Kujitambua, malengo sahihi ndiyo msingi wa maendeleo yako

Muktasari:

  • Changamoto iliyopo ni kujitambua au utambuzi wa kipaji chako. Bila kufanya hivi ni ngumu kuishi maisha ya ndoto yako. Haiba ya utambuzi ni chanzo muhimu cha uchumi binafsi.
  • Kwa tafsiri ya jumla neno utambuzi hutoa picha kamili ya uelewa wa kufahamu kuwa wewe ni nani? Umetoka wapi? Unahitaji nini? Na unaelekea wapi? Baada ya kupata picha ya utambuzi tujielekeze katika namna unavyoweza kukusaidia kubaini fursa na kutumia rasilimali chache ulizonazo kufanikisha mipango mikubwa uliyonayo.

Kila mmoja kati yetu angetamani kuwa na mafanikio yatakayomuwezesha kufurahia maisha yake akiwa duniani. Mafanikio haya hupatikana kwa kuvitumia vyema vipaji vyetu ambavyo kila mtu amejeeliwa na Muumba.

Changamoto iliyopo ni kujitambua au utambuzi wa kipaji chako. Bila kufanya hivi ni ngumu kuishi maisha ya ndoto yako. Haiba ya utambuzi ni chanzo muhimu cha uchumi binafsi.

Kwa tafsiri ya jumla neno utambuzi hutoa picha kamili ya uelewa wa kufahamu kuwa wewe ni nani? Umetoka wapi? Unahitaji nini? Na unaelekea wapi? Baada ya kupata picha ya utambuzi tujielekeze katika namna unavyoweza kukusaidia kubaini fursa na kutumia rasilimali chache ulizonazo kufanikisha mipango mikubwa uliyonayo.

Ukweli kuhusu maisha ya binadamu ni kwamba wote tulizaliwa tukiwa sawa hakuna hata mmoja alizaliwa akiwa tajiri au maskini isipokuwa tulijaaliwa vipaji tofauti. Ukikitambua kipaji chako kisha ukajiwekea malengo ya kutimiza, ndipo utakapoanza kuona mabadiliko ambayo mwisho wa siku yatakuletea mafanikio yako.

Mabadiliko ya mafanikio ndiyo yanayomtofautisha mtu mmoja na mtu mwingine. Habari njema ni kwamba kushindwa ni hali ya muda na unaweza kuibadilisha pale utakapojitambua na kujiwekea mipango mizuri itakayokuletea mafanikio yako unayoyatamani.

Mungu alitugawia vipaji vyetu kila mmoja kwa usawa na bila upendeleo ila utofauti huwa ni wakati gani na kwa namna tunavyotambua na kutumia vipaji vyetu. Utambuzi peke yake bila malengo ni sawa na kazi bure.

Haina maana yoyote kama baada ya kutamua kipaji chako hukufanya lolote kukiendeleza ili kikunufaishe. Haitoshi kusema una sauti nzuri lakini huimbi kwa faida kama wasanii tunaowafahamu. Iwe nyimbo za injili, bongofleva au ngoma za utamaduni.

Wapo wengi watu wa namna hii lakini wachache wanaoweka malengo ya kuwa waimbaji wakumbwa nchini hata kupanga kuwa wa kimataifa hufanikiwa. Mifano ya hili ipo mingi. Tambua kipaji chako kisha panga.

Malengo bila ya utambuzi nayo ni kazi bure vilevile. Hivi vitu viwili vina uhusiano unaoshahabiana kwa ukaribu katika kufanikisha maono na ndoto za maisha yako. Maono ambayo hubeba ndoto za maisha yako pia hutegemea utambuzi wako.

Maono hutoa msingi wa utengenezaji wa mipango ya kutimiza ndoto za maisha yako. Ni hatari kujiwekea mipango nje ya maono katika maisha. Hapana shaka mipango ya namna hii hufeli na mwishowe hufa kwani maana ni sawa na treni kutembea nje ya njia yake, lazima itapinduka tu.

Katika maisha ya kila siku, kuna watu walishindwa kujitambua na kuweka mipango yao mapema ili kutimiza maono na ndoto za maisha yao hivyo kuharibu rasilimali walizonazo. Wapo walioshindwa kuutumia vyema muda wao, marafiki na watu muhimu waliokutana nao au mali walizowahi kumiliki.

Hata kama utakuwa na fedha nyingi kiasi gani, bila ya kujitambua na kuwa na malengo mazuri, kamwe huwezi kutimiza ndoto za maisha yako. Kumbuka, ndoto ni kituo cha treni, maono ni dira ya kufika kituoni wakati kujitambua ni barabara ya kuelekea kituoni na malengo mazuri ni uangalizi wa safari yako wakati fedha ni mafuta kwenye safari hiyo.

Kuwa na fedha ni vizuri lakini si muhimu wala si hitaji la kwanza katika hatua ya mafanikio. Utambuzi ndiyo hatua muhimu ikifuatiwa na kuweka malengo mazuri kwa kutumia rasilimali ulizonazo vizuri. Kwa hiyo basi ili utumie rasilimali chache katika kutimiza malengo makubwa, sharti la kwanza na muhimu, jitambue.

Kwa kujitambua, itakusaidia kupata wazo litakalokusaidia kutengeneza maono ya kutimiza ndoto za safari ya maisha yako. Kumbuka, maisha ni safari na kila siku tuko safarini.

Nje ya kujitambua kuna vurugu na uzurulaji wa kutafuta fedha au fursa na kuishia kutamani huku ukijaribu kila kitu. Hakuna ubaya wa kujaribu kila kitu kipya, lakini bila malengo ya kukuongoza utakavyofanya na kukabiliana na vikwazo vitakavyojitokeza, ni kupoteza muda.

Kw akujitambua, unaweza kugundua kitu au fursa unayoweza kutumia rasilimali chache ulizonazo na kutimiza mipango mikubwa uliyojiwekea maishani mwako ndani ya muda.

Haijalishi lini umejitambua, muda mfupi baada ya hapo mafanikio yako yataanza kuonekana. Wanaowahi kutambua vipaji vyao hufurahia maisha kwa kipindi kirefu ingawa hata wanaochelewa kufanya hivyo pia hufanikisha azma za mioyo yao.

Upo msemo wa siku nyingi kwamba ‘ukimuona kuku kwa mganga ujue kilichomponza ni rangi yake.’ Kataa au kubali, hapo ulipo leo hii kumetokana na sababu fulani ambazo ama unazifahamu au huzifahamu.

Vivyo hivyo, kuwa masikini au kwenye kundi la matajiri kunasababishwa na mambo kadhaa, kubwa likiwa ni kujitambua na malengo maishani. Kuwa mwanafunzi mtiifu wa utambuzi kutakufanya uwe mwalimu mzuri wa mafanikio ya uchumi binafsi siku moja.

Malengo huwa hayaishi. Ukifanikisha moja lazima lizaliwe jingine. Ndiyo maana waliofanikiwa huendelea kufanikiwa kila siku kutokana na ujasiri walionao kutoka kwenye ufanikishaji wa malengo kadha wa kadha waliyojiwekea nyuma.

Muda ni mwalimu mzuri. Miongoni mwa malengo yako yapo yatakayoenda kombo na usiyafanikishe. Hilo likitokea, jifunze ulipokosea na urekebishe utakapokuwa unatekelez ampango mwingine ulionao.