Kuhamahama vyama dhana isiyoeleweka

Muktasari:

  • Wapo wanaosema hamahama ni kukosa msimamo, wengine wakisema ni hatua ya kutafuta chama kinachoridhisha nafsi za wahusika au kukidhi mahitaji ya matumbo yao.

Miongoni mwa mijadala mikubwa hapa nchini kwa sasa ni suala la kuhamahama katika vyama vya siasa. Ni suala ambalo wanaolijadili kila mmoja anatoka na dhana yake ambayo tofauti na ya mwenzake.

Wapo wanaosema hamahama ni kukosa msimamo, wengine wakisema ni hatua ya kutafuta chama kinachoridhisha nafsi za wahusika au kukidhi mahitaji ya matumbo yao.

Kusigana kwa mawazo ya watu wanaochambua suala hilo mbali na kuonyesha tofauti ya mawazo ya wachambuzi, pia kunaashiria kwamba hakuna dhana moja inayoweza kuelezea vitendo hivyo ambavyo kwa siku za karibuni vimekuwa ndiyo mchezo wa siasa.

Katika siku za karibuni vyama vya siasa vimegeuka kama mzinga wa nyuki, ni kuingia na kutoka. Kinyume na msemo wa Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kuwa “CCM siyo daladala”, unaweza kusema kwa uhakika na kwa takwimu kuwa vyama vya siasa ni sawa na daladala, watu wanapanda na kushuka kila uchao.

Mjadala wa kuhamahama kwenye vyama umeshika kasi mara tu baada ya makada kadhaa wa upinzani ama kujiunga au kurejea CCM na kupokewa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.

Katika hali ya kawaida, suala la kuhama vyama lisingeibua mjadala kwa kuwa ni haki ya kila mtu kulingana na ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Tanzania inayosema “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi.”

Msisitizo zaidi unawekwa na kifungu cha nne cha ibara hiyo kinachoeleza kuwa kufanya hivyo ni jambo la hiari,

“Bila ya kuathiri sheria za nchi zinazohusika ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote au shirika lolote, au kwa chama chochote au cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa.”

Hata hivyo, licha ya kuwao haki hizo zinazotolewa na Katiba na sheria nyingine zilizopo, mazingira ya watu kuhama vyama na pengine sababu wanazotoa kabla ya kuhama ndio sababu hasa ya mijadala kuibuka ikiwa na mwelekeo unaokinzana.

Nguli wa siasa

Kwa mfano, Mzee Joseph Butiku, aliyekuwa msaidizi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere analitazama suala hilo kama kukosa msimamo.

“Watu wanatoka katika chama chenye msimamo, wanasema msimamo hapo haupo wanakwenda huko. Wakati mwingine wanatoa matusi mengi na kashfa ya huko wanakotoka. Wakifika wanasema huku ndio tumefika kubaya kabisa, wanarudi wanasema huku tulikotoka kumbe pazuri. Mimi nina shaka sana na watu wa namna hii lazima niseme,” alisema Butiku.

Kwa mtazamo wa Butiku, uanachama ni imani na mtu mwenye kuamini kwenye itikadi ya chama fulani hawezi kuhama kirahisi kwenda kwenye itikadi nyingine.

Ndiyo maana anasema hana hakika kama hao wanaorudi CCM wamejitathmini na wanakubaliana na misingi na misimamo waliyoikimbia awali kwenda kwenye vyama vingine.

Mawazo wa Mzee Butiku yanakinzana na mtazamo wa Julius Mtatiro, ambaye katika moja ya safu zake kwenye gazeti hili anasema suala la kuhama vyama lipo na litadumu milele.

Akinukuu kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa “CCM siyo mama yangu” akiwa na maana kuwa CCM haikumzaa, hivyo anaweza kuondoka endapo itaachana na misingi yake muhimu ya kuanzishwa kwake, anajenga hoja kuwa mtu yeyote anaweza kuondoka pake alichokiamini kitabadilika.

Mtatiro ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii na mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa CUF, anasema wanasiasa wanahama kwenye vyama hasa kwa sababu ya madaraka, kwamba mwanasiasa akishakuwa mkubwa na akakosa jukwaa la kutoa uongozi ambao anautaka, atahamia kule ambako jukwaa hilo linapatikana.

Ingawa Mtatiro anayaona mazingira mengine tofauti ya kuhama, anasema mazingira hayo ni nadra.

“Ni wanasiasa wachache sana wanahama chama A kwenda chama B ili kusimamia ajenda au kufuata ajenda. Naweza kusema bila utafiti rasmi, kwamba asilimia 99 ya wanasiasa Afrika huhama kwenye vyama vya zamani kwenda vipya kutafuta nafasi za kuonyesha uwezo wao wa kuongoza na ama kutafuta nafasi za madaraka kwa sababu kule walikotoka wameona hakuna madaraka,” anasema.

