JICHO LA DAKTARI: Kuwa makini kuepusha muingiliano wa dawa

Muktasari:

Jingine linaloweza kusababishwa na muingiliano huu ni maumivu makali, usingizi wa ziada, uharibifu wa figo, ini na kushuka au kupanda kwa presha. Mgonjwa anaweza kuhisi mabadiliko ya mapigo ya moyo, kutonesha au kuongeza tatizo la vidonda vya tumbo. Kwa wajawazito, mtoto aliye tumboni anaweza kudhurika iwapo hili litatokea.

Muingiliano wa dawa na nyingine, au dawa na vyakula huipunguzia ufanisi na mgonjwa kutopona kwa wakati. Hilo likitokea mgonjwa huugua kwa muda mrefu zaidi.

Jingine linaloweza kusababishwa na muingiliano huu ni maumivu makali, usingizi wa ziada, uharibifu wa figo, ini na kushuka au kupanda kwa presha. Mgonjwa anaweza kuhisi mabadiliko ya mapigo ya moyo, kutonesha au kuongeza tatizo la vidonda vya tumbo. Kwa wajawazito, mtoto aliye tumboni anaweza kudhurika iwapo hili litatokea.

Ni kawaida mgonjwa kuandikiwa dawa zaidi ya moja ingawa wapo wachache ambao hununua wenyewe na kutumia bila kushauriwa au kuandikiwa na daktari, kitu ambacho siyo sahihi.

Kuna dawa ambazo huingiliana na nyingine iwapo zitatumika kwa pamoja. Cha msingi ni kufahamu kwamba tatizo hili lipo na linaathiri nguvu na ufanisi wa dawa, linaweza kusababisha madhara kwa mtumiaji.

Kwa mfano, kwa wanawake wanaotumia dawa za uzazi wa mpango, vidonge vya majira, kuna dawa zinazoingiliana nazo na huweza kupunguza ufanisi wa dawa za uzazi kiasi cha mwanamke kushika mimba wakati anaendelea kutumia vidonge hivyo.

Mfano mwingine ni kwa wanaotumia dawa za kutibu magonjwa yanayosababishwa na bakteria. Baadhi ya dawa hizo huingiliana na za kutibu fangasi, shinikizo la damu, kuzuia kuganda kwa damu, kisukari, kiungulia au vidonda vya tumbo.

Mifano hii imetolewa kwa lengo la kuelimisha kuhusu muingiliano kati ya dawa na dawa nyingine, na si vinginevyo. Kwa ushauri na maelezo zaidi kuhusu dawa unazotumia na muingiliano wake, pata ushauri wa daktari au mfamasia.

Upo muingiliano kati ya dawa na vyakula, pombe, juisi na matunda. Wapo ambao wamewahi kupewa dawa na kuambiwa wasile aina fulani ya vyakula, matunda au kunywa juisi za matunda ya aina fulani, au vinywaji vingine na wapunguze ulaji wa chumvi, wasinywe pombe.

 Ni vizuri kufahamu; vyakula, matunda, juisi na pombe vina vitamini, madini, mafuta na kemikali nyingine ambazo zinaweza kuingiliana na dawa na kuathiri ufanisi wake. Pia, huweza kuchanganyika na kuzalisha kemikali ambazo hudhuru mwili, kuharibu au kuongeza nguvu ya dawa na kusababisha mgonjwa kuzidiwa hata kufariki dunia.

Kwa mfano, flajili zinaingiliana na pombe na vinywaji vingine vya kimea na kusababisha maumivu makali ya tumbo, kichwa, kunyong’onyea kwa mwili na kujisikia vibaya.

Pombe inaingiliana na dawa nyingine nyingi kama za shinikizo la damu, kisukari au mzio. Matunda kama ndizi na machungwa huingiliana na dawa na kupunguza au kuzidisha nguvu ya dawa hizo.

Pia, mboga za majani, kachumbari au saladi na juisi za matunda huweza kuingilia ufanisi wa dawa. Kwa upande wa chakula, kuna dawa zinashauriwa kutumiwa baada ya kula na nyingine kabla ya kula.

Hapa maana yake ni kwamba ufanisi wake unategemea uwapo wa chakula tumboni, mgonjwa azingatie alichoelekezwa. Pia, maziwa yanaingiliana na baadhi ya dawa, mfano tetracycline.

Upo muingiliano kati ya dawa na magonjwa pia. Asprin, kwa mfano, huingiliana na vidonda vya tumbo na pumu. Kuna dawa nyingine nyingi ambazo huingiliana na magonjwa na kupunguza ufanisi wake, au kuuzidisha ugonjwa.

Kwa mfano, mwenye vidonda vya tumbo akitumia asprin vinaweza kuuma au viwe vikubwa zaidi. Mtu mwenye shinikizo dogo la damu (presha ya kushuka) akitumia vibaya dawa za kuongeza nguvu za kiume, presha yake inaweza kushuka zaidi. Hii ni mifano michache.