitaifa, ANC ambacho wakati mrefu Mandela alikiongoza, kinajionea kinapoteza umaarufu miongoni mwa wananchi. Kimepoteza zaidi ya asilimia nane ya wapigakura tangu uchaguzi wa 2011.

Hamna hata mmoja wa viongozi wa ANC aliyethubutu hadharani kumtaja mwenzake kutokana na hasara kubwa iliyopata chama chao Jumatano iliyopita. Lakini pembeni zilisikia sauti zilizodai kwamba sababu ya ANC kupoteza kura nyingi ni kutokana na kupungua ushawishi wa kiongozi wa chama hicho, Jacob Zuma, ambaye pia ni rais wa nchi.

Zuma amewahi kukabiliana na mashtaka ikiwamo kuwateua mawaziri wa fedha watatu. Kashfa nyingine kubwa aliyokumbana nayo ni matumizi ya dola za Marekani 500,000, fedha ambazo ni za umma. Alitumia kukarabati nyumba yake binafsi katika Mkoa wa KwaZulu-Natal. Mahakama ya katiba ya nchi hiyo ilisema lazima Zuma azirejeshe fedha hizo.

Hata hivyo, upungufu wa Zuma na kushindwa kake kuwashawishi wananchi wa Afrika Kusini, ni jambo ambalo pia linaonekana ndani ya ANC.  Chama hicho kinaamini kwamba kimepewa hakimiliki ya kuitawala nchi hiyo milele.

Zuma alikaririwa akisema, “ANC itatawala hadi  Yesu arejee duniani”. Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe, Alhamisi iliyopita alieleza jinsi ANC ilivyojaa kiburi alipotaja sababu ya chama hicho kupoteza kura nyingi miongoni mwa wananchi.

Alisema, “Wapigakura weusi hawachukulii uchaguzi  kuwa ni kitu muhimu.” Ajabu! Pindi mwanasiasa wa Kizungu angesema maneno hayo, basi angeshambuliwa kwamba ni mbaguzi.

Kiongozi wa DA, Mmusi Maimane, aliyapongeza matokeo hayo na kusema, “Hii inaudhihirisha ukweli kwamba sisi si tu chama cha upinzani, lakini ni chama cha Serikali.”

Alisema uchaguzi huo ulikuwa mzuri kwa demokrasia. Makamu wa rais wa ANC ambaye pia ni makamu wa rais wa nchi, Cyril Ramaphosa, alisema ANC itaiheshimu na kuifuata risala ya wapigakura.

Alisema: “Wazi ni kwamba watu wetu wametuma risala. Tutazisikiliza risala hizo. Sisi ni jumuiya yenye kusikiliza. Tutawasikiliza watu wetu.”

Kuzubaa kwa ANC

Kupoteza kura nyingi ANC katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa kunatokana pia na kuzubaa chama hicho na kila wakati kujaribu kuyadharau na kuyapuuza mafanikio ya DA. Katika uchaguzi huu, chama cha DA kimefaulu  kujivua dhana kwamba bado ni Chama cha Wazungu. Pia, imetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mmusi Maimane.

Mwanadini huyo, mwenye miaka 36  kutoka  Soweto, alipoingia bungeni alibezwa kwamba anachukua amri kutoka kwa mwanasiasa wa Kizungu, Dk Helen Zille, aliyemsaidia kumfikisha katika uongozi wa DA.

Hata hivyo, Maimane amedhihirisha kwamba anaweza kuwavutia wapigakura wa Kiafrika. Maswali yanaulizwa kuhusu mustakbali wa kisiasa wa Jacob Zuma mwenye umri sasa wa miaka 74. Japokuwa bado ana miaka mitatu kumaliza kipindi chake cha urais, lakini inaonyesha amekalia kuti kavu ndani ya chama chake tawala cha ANC.

Pindi viongozi wenzake katika ANC watakapomuona kuwa  ni mzigo kwa chama chao, bila shaka wataachana naye.

Kiongozi huyo atatakiwa kwa haraka kuyapita mawimbi makubwa yanayokabiliwa na Afrika Kusini hivi sasa, si tu katika upande wa siasa, lakini zaidi wa kiuchumi na kijamii.  Ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, uchumi unaokwenda chini kwa kasi pamoja na uhalifu uliopita kiasi katika miji mikuwa ni mambo yanayowashughulisha zaidi wananchi.

Faraja ni kwamba walioshinda na walioshindwa katika uchaguzi huu angalau wamekubaliana kwamba uchaguzi uliendeshwa  kwa haki na uwazi.