Akitolea mfano mazingira ya yaliyomfanya Edward Lowassa kuondoka CCM kwenda Chadema kuwa ni kwa sababu alinyimwa nafasi ya kupata madaraka ndani ya CCM. Na kuwa ndicho kilichomuondoa Raila Odinga kutoka Kanu mwaka 2002 ni kwa sababu alinyimwa nafasi ya madaraka.

Odinga ni mwanasiasa wa Kenya ambaye amekuwa akipambana kwa muda mrefu kugombea urais wa nchi hiyo bila mafanikio.

Mtatiro anahitimisha hoja yake akisema “muogopeni sana mwanasiasa ambaye anasema, mimi nitafia kwenye chama A au B, siasa za kufia kwenye chama fulani zinawezekana kirahisi kwenye dunia ya kwanza.”

Hoja ya Mtatiro ukiiunganisha na matukio ya waliowahi kuhama vyama zaidi ya mara moja, mfano Augustine Mrema kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi kisha TLP au Richard Tambwe Hiza aliyetoka NCCR-Mageuzi kwenda CUF, kisha CCM na sasa Chadema, inafikirisha zaidi.

Mchambuzi mwingine

Hoja hiyo pia inamwibua Mchambuzi mwingine, Luqman Maloto anayeandika katika safu yake kwenye gazeti hili kuwa hata suala la karibuni la Lawrence Masha aliyerejea CCM baada ya kukaa Chadema miaka miwili lisingetokea iwapo angefanikiwa kupata ubunge wa Afrika Mashariki kupitia chama hicho.

Akitumia falsafa ya Mackenzie King, kuwa, “My political party is not my religion and it shouldn’t be yours either”, yaani “Chama changu cha siasa si dini yangu na hakipaswi kuwa dini yako pia.”, Maloto anajenga hoja kuwa kuhama chama cha siasa si jambo la ajabu.

Mackenzie King, yaani William King, alikuwa Gwiji wa siasa za Canada na Waziri Mkuu kwa vipindi vingi zaidi nusu ya kwanza ya Karne ya 20, na Maloto anakumbushia mwongozo aliouweka kwa wanasiasa kuhusu vyama vyao.

Mosi; alisema “chama changu cha siasa si mwokozi wangu, hivyo wanasiasa wasivichukulie vyama vyao sawa na Yesu Kristo.

Pili; alisema “chama changu cha siasa hakinipendi, kwamba vyama huhitaji watu ili vijijenge kuwa vikubwa lakini pale inapobidi chama kinaweza kumjeruhi yeyote kwa ajili ya kutimiza malengo yake”.

Tatu; alisema “chama changu hakina uzima wa milele, hivyo kila mtu kwenye chama ni wa kupita tu, leo upo kesho haupo”.

Katika hitimisho lake, Maloto anasema mwongozo huo wa King ukibebwa na kila mwanasiasa kama kanuni, utaokoa kundi kubwa la watu ambao huwa waaminifu kwa vyama na kujenga chuki na watu hasa pale wanapovihama vyama vyao.

Ukifuatilia mijadala kwenye jamii, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu watu wanaohama vyama utaona ukweli ya hoja hiyo ya Maloto. Wapo watu wanaodhani mtu kuhama fulani ni usaliti, wapo wanaodhani huwezi kuhama hadi ununuliwe na wapo wanaodhani ukipata unafuu katika maisha, biashara au uhuru binafsi lakini uhamie chama fulani.

Ni kutokana na mjadala huo mpana, Njonjo Mfaume anaandika upo umuhimu wa vyama kuchunguza sababu za kuhama na kuchukua hatua badala ya kuzipuuza tu.

Anabainisha baadhi ya sababu zinazotajwa na wahamiaji hao kuwa ni pamoja na muundo na uendeshaji wa vyama usiotoa fursa kwa watu wapya kupenya nafasi za juu, vyama kuhama katika ajenda ya kupambana na ufisadi au chama kukosa mwelekeo na madai ya katiba mpya.

Pamoja hoja zake nyingi, Mfaume anasema hata hivyo kuhamahama vyama kuna gharama kubwa kwa hao wahamaji.

Anasema kutokana na kuhama kwao mara kwa mara kuna namna ambayo watu wanawatazama – kama vile mtu wasioaminika, waongo, wanafiki, wanaoangalia matumbo yao zaidi na wasio msimamo, mtazamo ambao unasawiri kabisa hoja za Mzee Butiku.