TUJADILI UCHUMI: Kwa maendeleo, uchumi ukue kuliko ongezeko la watu

Muktasari:

SIKU YA WATU DUNIANI

  • Siku hii huadhimishwa kila mwaka chini ya uratibu wa Shirika linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).
  • Kwenye maadhimisho yake, shirika hili huwa na ajenda inayotaka mataifa mbalimbali kuipa kipaumbele.
  • Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘uzazi wa mpango, huwezesha  watu kuendeleza taifa’ ikitoa hamasa kwa familia kuwa na mipango thabiti juu ya idadi ya watoto inayohitaji kuwa nao kulingana na uwezo wake na serikali kuchukua hatua stahiki kuboresha huduma za afya.
  • Miongoni mwa majukumu ya UNFPA ni kuhamasisha ajira zenye staha, kuhamasisha uboreshaji wa mazingira ya kazi na kujali afya za wafanyakazi.

Julai 11 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Idadi ya Watu. Suala la idadi ya watu ni kati ya mambo muhimu yanayopaswa kujadiliwa hasa kwa kuzingatia kwamba, pamoja na mambo mengine, linahusu uzazi wa mpango na maendeleo ya uchumi.

Nadharia na uhalisia wa uchumi vinaonyesha kuwapo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati ya idadi ya watu na maendeleo ya taifa. Hii ni kuanzia mtu mmoja mmoja, familia, kaya hata jamii nzima na dunia kwa ujumla.

Tanzania

Mpaka mwezi huu, takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha Tanzania ina zaidi ya watu 56.9 milioni sawa na asilimia 0.76 ya watu duniani. Ni nchi ya 24 kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni.

Asilimia 32.2 sawa na watu milioni 18.3 ya Watanzania wanaishi mjini. Kinachojalisha zaidi maendeleo ya uchumi siyo idadi ya watu tu bali kasi ya ukuaji wake ikilinganishwa na ya ukuaji wa uchumi.  Uchumi unatakiwa kukua kwa kasi kubwa kuliko ongezeko la watu. Hili bado halijatokea Tanzania. Uchumi unapokua, idadi ya watu nayo hukua hivyo tunashindwa kuona faida ya kukua kwa uchumi kutokana na watu waliopo.

Nguvukazi

Kichumi, idadi ya watu ina tafsiri nyingi. Mojawapo ni nguvukazi ambayo ni rasilimali muhimu kuliko zote katika nchi yoyote ikiwemo Tanzania. Nguvukazi inahitajika kwa wingi na ubora ili kuzalisha bidhaa na huduma katika sekta zote. Hizi ni pamoja na sekta ya umma na binafsi.

Nguvukazi inahitajika katika elimu, afya, maji, viwanda, kilimo, mifugo, uvuvi, madini, utalii na kwingineko. Waajiri wa sekta binafsi hata ya umma; ndani na nje ya nchi, wadogo, kati na wakubwa hutizama wingi na ubora wa nguvukazi.

Ubora huu hupimwa kwa vigezo kama vile elimu, ujuzi na uzoefu. Huangaliwa kwa jicho la uwezo wa watu kuzalisha mali kwa tija na faida kubwa.

Pamoja na viwango vya elimu kama vinavyojionyesha katika vyeti vya shule, waajiri makini hutizama ‘ujuzi laini’ unaohusisha kujituma, kujiamini, uaminifu, ubunifu, uthubutu, uwezo wa kufanya kazi na wengine na uvumilivu.

Hivyo, ongezeko la idadi ya watu lazima liendane na ubora ili kuwa na nguvukazi yenye ushindani katika soko la ajira nje na ndani ya nchi. Kupata ubora husika ni lazima kuwapo uwekezaji kuanzia kwa mtu binafsi hadi taifa.

La sivyo, nchi itakuwa na idadi kubwa ya watu wasio na ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira hivyo kushindwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa viwango vinavyokubalika.

Soko

Pamoja na kutoa nguvukazi, watu ni walaji au wateja wa bidhaa na huduma zinazozalishwa na kuuzwa popote. Watengenezaji na wauzaji wa bidhaa na huduma husika hutizama idadi ya watu na uwezo wao wa kununua.

Uchambuzi wa uchumi na biashara katika jambo hili huangalia, pamoja na mambo mengine, kipato cha watu kwa ujumla na kwa makundi mbalimbali. Hutizama tofauti ya kipato na ukuaji wake.

Kwa ujumla wawekezaji na wauzaji hupata faraja zaidi pale idadi kubwa ya watu nchi inapokuwa na kipato angalau cha kati. Hii ni kwa sababu kipato ni mojawapo ya vichocheo vya uwekezaji na biashara katika uchumi wa soko.

Hivyo, idadi ya watu inapaswa iongezeke sambamba na kipato ili ichochee maendeleo ya uchumi. Ongezeko la kipato ili kuweza kununua bidhaa na huduma kwa upande mwingine linategemea mazingira ya ajira kwa maana ya kujiajiri au kuajiriwa.

Uchumi

Idadi ya watu katika nchi huwa neema au mzigo kiuchumi kutegemeana na hali ya utegemezi katika watu wa nchi husika. Taaluma za idadi ya watu na uchumi hutizama utegemezi wa wasiofanya kazi lakini wanapaswa kupata huduma mbalimbali za msingi.

Makundi makubwa ya namna hii ni watoto wasiofikisha umri wa kufanyakazi na wazee waliostaafu. Japo halizungumzwi sana, kundi jingine tegemezi ni lile lisilokuwa na kazi kwani wachache wanaozalisha huduma na bidhaa hulazimika kipato kwa ajili yao na wanaowategemea.

Makundi haya hutegemezwa kwa njia mbalimbali ikiwapo kugawana kipato moja kwa moja au kupitia sera za kikodi. Utegemezi unapokuwa mkubwa ni mzigo kwa uchumi wa nchi. Hivyo, licha ya idadi ya watu kuwa neema, utegemezi hujalisha katika maendeleo ya uchumi.  Nchi nyingi zinazoendelea huwa na idadi kubwa ya watoto wanaotegemea wanaofanya kazi. Katika nchi zilizoendelea idadi kubwa ya wazee ni mojawapo ya vyanzo vya utegemezi.

Huduma za jamii

Uwezo wa nchi kuhudumia idadi ya watu wake hutizamwa kwa namna mbalimbali. Mojawapo ni katika uwezo wa nchi kutoa huduma na bidhaa za umma kwa watu wake.

Huduma hizi ni pamoja na elimu, afya, maji, ulinzi, usalama na miundombinu kwa upana wake. Kwa nchi yenye idadi kubwa ya watu na pato dogo la taifa, changamoto hudhihirika kwenye uwezo wa kutoa huduma hizi kwa wingi na ubora unaotakiwa.

Idadi kubwa ya watu wenye kipato kidogo huweza kusababisha wengi kukosa huduma zinazohitajika hata kuifanya nchi kukopa na kuongeza deni ili kukidhi huduma za msingi. Hivyo ni muhimu ongezeko la watu lizingatie upatikanaji wa bidhaa na huduma zote muhimu za umma.