Kuwa makini na lugha ya mwili kwa maendeleo binafsi

Muktasari:

Kama unashindwa kupata majibu ya maswali haya usiwe na wasiwasi. Tuko wengi tunaojieleza bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu jambo hili. Wataalamu wa mawasiliano huamini kuwa binadamu huweza kujieleza kwa njia kuu mbili.

Je, unajua katika maisha ya kila siku wakati huwa unajieleza bila maneno, unafahamu kuwa unafanya hivyo mara nyingi zaidi kuliko unavyojieleza kwa maneno? Tena kwa asilimia zaidi ya 90?

Kama unashindwa kupata majibu ya maswali haya usiwe na wasiwasi. Tuko wengi tunaojieleza bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu jambo hili. Wataalamu wa mawasiliano huamini kuwa binadamu huweza kujieleza kwa njia kuu mbili.

Kwa kutumia maneno au bila kutumia maneno. Kitaalamu wanaziita njia hizi mawasiliano ya maneno na mawasiliano yasiyo ya maneno.

Hata hivyo, napenda ieleweke kuwa hapa tunapozungumzia njia ya kujieleza bila kutumia maneno hatukusudii ile lugha ya alama kwa viziwi. Tunazungumzia mbinu ya kutotumia maneno kwa watu wenye uwezo kamili wa kuona na kusikia.

Hivi ni kweli kuwa mtu anaweza kujieleza bila kutumia maneno? Siyo tu kujieleza bila kutumia maneno lakini kufanya hivyo hata bila yeye kukusudia?

Hebu fikiria, umemkuta mtu amekaa mgahawani kwenye meza ya peke yake. Anakula huku anasoma gazeti na hazungumzi na yeyote. Je, kwa kumtazama tu mtu huyu unaweza kupata ujumbe wowote?

Hakika utaweza kustaajabu kwa aina kadhaa za ujumbe ambazo mtaalamu ataweza kupata kutoka kwa mtu huyo hata bila kuongea naye. Kwa kutazama nguo alizovaa utaweza kufahamu kuwa, huyu ni mtu wa daraja gani katika jamii kama wa daraja la juu, kati au chini. Wengine wataweza kutambua tabia yake kama mkarimu, katili au mcheshi kutokana na jinsi anavyotazama watu.

Pia, wanaweza kutambua mambo anayopendelea kufanya kama burudani kutokana na mavazi yake. Wachunguzi walio makini zaidi huweza hata kutambua kama mtu mkakamavu au legelege kutokana na atakavyokuwa amekaa kwenye kiti na pengine namna alivyojiegeza kwenye meza.

Lakini kutokana na kushangaa na kama mara kwa mara anatazama nje kupitia dirishani, inaweza kuonyesha kuwa yeye ni mgeni sehemu hiyo ama la.

Kutokana na mifano hii kuna jambo moja tunajifunza kuwa mawasiliano yasiyo ya maneno yanaweza kuwa yale yanayotendwa na mtu kwa kukusudia, au yale yanayojionyesha yenyewe bila mhusika kukusudia.

Yote yanayobainika kuhusu mtu huyo tuliyemtolea mfano hapo juu hakuyatenda ila yamesomeka kutokana na namna anavyoonekana. Unaweza ukajiuliza kuna aina au njia ngapi za mawasiliano yasiyo na maneno ili kukuza uelewa wako kuhusu suala hili.

Ishara. hii ni njia mojawapo ya mawasiliano yasiyo ya maneno ambayo huhusisha mikono, vidole, kichwa na viungo vingine vya mwili. Kwa mfano; ishara maarufu kote duniani ni watu kushikana mikono wanaposalimiana.

Katika mataifa fulani, wanapo ipandisha mikono juu na kushusha chini ni ishara ya kukubali, yaani ndiyo. Lakini wanapoipeleka kulia na kushoto huku wameshikana ina maana ya kukataa, yaani hapana.

Ishara nyingine ya mikono iliyo maarufu ni kupiga makofi kwa kutumia viganja vya mikono ambayo kwa kawaida maana yake ni kupongeza. Pia, watu hupungiana mkono kama ishara ya kuagana.

Ishara nyingine ni mtu kukiweka kidole chake kirefu cha mkono wa kulia kwenye shingo kama kwamba anataka kuikata. Kitendo hiki kina maana nyingi. Iliyo ya kawaida sana ni kumtisha mtu unaye muonyesha kuwa utamchinja. Pia, watu wengine hufanya kitendo hicho kama ishara ya kuonyesha kiapo. Katika nchi nyingine, alama hii inapotumika ni kama kusema ‘nakupenda.’

Watu wenye uzoefu wa kusoma alama za nyuso wamegundua namna ya kutambua hisia za mtu kutokana na mwonekano wake. Kuwa makini namna ya kutumia alama za uso wako. Akipandisha nyusi juu hadi zikasababisha mikunjo midogo kwenye paji la uso, ni ishara ya furaha au mshangao.

Anapozishusha chini hadi macho yakafumba kidogo ni ishara ya hasira au udadisi, lakini vitendo hivi vyote huambatana na kinywa au mdomo. Mtu anapoacha kinywa wazi ni mshangao na anapofunga kinywa akawa kama ana kitu kinywani mara nyingi ni ishara ya hasira. Katika njia zote anazoweza kutumia binadamu kujieleza bila kutumia maneno, hii ya macho na uso ndiyo ambayo mtoa ujumbe anao uwezo mkubwa wa kuidhibiti. Mtu mwenye hasira anaweza kuonyesha uso usio na ishara yoyote, hivyo kuficha asionekane kama ana hasira.

Wakati mwingine anaweza hata kuonyesha tabasamu la uongo ikiwa atalazimika kufanya hivyo kwa lengo maalumu. Hata hivyo, lazima kuepuka kuchanganya mawasiliano ya maneno na ishara za uso. Unaweza kuonyesha ishara ya uso ambayo haiendani na maneno.

Bondia maarufu wa zamani, Mohammed Ali alikuwa na tabia ya kumtazama mpinzani wake kwa macho makali na uso wa hasira. Alikuwa akifanya hivyo katika vipindi vya mapumziko mafupi katikati ya mapambano ili kumtia hofu na wasiwasi. Mara nyingi mpinzani wake aliingiwa na woga hivyo kumfanya ashinde kisaikolojia wala siyo nguvu.

Kwa taarifa tu unaweza kudhibiti mawasiliano hayo kama unavyochagua maneno ya kusema wakati unapokuwa ukijieleza na ukiweza kuwa mwalimu wa matumizi mazuri ya maumbile yako katika kuwasilisha mradi au fursa yeyote ni mwanzo mzuri kumiliki na kujenga hoja ya uchumi binafsi imara.