Kwanini wanasiasa wengi ‘wanapotea’ kirahisi?

Muktasari:

  • Zipo nyakati za furaha na hazidumu bali hukaa kwa kitambo, lakini pia kuna nyakati za maombolezo, na hizo hazidumu japo maumivu yake ni makubwa.

Nimekaa kwa muda bila kuandika, si kwa bahati mbaya, bali kuweka sura ya utulivu kwa kuzingatia taswira ambayo Taifa langu linatengenezewa.

Zipo nyakati za furaha na hazidumu bali hukaa kwa kitambo, lakini pia kuna nyakati za maombolezo, na hizo hazidumu japo maumivu yake ni makubwa.

Naiona sura ya maombolezo yasiyoisha lakini jambo linaloombolezewa limekwisha. Tunashuhudia wale tunaodhani ni majasiri na mashujaa wakitetereka bila kuwashikilia.

Taifa letu liko imara na hata linapojaribu kutikiswa, bado linabaki imara. Ninafurahi jambo moja, Watanzania kwa umoja wetu, tumeamua kutoyumbishwa ingawa makelele ya kutuyumbisha ni mengi na sauti ni kubwa mno.

Tupo katika hali hii ya mpito takribani nusu mwaka sasa, mapambano yetu ya kiuchumi yanaendelea na adui mkubwa anaibuka ndani ya nchi.

Vita ya uchumi haitafanikiwa ikiwa siasa ya nchi haijielekezi katika mapigano hayo. Na ni dhambi kuu isiyosameheka adui anapojiinua kutoka ndani.

Mwanzoni mwa mwaka huu nilipoanza kuandika makala haya, nilijielekeza katika msingi wa kuonyesha ni vipi kama taifa tuko imara na tunasonga mbele. Nilijielekeza katika kukosoa wale waliohitaji uhuru wa kuendesha siasa za harakati hata baada ya uchaguzi mkuu. Lakini, pia nilijaribu kwa kiwango nilichoweza kueleza dhana ya uhuru usio na mipaka na ubaya wake, lakini ubora wa kuuminya uhuru huo.

Sijapata bado mwelekeo halisi wa kimtazamo wa wanasiasa wanajipangaje kukabiliana na hali hii baada ya juhudi zao za heri na hila kugonga mwamba. Ningekuwa mwanasiasa, njia rahisi kabisa ipo, na ningefanya hiyo na siasa ningeendelea nazo. Tuliwahi kuandika kuhusu mabadiliko tuliyoyataka 2015, na kujiuliza sana hivi ni mabadiliko gani tuliyoyahubiri?

Tulijaribu kujifikirisha ikiwa hiki tunachokiona sasa ni sehemu ya kile tulichokiamini kabla hakijafika. Uelewa wa pamoja ni kwamba mabadiliko yana shubiri zake na haziangalii nani ni nani?

Walionuna ni wengi, na wamenuna kwelikweli bila kujali wapo chama chao kinatawala au vyama vyao ni vya upinzani. Hawakutarajia, ndiyo maana mwanzoni walisema ni nguvu ya soda, lakini mwenyewe akawajibu, “soda ikichanganywa na gongo, si soda tena, ni Soda Spesho”.

Tunashuhudia mabadiliko makubwa, na kwa namna hii, tunakubaliana kuwa kwa kipindi hiki tumenuna, lakini tuendako kuna mwanga na faida kubwa kwa Taifa.

Matukio na hali ya siasa

Tunajiweka katika misingi ya uadilifu kwa kutenda, kuzungumza na kuwahimiza wengine watende kwa uadilifu.

Katika mfululizo wa makala haya, tumewahi kuwatahadhalisha Chadema na kuwasihi wajitafakari namna wanavyoendesha siasa zao.

Tahadhali yetu ililenga katika kutoa wosia usio na chuki kwamba yawezekana hawaoni jinsi wanavyopotea, na kwamba siasa za nchi hii wataziaga kwa namna ya ajabu kabisa.

Hatupendi waondoke kwa kuwa wamekuwa taswira ya siasa za kweli za ushindani, ingawa wanakoelekea hakuonyeshi mwanga.

Tunakwenda kama mlevi, hatujui hatua ijayo tutakanyaga wapi. Tunajaribu kujiondosha kwenye mifumo rasmi na kusemea vichochoroni.

Kwa kuwa mbunge ana kinga na ana uhuru wa kusema lolote ndani ya Bunge, basi akisha kulisema bungeni, inatosha huku nje watuachie siye tusio wabunge.

Msingi wa utawala bora ni kuheshimu mamlaka inayokuongoza na kusimamia vema kanuni za mamlaka unayoiongoza au uliyoko ndani yake.

Huku nje ya Bunge, inapotokea walio wajumbe halali wanaleta ya kule ili kutufanya tuwajadili wao, ni utovu wa nidhamu na kwa namna yoyote hauvumiliki.

Tunajaribu kuendesha siasa kwa matukio, na kuyafanya makubwa mno. Yapo yanayofedhehesha Taifa, na zaidi sana, tunavyoyashughulikia yanalifedhehesha zaidi.

Inatia aibu Watanzania kila uchao wanasimama, tena wakiwa ardhi ya ugenini wanalituhumu Taifa lao kwa mambo kadha wa kadha na kisha wanadhani ni jambo la sifa.

