Kuna mwanamke akikupa jukumu la kutunza nywele jasho litakutoka

Muktasari:

Tunaposema mwanamke wa kuendana naye hatumaanishi utafute mwanake mfupi kwa sababu na wewe ni wa kimo hicho, hapana; tunazungumzia kutafuta mwanamke anayeingia kwenye mfuko wako, mwanamke mwenye matumizi ya fedha unayoweza kuyamudu.

Namwambiaga’ mdogo wangu, kama ukiona maisha yako mwenyewe tu yanakuwa mzigo achana na habari za wanawake au kama huwezi kabisa, tafuta mwanamke wa kuendana na wewe; na huu ndiyo ukweli ambao wanaume wengi hatupendi kuusikia.

Tunaposema mwanamke wa kuendana naye hatumaanishi utafute mwanake mfupi kwa sababu na wewe ni wa kimo hicho, hapana; tunazungumzia kutafuta mwanamke anayeingia kwenye mfuko wako, mwanamke mwenye matumizi ya fedha unayoweza kuyamudu.

Mjini kuna mwanamke anaweza akakupa jukumu moja tu la kutunza nywele zake na mtoto wa kiume ukachemsha ndani ya mwezi. Sasa mwanamke wa hivyo ukimng’ang’ania si unaweza ukapata saratani ya ubongo kwa kufikiria jinsi ya kupata pesa ya kumtimizia kila anachokitaka.

Maneno ya hivi tulishawahi kumwambia jamaa yetu Selesini; yeye bwana uchumi wake ndo huu huu wa kina sisi, lakini macho yake ni kama yamerogezewa, yenyewe yanaona wanawake wazuri wenye kupenda mambo makubwa tu, wanawake wa mjini.

Kuna kipindi alikuwa na mwanamke anaishi Tegeta na alituambia kuwa anataka kumuoa kabisa, lakini sisi tunaomfahamu Selesini na tuliokuwa tunamtazama yule mwanamke kwa jicho halisi tulijua kabisa kwamba hiyo ndoa haiwezi kutokea. Kwanza kwa sababu kabla ya siku ya harusi kufika, Selesini angekuwa anaishi kwa kujificha kukwepa madeni ambayo angekuwa anakopa ili kumuhudumia mwanamke.

Kumtoa huyo mwanamke Tegeta mpaka Sinza alipokuwa anaishi Selesini, jamaa yetu ilikuwa inamtoka pesa ya maana, hapo bado ya mapochopocho wakishakutana na usisahau gharama za kumrudisha Tegeta.

Kama marafiki tulikuwa tunamueleza madhara ya kung’ang’ania matatizo namna ile, lakini sina uhakika kama alikuwa hata anatusikia-- yeye alishakufa kuoza.

Mwanzo alikuwa anajifanya nunda, kwamba anao ubavu wa kumhudumia yule mwanamke, lakini maji yalipomfika shingoni mwenyewe alisalimu amri, akanyoosha mikono juu na kuanza kumpotezea taratibu. Ikawa kila mwanamke akiomba wakutane, Selasini anamwambia nakutumia nauli, kisha anachokifanya anaingia ‘google’, anapakua picha ya ‘screenshot’ ya simu inayoonesha ujumbe wa hitilafu kwenye huduma utumaji wa pesa za kimtandao, halafu anamtumia yule mwanamke akimueleza kuwa kila akimtumia pesa simu yake inaandika ujumbe huo.

Mwanamke akiomba atumiwe pesa moja kwa moja kutoka kwa wakala, Selesini anajifanya eneo alilopo hakuna wakala karibu; yaani alitumia njia ya kisasa zaidi kumuelezea mwanamke kwamba penzi lao haliwezekani kuendelea.

Ubishi na ujinga wa Selesini upo kwenye vichwa vya wanaume wengi hasa vijana; wenyewe wanaamini katika mapenzi yanayoonekana katika filamu, yale ya mtoto wa tajiri kumpenda maskini. Sawa, hayo yanawezekana lakini bado nafasi ya mwanaume katika kuhudumia familia inabaki pale pale.

Hatumaanishi kwamba mwanaume bila pesa huwezi kupendwa, hapana. Tunachosema ni kuwa, ukiwa na pesa za kutosha kumudu matumizi ya kawaida ya mkeo, kwa kiasi fulani unampa nguvu ya na jeuri ya kutotetemeshwa na wenzako wanaompenda huko njiani.