Ipo haja ya kuwadhibiti ipasavyo, kwani kuendelea kuwaacha ni kudhoofisha juhudi za Watanzania kwa faida ya wanasiasa wachache.

Taifa letu liko salama na inapotokea wapo watu wanaotumia migongo ya wanaotumia au wanaopambania maisha yao mahala fulani kwa faida zao kisiasa, linaongeza maumivu si tu kwa walioumizwa bali kwa Taifa kwa ujumla. Tanzania si dhaifu kiasi ambacho kinataka kuelezwa, lakini tunapata shida sana pale wanaoituhumu Tanzania ni Watanzania bali wanafanya hayo tu kwa ubinafsi wao.

Wanasiasa wanapotea

Ninaanza kupata mashaka makubwa kwenye tafsiri ya siasa na wanasiasa wetu hasa wa vyama vya upinzani.

Walikuwa imara sana na wenye hoja na kusikilizwa sana, lakini wamepotea. Watanzania wanajiuliza uimara wa wakongwe wa siasa za upinzani, kwa nini hawajarithisha vipawa vile? Wapi akina Mabere Marando wanaobaki mashabiki tu? Wapi akina Jamed Mbatia, wamepotelea wapi?

Nini kimeleta mageuzi makubwa kwa kiwango ambacho hakijapata kushuhudiwa katika miaka ishirini na tano ya siasa za vyama vingi Tanzania?

Ni nani aliyewaroga au madaraka yamewalevya, wameamua kupotea kwa mgongo wa kuyatafuta kwa gharama yoyote?

Tuliwahi kuzipenda siasa za upinzani, na tuliwahi kuona huku ni kujivunia na ni Utanzania mzuri kuwa na wanasiasa wa chama tawala na wapinzani kwa pamoja. Tumefika kubaya kwa kiwango cha juu kabisa kwamba lolote litokealo lazima atokee wa kulaumu na sana atailaumu Serikali.

Ujuzi wa kupanga maneno na ushawishi ni mkubwa. Ni bahati iliyo njema kuwa Serikali na viongozi chama tawala wamekaa kimya, wameacha vijana wakereketwa wajibizane, na huu nauita ukomavu wa hali ya juu.

Ukiangalia kwa umakini na kuunganisha nukta, utaona ni kwa namna gani upinzani umerudi nyuma na umejipoteza kabisa kwenye siasa za Taifa hili.

Tumebaki na wanasiasa wachumia matumbo yao, na watu makini wamenyamaza au kunyamazishwa na hali ikiendelea hivi, sina shaka mfumo wa vyama vingi utakufa wenyewe.

Chama cha Mapinduzi mwaka 1992 kilikuwa na umri wa miaka 15, miaka ishirini na tano baadaye kina miaka arobaini. Wapinzani kwa umri wa sasa wako miaka 10 zaidi kiumri ya CCM ya mwaka 1992, lakini siasa zinazofanywa, ni kama tuko bado kwenye harakati za kuanzisha mfumo wa vyama vingi.

Lazima tukubaliane kukua na kama hatukui tutakuzwa, na kwa hakika sasa tunakuzwa.

Maombi kwa Lissu

Kila binadamu ana utu, kila utu hujali utu nami kwa ubinadamu wangu najali utu na kwa namna ya pekee namtumia salamu zangu Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki.

Najua kwa sasa yuko na hali mbaya, lakini namuombea kwa Mwenyezi Mungu amjaalie heri na ampe uponyaji ili arejee kwenye majukumu yake.

Nimejawa na huzuni na masikitiko kwa jinsi tukio la kihalifu kudhuru maisha ya Lissu lilivyochukuliwa.

Uongo na chuki vimejengwa na kuenezwa sana. Na wasio na haya wameamua kumfanya Lissu kuwa daraja lao.

Matukio kama haya yanatokea sana duniani na hata Tanzania yamekwishatokea, na si vema kuhusisha tukio nzito kama lile na siasa nyepesi za wanasiasa wachovu. Nimesikitika kuona wanaolichukua hili kama daraja lao, wakijitahidi mara wajirekodi, mara waende vyombo vya habari vya Kenya, mara watafute kuungwa mkono hapa na pale, cha msingi watafute umaarufu wao.

Na niseme tu, hawa wakishafanikiwa katika harakati zao hawatamhitaji tena Lissu. Nampa pole Lissu kwa sababu wakati yeye anahangaikia roho yake kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, wajanja wapo nje wanahangaika usiku na mchana kutafuta nguvu yao kisiasa kwa kutumia mgongo wake.

Wanajua, umahiri wa Lissu ulianza kuwaondoa katika siasa, ndiyo maana unaweza kumsikia mmoja anajieleza eti anafuatiliwa sijui na wengine wanafuatiliwa.

Niwaombe Watanzania, tuwe watulivu katika kipindi hiki cha upotoshwaji. Niwasihi kwa majina yote ya babu zetu, kwamba kwa wakati huu tunahitajika tuwe wamoja kumwombea Lissu ili arejee kwenye majukumu yake.

Na roho yangu iungane na ya Lissu na tuambizane, akirejea asitake kudanganywa kutafuta maadui ambao ataikuta orodha yake imeandaliwa na wapiga dili, atafute rehema na roho ya msamaha, asipofanya hivyo atakutana na mambo ya ajabu.

Falesy Kibassa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa. Simu: +255716696265/ [email protected]